KAMA UNAMPENDA, MWACHE AJICHUNGE, ACHA KUMFUATILIA! - EDUSPORTSTZ

Latest

KAMA UNAMPENDA, MWACHE AJICHUNGE, ACHA KUMFUATILIA!

KAMA UNAMPENDA, MWACHE AJICHUNGE, ACHA KUMFUATILIA!

HUKO nyuma niliwahi kufanya uchunguzi kwa kuzungumza na baadhi ya wapenzi kuhusu suala la usaliti. Hakika wengi walikiri kujua kwamba kuna uwezekano mkubwa wapenzi wao wanawasaliti lakini wenyewe wanadai ni mambo ambayo wakiyafuatilia sana wanaweza kujikuta wanaachana wakati huenda bado wanapendana.

Msikie huyu;  “Hivi unadhani ni wakati wa kuamini asilimia zote kwamba husalitiwi? Binafsi kwa ninavyomjua mpenzi wangu na huu utitiri wa wanawake wa bei chee huko mtaani, nahisi kwake itakuwa ngumu sana kuvumilia, ila kinachonifanya niwe na amani ni kwamba, ananiheshimu na sijawahi kumfumania.

“Hilo ndilo linalonifanya niwe mpole ila najua hakosi mchepuko na nikimfuatilia najua wazi kuwa nitamfuma, tutagombana na hata kufikia hatua ya kuachana, sasa ya nini hayo?

“Maana ninachojua ni kwamba, ukimfuatilia sana mpenzi wako unatafuta sababu ili muachane, sasa kama hauko tayari muachane ni vyema ukamuamini na kama huko pembeni ana michepuko, ni yeye na Mungu wake,” alisema Sara wa Magomeni jijini Dar.

Mwingine ambaye nilibahatika kuzungumza naye alijitambulisha kwa jina la Salum Koti wa Kariakoo jijini Dar. Huyu anaeleza kuwa, amekuwa akishuhudia wanawake wengi anaowaheshimu akiamini kwamba wametulia na wapenzi wao wakiwasaliti. Hilo linamfanya hata mpenzi wake asimuamini kwa asilimia zote.

"Huwa nawaona wanawake ambao sikuwahi kufikiria kuwa wanaweza kuwasaliti waume zao lakini wanafanya hivyo. Mfano kuna shemeji yangu, mke wa rafiki yangu, anaonekana asiye na ‘time’ na wanaume. “Huwezi kuamini siku moja nilimfuma akiingia gesti. Nilipigwa na butwaa na hapo ndipo nilipoamini kwamba hakuna asiyesalitiwa na kama yupo basi ana bahati sana.”

Hao ni watu wachache tu ambao niliongea nao lakini wengi walikiri usaliti upo tena wanaoongoza kusaliti ni wale ambao wapenzi wao wanawaamini sana.

Kuna ambao walifikia hatua ya kukiri kwamba eti wakibaini wapenzi wao wanawasaliti na wao wanachepuka. Hii yote inaonesha ni kwa jinsi gani mapenzi ya sasa usaliti unachukuliwa kama fasheni. Yaani mama fulani akimuona shoga yake ana mchepuko basi naye anatafuta wake. Huu ni ulimbukeni uliopitiliza.

Suluhisho ni nini? Kutokana na utafiti huu niliofanya ambao naamini hata wewe unakubaliana nao, kuna kila sababu kila aliye kwenye uhusiano kumuamini mwenza wake kwa kiwango kinachostahili.

Sisemi umuamini tu hata kama unaona anakuchezea rafu, lahasha! Muamini pale ambapo una sababu ya kufanya hivyo.

Ukiona dalili za wazi kwamba anakusaliti, ukafuatilia na kugundua ni kweli ana mtu au watu wengine unaochangia nao penzi, hutakiwi kuvumilia.

Mtu huyo atakuwa hana nafasi kwenye maisha yako. Lakini sasa, hii tabia ya kumchunguza na kumfuatilia sana mpenzi wako nayo haifai. Kuna msemo usemao mkimchunguza sana bata huwezi kumla. Kwenye mapenzi nako ni hivyo,  ukimchunguza sana mpenzi wako huwezi kudumu naye.

Hii ni kwa sababu ukiamua kufuatilia sana nyendo za mpenzi wako kuna mambo utayabaini na utashindwa kuendelea kuwa naye.

Kwa maana hiyo unatakiwa kujenga hisia za lazima kwa mpenzi wako ili uwe na amani. Hii kufuatilianafuatiliana kwa wapenzi kunaboa na kama nilivyosema huko nyuma kwamba kufanya hivyo unaweza kumpa hisia mpenzi wako kwamba humpendi na unatafuta sababu za kuachana naye.



Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

Edusportstz