Jafo akibana kiwanda kilichobadili jina kiholela - EDUSPORTSTZ

Latest

Jafo akibana kiwanda kilichobadili jina kiholela

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Seleman Jafo amewataka wawekezaji kuacha udanganyifu katika usajili wa majina na utekelezaji wa sheria za mazingira.

Jafo ameeleza hayo leo Jumamosi Juni 12, 2021 mkoani Pwani alipotembelea na kufanya ukaguzi katika viwanda vitatu kujionea wawekezaji wanavyotekeleza maagizo ya Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Akiwa katika ziara hiyo amebaini kiwanda cha kutengeneza misumari kufanya udanganyifu kwani kimesajiliwa kwa jina la Shark Tachi na sasa kimebadilishwa jina la umiliki kienyeji na kuitwa Vunjo Afro Company huku kukiwa hakuna taarifa zozote zilizowasilishwa serikalini.

"Nimefika hapa na kukuta kiwanda cha misumari ambacho ofisi yangu inakitambua kwa jina la Shark eti tayari kimebadilishwa kinaitwa Vunjo Afro Company, maana yake huyu mtu amekiuka sheria nyingi na kuna udanganyifu unafanyika dhidi ya Serikali. Niwaonye ambao tunawapa cheti cha mazingira wasifanye mambo ya kienyeji,  kama kuna badiliko lolote ofisi yetu ipate taarifa ya kutosha mapema,” amesema Jafo.

Jafo alionyesha kukerwa na hali ya mazingira aliyoyakuta kwenye kiwanda hicho cha Shark  ikiwemo utiririshaji maji machafu usio salama na utupaji holela wa takataka za vumbi za chuma zinazotokana na misumari .

Ametoa maelekezo kwa meneja wa kiwanda hicho,  Deus Anthony kuhakikisha ndani ya miezi miwili amejenga mabwawa ya kuchuja maji machafu ili yanavyotiririka kwenda kwa makazi ya watu yawe salama na kwamba hadi  Juni 14, 2021 wampe taarifa kuhusu utupaji taka.

Katika ziara hiyo Jafo alikipongeza kiwanda cha kutengeneza mitungi ya gesi cha Lake Cylinder kwa kutunza mazingira na kushauri waendelee kufanya uzalishaji zaidi.





Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz