INSHU SIO NDOA,UNAOA AU UNAOLEWA NA NANI? - EDUSPORTSTZ

Latest

INSHU SIO NDOA,UNAOA AU UNAOLEWA NA NANI?

INSHU SIO NDOA,UNAOA AU UNAOLEWA NA NANI?

MOJA kati ya maswali ambayo vijana wengi wanakutana nayo mara kwa mara ni umeoa au umeolewa? Swali hili huwa linawakumba sana vijana hususan wale ambao umri wao unaanza kuwatupa mkono kutoka kwenye ujana, kuelekea kwenye utu uzima au uzee.

Swali hili huwa linachagizwa na lile lingine la ‘una mtoto labda’. Unapokutana na kijana ambaye tayari ameshaingia kwenye ndoa, baada ya salamu na stori mbili-tatu utamsikia akichomekea hilo suala. Tena wengine wanakwenda mbali zaidi kwa zile kauli za ‘umri unaenda, maisha mafupi haya’.

Ndugu zangu, nimeandika makala haya si kwamba sikubaliani na suala la ndoa, ninakubaliana nalo kwa asilimia mia moja kwamba ni jambo la msingi sana. Ndoa ni mpango wa Mungu, mwanadamu anapoutimiza anakuwa amefanya jambo jema maishani mwake na kwamba anakuwa ametimiza mpango huo wa Mungu.

Pamoja na kwamba jambo hili ni la kheri, yatupasa kujifunza sana kwamba mwanadamu yeyote ambaye amezidi miaka 18 ana wajibu wa kulifikiria. Anapaswa kuliweka kwenye akili yake na kulipanga kwamba ni lini anafikiri atakuwa tayari kuoa au kuolewa.

Ukishamalizana na fikra hizo, jambo linalofuatia hapo ni swali ambalo nimeliandika kwenye makala yangu hapo juu; unaoa au kuolewa na nani? Huyo mtu unayetaka kuingia naye kwenye ndoa, ana sifa au tabia gani?

Kwa kawaida binadamu anaweza kubadilika wakati wowote, lakini suala la msingi ambalo nimekuwa nikilizungumza mara kwa mara hapa kwenye makala zangu ni kwamba, huyo ambaye unataka kuingia naye kwenye ndoa ana hofu ya Mungu kweli?

Sikia rafiki, hiki kigezo kiwe cha kwanza kabisa kabla ya vigezo vingine vyoyote unavyovijua wewe. Achana na matamanio ya mwili, lakini afya ya uhusiano wako inabebwa zaidi na mtu ambaye anatambua kwamba Mungu ndiye kila kitu maishani mwake.

Anayetambua kwamba, hakuna changamoto au shida yoyote ambayo itawakumba halafu isiwe na majibu kwa Mungu. Ukimpata mtu wa hivyo, mshikilie na kweli muingie naye kwenye hiyo ndoa maana kinyume cha mtu asiye na hofu ya Mungu ni kisanga.

Nasema ni kisanga kwa sababu waliopitia kwenye changamoto nyingi za ndoa au kuzisikia wanaweza kuwa mashahidi juu ya jambo hili. Kuna watu wengi wanaishi kwenye ndoa, lakini wanatamani dunia ipasuke, waingie ndani kutokana na mateso wanayopitia.

Watu wanabadilika, wanakuwa hatari kuliko hata wanyama wakali wa mwituni. Watu wanauana ili tu kurithi mali. Unapokuwa naye mtu wa aina hiyo hata hiyo ndoa huwezi kuiona maana yake. Utakuwa unawasikia tu rafiki au majirani zao wakifurahia maisha ya ndoa wakati wewe unateseka mwanzo mwisho.

Ndugu zangu, kelele za watu kuhusu suala la ndoa zisikupe presha. Zichukulie kama chachu ya kukuimarisha wewe uelekee kwenye hatua hiyo kubwa kwenye maisha ya mwanadamu. Jipange vizuri kiakili, mtafute yule ambaye atakuwa sahihi maishani kwa kigezo kile tu, hofu ya Mungu.

Acha kupoteza muda kwa kula ujana, mtazame uliye naye na ufanye uamuzi sahihi maana pamoja na yote, muda nao ni muhimu maishani. Lakini nasisitiza tu, usikurupukie, kama unaona haupo sehemu sahihi, ondoka haraka na utampata mtu sahihi na utafunga naye ndoa.


Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

Edusportstz