Aliyewahudumia Uamsho Gerezani Miaka 8 Afunguka - EDUSPORTSTZ

Latest

Aliyewahudumia Uamsho Gerezani Miaka 8 Afunguka

 


Unguja. “Haikuwa rahisi kuwahudumia.” Ni kauli iliyotolewa na mmoja wa watu waliokuwa wakiwahudumia masheikh wa Uamsho katika kipindi chote cha miaka minane ya hekaheka gerezani.

Masheikh hao 36 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka 14, waliachiliwa huru kuanzia Juni 14, mwaka huu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwafutia mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.

Viongozi hao, wakiwamo Farid Hadi Ahmed na Mselem Ali Mselem na wenzao 34 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na makosa ya ugaidi kinyume na kifungu cha 27 (c) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002, wakidaiwa kutenda makosa hayo Januari 2013 na Juni 2014, Tanzania Bara na Zanzibar.

Ilyasa Mohamed Bakari, ambaye ni kiongozi wa wahudumu waliokuwa wakisimamia mchakato wa kuwapelekea chakula gerezani masheikh hao, aliliambia gazeti hili juzi kuwa wamewapeleka hospitali ili kujiridhisha na afya zao kwa sababu walikuwa mahabusu kwa muda mrefu.

“Tunataka waangalie afya zao kwanza kwa sababu ndio jambo la msingi baada ya kutoka gerezani. Baadhi yao walionekana kudhoofika afya, lakini wengine wapo imara,” alisema Bakari.

“Wale wote waliobainika na changamoto mbalimbali baada ya kupata vipimo wanaanza matibabu mara moja ili afya zao zitengemae. Mchakato unafanyika kwa ushirikiano wa familia zote za masheikh hawa pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.”

Akizungumzia jinsi alivyokuwa akiwahudumia, Bakari alisema kwa miaka minane wakati akiwahudumia masheikh hao katika magereza ya Ukonga na Segerea changamoto zilikuwa nyingi.

Bakari, ambaye alikuwa miongoni mwa watu watatu walioteuliwa awali na familia za masheikh hao, alisema mwanzoni walipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wasimamizi wa Gereza la Segerea, lakini kadri walivyoendelea mambo yalibadilika.

Alisema walianza kupata vikwazo kadhaa wakati wa kuingiza chakula gerezani.

“Ndugu walikuwa wanajichanga vyakula vinapikwa pamoja, halafu sisi tunavipeleka kwa zamu, leo anakwenda mmoja na mwingine siku inayofuata,” alisema Bakari.

Hata hivyo, alisema walipata usumbufu zaidi mwaka 2017 walipohamishwa kutoka Segerea kwenda huko Ukonga wahudumu wao hawakuarifiwa.

“Tulipofika Ukonga tuliambiwa lazima tupate vibali vipya maana vibali tulivyokuwa navyo vilikuwa ni kwa ajili ya Segerea tu, kwa hiyo zile ndoo mbili za chakula na nyingine ya mchuzi tulilazimika kurudi nazo na kuzipeleka kwa watoto yatima,” alisem Bakari.

Alifafanua kuwa licha ya baadaye kufanya taratibu za kupata kibali kipya, lakini walibadilisha utaratibu wa kupeleka chakula hicho, walipangiwa wawe wanapeleka Jumamosi na Jumapili badala ya kila siku kama awali.

“Mbaya zaidi tuliambiwa kila mtu mmoja (mahabusu) anatakiwa ahudumiwe na watu watatu tofauti, kwa hiyo ule utaratibu wetu wa sisi tuliokuwa tumeteuliwa kuwahudumia ukabadilika.

“Tulijitahidi angalau kupata watu hao, lakini ilikuwa ngumu kuwapata kutokana na hali ya uchumi wa ndugu kuweza kumudu gharama hizo, tulijitahidi lakini hatukufankiwa kuwapata wote,” alisema Bakari.

Utaratibu mwingine uliobadilika katika Gereza la Ukonga ni ule wa kuingiza chakula chote kilichokuwa kinapelekwa, badala yake walianza kupima chakula kwenye bakuli na kingine kikawa kinarejeshwa.

Mwananchi





Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz