Hofu yatanda kodi miamala ya simu na laini - EDUSPORTSTZ

Latest

Hofu yatanda kodi miamala ya simu na laini

 


Dar es Salaam. Mapendekezo ya mapato na matumizi ya bajeti ya Serikali yanayoongeza kodi ya miamala na laini za simu yamezua hofu ya kwenda kuwa mzigo kwa wananchi na kupunguza idadi ya watu wanaotumia simu za mkononi.

 Katika bajeti kuu iliyosomwa wiki iliyopita na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali inakusudia kutoza Sh10 hadi Sh10,000 katika miamala ya kutuma na kutoa pesa kwenye bajeti yake ya Sh36.33 trilioni kwenye mwaka ujao wa fedha wa 2021/22.

Pia, alisema Serikali inakusudia kutoza Sh10 hadi Sh200 kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa watumiaji na pendekezo hili litasababisha kuongeza mapato ya Serikali kiasi cha Sh396.30 bilioni.

Kutokana na tozo hizo, kwa mwaka ujao wa fedha, Serikali inatarajia kupata Sh1.65 trilioni kama kodi mpya kutoka kwa watumiaji zaidi ya milioni 53 wa simu za mkononi nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema licha ya uzoefu kuonyesha wananchi hawataepuka huduma hizo za simu, lakini utakuwa mzigo mzito utakaoathiri huduma nyinginezo.

“Kuna utafiti uliofanywa na Synovate mwaka jana ulionyesha bei ya miamala ikiongezeka, mtu hapunguzi matumizi ya hiyo huduma lakini atakwenda kupunguza matumizi ya mahitaji mengine ili apate fedha za kuendelea kutumia vifurushi. Kwa hiyo kodi hizi zitakuwa na madhara kwenye matumizi ya bidhaa nyingine,” alisema Zitto.

Huku akigusia pia ongezeko la kodi kwenye mafuta, Zitto alisema Serikali inakusudia kukusanya zaidi ya Sh2 trilioni kwa mwaka, akishauri fedha hizo kuwekwa kwenye mfuko maalumu.

“Ni fedha nyingi na zinapaswa kupewa uzito huo, kwa sababu mapato ya ndani ya Serikali ni Sh25 trilioni, ambapo mapato ya kikodi ni Sh22 trilioni, mapato ya halmashauri ni Sh800 bilioni na yasiyo ya kikodi zaidi Sh2 trilioni.

“Kwa hiyo Sh2 trilioni kwa zaidi ya asilimia saba ya mapato ya ndani yatatokana na kodi hizi. Ni fedha nyingi na atakayebeba ni mwananchi wa mwisho,” alisema.

Huku akitaka kuwepo mjadala mkubwa wa kitaifa kuhusu tozo hizo, ameitaka Serikali kujitokeza na kukiri kuwa haina fedha ya kukamilisha miradi yake.


“Ni muhimu Serikali ijitokeze kueleza sababu za kuwabebesha wananchi huu mzigo?” alihoji Zitto.

Alitaja miradi ambayo Serikali imelenga kupeleka fedha hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara vijijini, maji vijijini, mradi wa umeme Mto Rufiji na ujenzi wa reli ya kisasa SGR.

“Kumekuwa na uzoefu wa kuchepusha fedha zinazopangwa kwenye miradi husika. Sasa kama tunashindwa kuzuia kodi hii kutotozwa, kwanza itengewe uwe mfuko maalumu kwa kazi hiyo na pili, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) awe anafanya ukaguzi kila miezi mitatu, ili wananchi wajue fedha zao na kama tutaendelea na kodi hizo moja kwa moja?,” aliongeza.

Hofu ya ongezeko la kodi hiyo pia imeelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Hisham Hendi aliyekuwa akizungumza katika mdahalo ulioandaliwa PWC uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, akisema kuanzishwa kwa tozo hiyo ni kuongeza mzigo kwa watumiaji kwa kuzingatia kuwa uchumi wao sio mzuri.

“Kwa sasa kuna hofu iwapo wateja watamudu gharama hizo, kuanzisha tozo ambayo inazidi dola moja (Sh2,300) kwa kuzingatia uchumi wa Watanzania walio wengi ni mzigo,” alisema Hendi.

Hendi aliongeza kuwa: “Kutakuwa na athari kubwa na sekta ya mawasiliano ya simu inaendelea kuzuiliwa kukua.”

Hoja ya Hendi iliungwa mkono wa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Millicom Tanzania (Tigo), Balozi Ami Mpungwe aliyesema tozo mpya zilizopendekezwa zitapunguza uwezo wa watu kutumia huduma za simu.

“Mapendekezo hayo ya kodi yataathiri ukuaji wa sekta ya huduma za simu badala ya kupanuka, sasa itarudi nyuma, hata uwekezaji katika sekta hiyo huenda ukapungua,” alisema.

Alisema si rahisi kupata mwekezaji mpya katika sekta iliyodumaa au ambayo haikui kwa kuwa matamanio ya kila mwekezaji ni kupata faida kutokana na uwekezaji alioufanya.

Alisema hatua hizo zitaathiri jitihada za kuwa na huduma za kifedha jumuishi kwa kuwa miamala ya simu ilichukua nafasi kubwa kufanikisha hilo, lakini pia zinakwamisha uchumi wa kidijitali ambao hivi sasa ndiyo unapigiwa chapuo duniani.

Muswada watua bungeni

Jana Muswada wa Sheria ya Fedha uliwasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni wakati wabunge wakiendelea kuchangia makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 huku hoja ya kodi za simu na majengo zikitawala majadala.

Muswada huo uliowasilishwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Masauni unalenga kutoa nafuu katika baadhi ya maeneo ikiwemo sekta za kilimo, viwanda na biashara huku ukianzisha tozo za simu na majengo kwa kupitia ununuzi wa Luku.

Maeneo mawili yanayogusa watu wengi ya tozo za laini na miamala ya simu na utaratibu mpya wa kutoza kodi kwa njia ya Luku ndio vimezua mjadala.

Hata hivyo, muswada huo unaelekeza kuwa utekelezaji wa kodi za miamala na laini za simu utatungiwa kanuni na Waziri wa Mawasiliano na Maendeleo ya Teknolojia kwa kushauriana na Waziri wa Fedha za Mipango.

Akitoa mchango wake kwenye mjadala wa bajeti, Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi aliwatoa hofu wananchi kuhusu malalamiko ya tozo za miamala ya simu na kwamba kazi ya wabunge ni kuishauri Serikali kuhusu mambo mbalimbali.

“Haya masuala kabla ya kutekelezwa yatakuja katika Sheria ya Fedha. Hivyo, sisi kama ambavyo bajeti ikisomwa tunapewa siku moja ya kuitafakari, wananchi nao wanaitafakari. Na sisi humu ndani tunatoa maoni yetu kulingana na `feelings’ (hisia) za wananchi ambazo tushaziona,” alisema.

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko alisema Serikali itakusanya Sh1.25 trilioni ambazo kwa mujibu wa Dk Mwigulu fedha zitapelekwa katika sekta afya.

Alishauri fedha zote zitakazopatikana kuwekewe uzio (ring fance) na Serikali ihakikishe kweli zinaenda katika sekta hiyo.

Kodi ya majengo

Kwa upande mwingine, Zitto alizungumzia utozwaji wa kodi ya majengo kupitia malipo ya umeme kwa kadiri mtu anavyotumia (Luku), akiitaka Serikali ikiri makosa ya kuhamisha kodi hiyo kutoka Serikali za Mitaa na kupeleka Mamlaka ya Mapato (TRA).

“Wakati kodi ya majengo inachukuliwa kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenda TRA kwa kigezo kuwa mamlaka hizo haziwezi kukusanya mapato mengi, kwa mwaka ule wa 2016 mapato yote kwa nchi nzima yalikuwa Sh45 bilioni,” alisema Zitto.

Alisema baada ya kuhamisha ukusanyaji huo, makusanyo yalishuka hadi Sh7 bilioni kwa mwaka.

“Kwanza Serikali ikiri kuwa ilikosea kutoa kodi hii kutoka Serikali za Mitaa kwenda TRA. Inatakiwa ndani ya Bunge la Bajeti Waziri wa Fedha asimame aseme tulikosea kuchukua hizo fedha na tumeshindwa kukusanya,” alisema na kuongeza:

“Kama itakusanywa kwa Luku, ikusanywe huko huko kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa.”

Akichangia mjadala huo kuhusu kodi ya majengo, Jaffar Chege (Rorya-CCM) alimtaka Dk Mwigulu kutoa ufafanuzi kwa wamiliki waliojenga nyumba zaidi ya moja katika kiwanja kimoja na wanatumia umeme kutoka katika luku moja.

“Sheria inasema nyumba zikiwepo katika kiwanja kimoja kila moja inalipia kodi ya jengo, ukija utuambie ni mpango gani uliowekwa kuhakikisha nyumba zote zinalipia kodi za majengo,” alisema.

Mbunge wa Geita Mjini (CCM) Costantine Kanyasu alisema anaunga mkono watu kulipa kodi ya majengo kupitia Luku, ambapo alisema ni jambo sahihi.

“Jambo hili litaepusha makadirio ya ovyo ovyo yaliyokuwepo mwanzo. Lakini uhakika wa ukusanyaji wa fedha yenyewe. Na duniani kote maendeleo yanakuja kwa watu kulipa kodi. Lazima watu walipe kodi ndio maendeleo yanakuja,” aliongeza Kanyasu


Imeandikwa na Bakari Kiango, Ephrahim Bahemu na Elias Msuya.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz