Kuna Sababu za Vipigo Kwenye Mapenzi, Tuzitambue! - EDUSPORTSTZ

Latest

Kuna Sababu za Vipigo Kwenye Mapenzi, Tuzitambue!


 Lengo hapa siku zote ni kupeana elimu, kushauriana na kusaidiana mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano ili mwisho wa siku, wote tuishi mahali salama.

Uhusiano wowote unapaswa kuwa chachu ya furaha, amani na upendo. Kwa kawaida kila mtu anapofikiria suala la mapenzi, huwa akili inampa majibu kwamba ni eneo la kustarehe.


Maisha ya uhusiano ni burudani, ni furaha, ni udugu na kila mmoja anatamani kuona anaishi kwa upendo na mwenza wake. Kwenye furaha, wafurahi pamoja na hata kwenye kuhuzunika, basi wahuzunike pamoja.


Tofauti na matarajio hayo ambayo kila mmoja anayatamani, dunia ya sasa imekuwa ikishuhudiwa machafuko mengi. Badala ya uhusiano kuwa sehemu ya upendo na furaha, imegeuka kuwa sehemu ya karaha.


Pakua App MPYA ya 'EDUSPORTSTZ NEWS-(Lite Version)' Uweze kufurahia Habari zote za Mapenzi; Udaku, Ajira na Michezo kila siku Ipo Google Playstore, Kwa Ku BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD Kwenye Simu yako Utasoma habari zote hata kama hauna MB


Hii imesababisha hata baadhi ya watu kuanza kuamini kwamba maisha ya uhusiano hayana thamani yoyote. Walioko kwenye uhusiano, kwenye ndoa wanatamani kutoka maana upendo walioutegemea haupo tena.


Kutokana na makwazo mbalimbali, baadhi ya watu wamegeuka kuwa kama wanyama. Baadhi ya wanaume wanawapiga wanawake na wakati mwingine pia wapo wanawake wanaothubutu kuwapiga wenza wao, huu ni ukatili ulioje!

Lakini tujiulize kwa nini haya yote yanatokea? Ndugu zangu zipo sababu. Watu mnakutana, mnapendana na kukubaliana muishi kama mke na mume miaka yenu yote, vipi mje mfikie hatua ya kupigana na kutaka hata kuuana?

Mtu ambaye umempenda, ukamuahidi kwamba mtaishi miaka yenu yote pamoja, nini kinakusukuma uchukue panga au kisu kumjeruhi? Hapa ndipo kwenye msingi wa mada yangu, tutafakari kwa kina ili tuweze kuelewa.

 

HASIRA

Ndugu zangu, kinachosababisha haya yote yatokee, huwa ni hasira. Hasira wanasema siku zote ni hasara. Mtu hujikuta amempiga mwenza wake kwa sababu tu ameshindwa kujizuia hasira zake. Analazimika kufanya jambo ambalo pengine hakupanga kulifanya.

 

MAUDHI

Maudhi yanafungamana na hasira. Unamuudhi mwenza wako mara kwa mara ndiyo unazalisha hasira. Hasira zikifika kwenye kiwango cha juu, ndizo zinazalisha tukio la kipigo ambacho kimsingi anayekifanya kitendo hicho anaweza kuwa hajadhamiria.

 

HOFU YA MUNGU

Mnapokuwa hamna hofu ya Mungu kwenye maisha yenu, siku zote ni rahisi sana roho ya kinyama kuwaingia. Mwanadamu mwenzako mwenye roho kama wewe unamuona kama kitu kidogo sana kisichokuwa na thamani na unaweza kukifanya lolote.

 

HULKA

Kuna baadhi ya watu huwa wao kupiga ni kama vile tabia. Yaani ana mkono mwepesi sana kumpiga mwenzake hata kama ametendewa jambo dogo kiasi gani. Yeye kunyanyua mkono ndiyo namna yake ya kumuelekeza mwenzake pale anapoona amekosea jambo.

 

TUJIFUNZE

Ndugu zangu, pamoja na sababu hizo nilizozianisha, ukifuatilia matukio mengi ambayo yanatokea kwenye jamii zetu utagundua kwamba, chanzo chake kilikuwa pengine ni maudhi au kufanyiwa jambo zito ambalo kwa harakaharaka ni ngumu kujizuia.

Ndiyo maana unakuta watu wanaua. Ukifuatilia kwa undani, utakuta aliyetenda kosa na kuua alikuwa akinyanyanyaswa na mwenzake pengine hata kiasi cha kuzaa nje ya ndoa na hata anapoulizwa hajali, anazidi kumpa maudhi mwenzake.

 

TUCHUKUE HATUA

Kwanza tunapaswa kuhakikisha tunapoingia kwenye uhusiano, tuingie na watu sahihi wenye hofu ya Mungu. Baada ya hilo, tuhakikishe tunatambua kwamba wote ni binadamu hivyo kila mmoja ambebee mwenzake mapungufu yake.


Mtangulize upendo zaidi na amani. Muepuke maudhi kwa namna yoyote. Pale inapotokea mmetofautiana, haraka sana mjitahidi mrudi kwenye hali ya kawaida. Jukumu hilo liwe ni la kila mtu kwa sababu linahusu uhai wa penzi na maisha yenu.


Usikubali kuishi na mwenzako katika hali ya maudhi maana ni hatari kwenu wote. Muelekezane kwa upole, muonyane kwa hekima ya hali ya juu. Mumtangulize Mungu katika kila jambo, hakika atawasimamia.


Na mkiona mmeshindwa kuishi pamoja na mmefanya kila linalowezekana imeshindikana, bora muachane kwa amani na kila mtu ayafurahie maisha yake hapa duniani. Kupigana hakufai, kuuana hakuna maana yoyote kwenye mapenzi.



Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz