Kumekucha Huko.. Freeman Mbowe Amuomba Rais Samia Kuunda Tume ya Maridhiano - EDUSPORTSTZ

Latest

Kumekucha Huko.. Freeman Mbowe Amuomba Rais Samia Kuunda Tume ya Maridhiano


Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume ya Ukweli na Maridhiano, ili kutibu majeraha ya makundi mbalimbali ya kijamii yaliyotokana na alichokisema uongozi usiozingatia sheria na katiba.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Jumatatu Julai 19, Mbowe amesema japo wapo ambao maumivu yao yanajulikana ni viongozi wa kisiasa na wanaharakati, wapo Watanzania kwa mamia wameumizwa ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.

"Wafugaji mifugo yao imetaifishwa, wafanyabiashara wameporwa fedha zao kwenye akaunti, wale wa maduka ya fedha za kigeni nao hawakubaki salama; maduka yalifungwa na fedha zao kuchukuliwa," amesema Mbowe

Amesema japo siyo wengi wanathubutu kujitokeza kuzungumza, lakini ukweli ni kwamba watu wengi wameathirika na kuna haja ya kupewa fursa ya kuzungumza madhila yao ili kuponyesha nafsi zao na Taifa kwa ujumla.

Huku akikumbushia barua yake ya kuomba kukutana na Rais Samia, kiongozi huyo amesema Chadema imesubiri kwa zaidi ya miezi mitatu sasa ahadi ya kukutana na Mkuu huyo wa nchi.

"Tumesubiri kwa zaidi ya miezi mitatu ahadi ya kukutana na Rais Samia kujadiliana kuhusu mustakabali wa Taifa. Wakati tukiendelea kusubiri, tutaendelea na kazi nyingine za kikatiba kama taasisi halali ya kisiasa," amesema

Amesema, katika msimamo huo, Chadema itaendelea kusimamia kile inachokiamini kuwa ni muhimu kwa Taifa bila kujali misimamo ya vyama na makundi mengine ya kijamii.

"Sitaki kuvisemea vyama vingine kuhusu suala la Katiba mpya, lakini Chadema tutaendelea kusimamia hoja ya Katiba mpya kwa mujibu wa sheria," amesema Mbowe


Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz