SIMULIZI; UKINIKUBALI NAACHANA NAYE TUNARUDI KWENYE NDOA YETU! - EDUSPORTSTZ

Latest

SIMULIZI; UKINIKUBALI NAACHANA NAYE TUNARUDI KWENYE NDOA YETU!

Nilirudi nyumbani nikiwa nimechelewa kidogo, ingawa sikupanga kurudi na nilishamuaga mume wangu kuwa nitalala kwa Mama lakini ilinilazimu kurudi kwani Mama alilazwa hospitalini na Dada yangu alichukua zamu ya kulala nayeye kwa siku hiyo kwani kesho yake mume wake alikua anasafiri hivyo asingeweza. Mimi nilirudi nyumbani, ulikua usiku wa kama saa mbili hivi, nilipanda bodaboda mpaka nyumbani, kufika nilisukuma mlango wa geti na kuingia ndani.
Niliingia na kwenda moja kwa moja mpaka chumbani, mume wangu hakuepo lakini nilimuona mwanangu wa miaka miwili kalala, nilishangaa kidogo kwani mara nyingi huwa tunamlaza katika chumba chake lakini nilidhani mume wangu kaamua kumlaza pale. Nilitoka na kuanza kumuita binti yangu wa kazi, niliita mara mbili lakini sikusikia mtu akiitika, niliamua kumfuata chumbani kwake.
Kabla ya kufungua mlango nilimuona mume wangu akitoka, alikua kavalia boxer, shati kashikilia mkononi jasho linamtoka. “Hajisikii vizuri nilikua namuangalia!” Aliniambia bila hata ya kunisalimia. Sikutaka hata kuingia ndani kwani nilijua kilichokua kimetokea, ile haikua mara yangu ya kwanza kumfumania mume wangu na binti wa kazi, nilishamfumania kwa zaidi ya mara tano na katika mara zote hizo niliwafukuza mabinti wa kazi na kutafuta wengine.
Ninaposema mara tano simaanishi kwamba nina ndoa ya miaka 20, hapana mpaka wakati huo ndoa yangu ilikua ni ya miaka mitatu. Ilikua ni kawaida ya mume wangu kutembea na mabinti wa kazi, tena waziwazi na mara nilipokua nikilalamika aliniambia mimi simhudumii vizuri hivyo kama ninataka aache hiyo tabia basi niache kazi. Aliniambia hawezi kuishi na mwanamke ambaye hatakua nyumbani kwa wakati wote hivyo kama ningekua nyumbani kusingekua na haja ya yeye kutembea na wadada wa kazi.
Siku hiyo nilichanganyikiwa zaidi kwani Mama yangu, mtu pekee ambaye alikua akifahamu matatizo ya ndoa yangu alikua anaumwa, hali mbaya mahututi na hawezi kufanya chochote. Nilijikuta naingia ndani na kuanza kulia tu, nilitamani kumfukuza yule binti usiku uleule lakini sikua na mtu mwingine wa kumuachia mtoto na siku iliyofuata nilitakiwa kwenda kazini.
Usiku nilishindwa kulala, mume wangu hakuomba msamaha na wala hakujali chochote, alikua akiniongelesha kama vile hakuna kilichotokea. Binti wa kazi yeye alikua akilia kwa uoga, nilimuangalia bila kummaliza, alikua ni binti mdogo wa miaka 16, mwili hana tena nilimchagua mdogo mdogo kabisa nikiamini kuwa mume wangu hawezi kumtamani. Kuna wakati nilimkasirikia lakini mara nyingi nilimuonea huruma kwani niliona kama vile kabakwa.
“Dada leta mtoto nimbembeleze!” Aliniambia, nilikua nimembeba mtoto analia na mimi ninalia, wote ni kelele hakuna mtu wa kusikilizana, ulikua ni usiku wa kama saa sita hivi, mume wangu nilimuacha chumbani kalala anakoroma hata hajali kama mtoto analia na Mama yangu kalazwa hospitalini. Nilimuangalia yule binti na labda niseme katoto na kushindwa kummaliza. Niliduwaa tu akamchukua mtoto mikononi mwangu na kumbembeleza mpaka kunyamaza, akalala mimi nikiwa nimekaa palepale kama vile sijitambui.
“Alisema kama nisipokubali ataniua na hakuna mtu ambaye atakuja kuniokoa kwani hata wewe unajua…” Yule binti aliongea, machozi yalikua yanamtoka na kwa mara ya kwanza sikumuangalia kama mke mwenzangu, mwizi wa mume wangu, nilimuangalia kama binti aliyebakwa. Wakati nikiwa katika hali ile, usiku uleule nilipokea simu, ilikua ni ya Dada yangu yule ambaye alikua hospitalini akimuuguza Mama.
Mama alikua amefariki dunia usiku ule na alikua ananipa taarifa. Nilizidi kuchanganyikiwa, nilimuamsha mume wangu na kumuambia lakini hakuonyesha kujali “Sasa unaniambia hivyo unataka mimi nifanyeje? Unataka nikamfufue!” Aliongea kwa hasira na kurudi kulala, sikua na namna zaidi ya kusubiri mpaka ausbuhi na kwenda nyumbani, mume wangu alikuja baadaye mchana na kujishaua kutoa pole akijifanya kujali, niliumia sana lakini nilivumilia.
****
Baada ya mazishi ya Mama mume wangu alizidisha vituko, alikua anataka niache kazi, kila siku ilikua ni vipigo, anatembea na wanawake mbalimbali, anapigiwa simu usiku na matusi kila siku. Nilitaka kuondoka lakini baada ya kifo cha Mama sikua na sehemu ya kwenda, niliwaza kwenda kupangisha chumba mjini na kukaa na mwanangu lakini kabla ya kufanya hivyo niligundua kuwa nina ujauzito wa mtoto wapili.
Hapo nililazimika kubaki na mume wangu alinilazimisha kaucha kazi, nilikataa sana lakini mwisho wa siku ili kuepuka manyanyaso na nikiamini kuwa mume wangu atabadilika niliacha kazi, nikamfukuza binti wa kazi na kubaki mwenyewe. Niliamini nitamfurahisha mume wangu na yeye kubadilika lakini wapi, alizidi kuchelewa kurudi, alikua hakai nyumbani, anabadilisha wanawake kama kawaida yake.
Kila nilipoongea naye alijifanya “Mimba yako hainitaki ngoja ukijifungua nitaacha!” Hakunigusa tangu mimba ikiwa na miezi mitatu mpaka kujifungua, hata nilipojifungua basi hakuna kilichokua kimebadilika, mateso yalikua ni yaleyale, hata mtoto alipokua mkubwa mume wangu hakubadilika, mbaya zaidi nilikua nimeshaacha kazi hivyo alizidi kuninyanyasa na kunitukana karibu kila siku.
Aliacha kuhudumia familia, nilikaa mwaka mmoja nyumbani sina kitu, zaidi ya chakula ambacho nacho alikua akitoa kwa mbinde hakuna kitu chochote alichokua akinihudumia. Niliishia kulia tu kila siku, kila nilipokwenda kuomba ushauri niliambiwa vumilia, ndugu zake walianza kunichukia wakisema kuwa namzushia mtoto wao uongo, walinipa majina mengi na kunitenga kabisa, hata wanangu waliwachukia na kuwa nyanyapaa.
Siku moja nilikua nyumbani naumwa, tangu asubuhi yake nilikua na homa, nilienda hospitalini na kuandikiwa Dawa lakini sikuwa na hata Shilingi kumi, nilimpigia simu Dada yangu ambaye alinitumia pesa, mume wangu alikua na siku mbili hajarudi nyumbani, nilishampigia simu na kumtumia meseji nyingi lakini hakujali, jioni yake alirudi, ilikua kama saa kumi na mbili hivi lakini alikua tayari ameshalewa.
Sikua na nguvu hata ya kugombana naye, baada ya kutenga chakula na kuwalaza wanangu niliingia chumbani kulala. Ilikua mapema kabisa wakati napanda kitandani kama saa mbili hivi, mume wangu bado alikua ndani lakini pombe zilikua zishamuishia kidogo. Aliponiona nimelala alikuja kitandani na kuanza kunishikashika, nilimuambia kuwa mimi naumwa aniache lakini hakutaka, alisema ananitaka.
Alinivamia pale na kuanza kuniingilia kinguvu, nilitamani kumuondoa katika mikono yangu lakini nilishindwa, alinizidi nguvu na sikuweza hata kupiga kelele kwani ni mume wangu. Hakuishia tu kufanya mapenzi kawaida na mimi, hapana alianza kunilazimisha na kuniingilia kinyume cha maumbile, ilikua ni mara yangu ya kwanza kuona upande wa pili wa mume wangu, aliniingilia kwa nguvu, pamoja na maumivu makali lakini hakujali.
Aliniingilia mpaka nilipoanza kutokwa damu ndipo alinyanyuka na kuondoka, alinaicha pale, alienda na kukaa kama siku tatu. Mimi nilikua ndani tu naugulia, niliona aibu hata kumuambia Dada yangu, sikumuambia mtu yeyote, nilijiuguza mpaka kupona. Aliporudi siku ya tatu alijifanya kuniomba msamaha. Aliniambia ni pombe, aliongea mambo mengi na kuahidi kubadilika, sikuwa na hamu hata ya kumuona lakini nisingeweza kuondoka kwakua sikuwa na kazi na sikuwa na pakwenda.
Sikua hata na uamuzi wa kumsamehe lakini ilinibidi kuvumilia. “Hiyo ndiyo sababu mimi nachepuka, ungekua unanipa mwenyewe wala nisingechepuka…” Aliniambia, alikaa kama siku mbili ananibembeleza tufanye tena mapenzi kinyume na maumbvile lakini nilikataa, alipoona sitaki tena alinilazimisha tena kinguvu. Kwake nilikua kama mtumwa hivyo nilijikuta nakubaliana na kila kitu, ulianza kuwa kama mchezo wake kunifanyia vile kila siku.
Nikiri tu kuwa baada ya muda nilizoea na kwakua mume wangu alibadilika kidogo, akaacha kunionyesha dharau, kila mara akininunulia zawadi, alihudumia familia niliona labda kweli ndiyo sababu alikua anachepuka hivyo nikawa namkubalia tu. Tuliendelea na ule mchezo kwa kama mwaka mmoja tu lakini mume wangu alibadilika tena, hakutaka kunigusa tena, alikua harudi nyumbani na mara kadhaa alikua akiniambia niondoke nikakae kwingine atanihudumia huko huko.
Sikumuelewa, kila siku nilijaribu kujishushjha na kumuuliza tatizo lilikua ni nini mbona nikilikua nampa kila kitu lakini alikataa kuniambia siku moja ndiyo aliamua kuniambia “Umepanuka sana siwezi kuishi na wewe nataka mwanamke mwingine wa heshima wewe hapana tafuta mwanaume mwingine!” Kweli niliumia sana maneno aliyokua akisema nikweli, nilishaanza kuharibika na kwakua yeye ndiyo alikua akiniharibu basi niliamini atanivumilia.
Hakufanya hivyo, siku moja alitoa vitu nnje na kunifukuza mimi na wanangu wawili, sikujua hata naenda wapi lakini yeye alisema anahitaji mwanamke mwingine. Nililazimika kwenda kwa Dada yangu ambaye naye alikua kaolewa, kula nilikaa kwa wiki mbili ambapo shemeji yangu alimuambia Dada hataki kuniona pale, mwanzoni hakumuambia kwanini lakini baada ya Dada kukataa kunifukuza ndipo alimuambia ukweli.
Tabia ya mume wangu kufanya mapenzi kinyume na maumbile ilikua inajulikana mtaani hivyo ni kama kila mtu alikua anajua nilichokua nakifanya nikiwa naye. Shemeji yangu alizisikia na hakutaka niwe karibu na watoto wake, Dada alijaribu kunitetea lakini shemeji hakumsikiliza alimuambia kama ananipenda sana basi niondoke naye lakini yeye hawezi kunivumilia. Akihofia kufukuzwa Dada alinipa hela kidogo na kuniambia niondoke.
Kwetu tumezaliwa wawili tu hivyo baada ya kutoka kwa Dada sikua na sehemu ya kwenda, nilikua ni kama chizi. Baba na Mama walishafariki na hawakutuachia chochote. Nilikata tamaa ya maisha na mara kadhaa nilitamani hata kujiua lakini kila nilipowaangalia wanangu nilihisi kama nitawadhulumu. Mara kadhaa nilitamani kuwapa wanangu sumu na mimi kunywa sumu lakini nilishindwa, kwa hela aliyokua kanipa Dada niliweza kupanga chumba hapahapa Dar, lakini sikua na matumaini yoyote ya maisha.
***
Wakati nikiwa katika ndoa na nilipokua nahudumiwa kidogo na mume wangu nilikua nasoma Makala zako, ingawa kuna mambo mengi ulifundisha na sikuyafuata lakini bado nilipenda kukusoma. Wakati naachika sikua na simu ya kuingia Facebook lakini kwakua nilikua na namba yako basi niliamua kukupigia. Nashukuru pamoja na kufanya ujinga mwingi bado ulinisikiliza na kunishauri, hukuni hukumu kama wengine.
Uliniambia ukweli kuwa kitu ninachohitaji kwasasa ni kwa mimi kuanza kujipanga na kuanzisha maisha yangu mwenyewe, ulinielezea kuhusu ugumu wa kupata ajira na kunishauri kufanya biashara. Nilikuambia sina mtaji lakini hukukubali kulisikia hilo uliniuliza kama nina Shilingi ngapi nikakuambia nina elfu hamsini tu. Ukaniambia kwakua watoto wana sehemu ya kukaa basi fanya biashara yoyote ile.
Uliniambia kwa mtaji wangu ninaweza kuuza hata mayai au kununua Diamond Karanga na kwenda kuuza majumbani kwa watu na mtaani. Pamoja na elimu yangu ya chuo kikuu lakini kwa hatua niliyokua ningeweza kufanya chochote kile, nilichukua kweli ile pesa na kununua Trei la mayai, nikayachemsha nikatafuta chumvi na kuanza kuzunguka nayo, nyumbani nilimuacha mtoto wangu wa miaka mitano akae na mdogo wake wa miaka miwili.
Bahati nzuri majirani walikua wanashinda nyumbani hivyo walinisaidia. Mwanzo biashara ilikua ngumu kidogo lakini karanga zilikua zinatoka kwani kipindi kile ndiyo Diamond alikua anazitangaza sana na zilikua mpya, nilianza kuona matunda na kuwa napata mpaka elfu kumi kama faida na siku nyingine elfu kumi natano. Sikuona aibu niliingia hata kwenye maofisi, baada ya kuona karanga zinalipa zaidi niliacha kuuza mayai na kudili na karanga peke yake.
Lakini pia uliniambia nisikubali kulea watoto peke yangu, uliniambia kwenda ustawi wa jamii, huko nilienda kweli, mume wangu aliitwa lakini hakwenda ukanishauri nimfuate ofisini ambapo alikasirika sana lakini sikujali, alikuja kunipiga ila kwakua nilishachoka nilienda Polisi, nikamchukulia RB na kweli alikamatwa, alikaa ndani siku moja na kuniomba nifute kesi.
Mimi nilimuambia nataka kitu kimoja tu, simtaki yeye bali nataka ahudumie watoto wake la sivyo sitaacha kwenda ofisini kwao kumsumbua hata kama atakua ananipiga kila siku basi na mimi kila siku nitaenda Polisi. Tulikubaliana akawa anatuma laki moja kwa mwezi, hazikua zikitosha lakini niliona ni mwanzo mzuri na angalau sasa nilikua na uhakika wa kulipa kodi.
Niliendelea na biahsara ya karanga mpaka mwaka huu mwanzoni, hapo nilipata mtaji wa kufungua kibanda lakini kwa bahati nzuri wakati naendelea na biashara bado nilikua naomba kazi hivyo mwaka huu mwezi wa pili nilipata kazi nyingine ambayo nashukuru Mungu inakipato zaidi. Ni kazi ambayo niliipata kwa kuuza hizi hizi karanga na pia inatokana na ushauri wako Kaka kwani uliniambia huko katika maofisi ninakowauzia karanga basi ndiyo kuna mabosi wangu.
Uliniambia hata kama siwezi kutembea na CV kila sehemu lakini kwa elfu kumi tu ninaweza kutengeneza Business Card zangu, upande mmoja ukawa na mawasiliano ya kuhusu biashara ya karanga na upande mwingine ukawa ni kuhusu elimu yangu na uzoefu wangu hivyo kila nikienda katika ofisi natoa mawasiliano yangu na mtu akisoma kuwa nina Digrii na uzoefu basi naweza kupata kazi.
Kweli kuna Mama mmoja ambaye ni bosi wangu kwa sasa, alikua akinunua karanga kwangu kwaajili ya wajukuu zake. Alipoona kwanza alivutiwa na ubunifu wangu kuwa nauza karanga lakini najielewe mpaka kuwa na Business Card, pili alivutiwa na CV yangu, kulikua na nafasi katika lile shirika na aliniambia niombe, niliomba kama wengine kwani ni shirika ni la nnje nashukuru Mungu alinipigia chapuo nikapata ile kazi.
Nashukuru Mungu kwa kuweza kujuana na wewe, nashukuru Mungu kwakua ulinisikiliza na kikubwa hukuniruhusu kukata tamaa, ni mara nyingi sana nilikua nakupigia simu usiku nalia nimekata tamaa lakini ulinisikiliza na hukukasirika, kila wakati umekua ukisikiliza matatizo yangu na kuniambia ukweli. Wiki mbili zilizopita mume wangu baada ya kuona nina kazi nzuri alitaka kurudi, alikuja kuomba msamaha na kuniahidi kubadilila.
Alituma mpaka wazee na mchungaji aliyetufungisha ndoa, kusema kweli nilijikuta namsikiliza na nilitamani kurudiana naye, kila mtu niliyekua naongea naye aliniambia kuwa nimrudie kwasababu ya mtoto kwani atakua amejifunza. Lakini kwakua wewe ndiyo ulinisaidia niliamua kukuambia nashukuru ulinichana na kuniambia ukweli. “Anataka kurudiana na wewe si kwakua anakupenda bali anaona unafuraha bila yeye, anachotaka ni yeye kuja kuichukua kisha kurudi kukunyanyasa vile vile…”
Kuna kitu kilikua kinaniambia nimpe nafasi ya mwisho na karibu kila mtu alikua ananiambia hivyo. Uliniambia nichunguze kidogo na haikuchukua muda niligundua kuwa bado anaishi na mwanamke mwingine, nilipomuambia mbona anataka kunirudia wakati anaishi na mwanamke mwingine aliniambia “Naishi naye kwakua bado hujanikubali, ukinikubali naachana naye tunarudi kwenye ndoa yetu…” Maneno yake yalinikumbusha maneno aliyoniambia kabla “Ninachepuka kwakua hutaki kunipa mapenzi kinyume na maumbile ukinipa kila kitu nitaacha!”
Sikutaka kurudia tena kosa kwani nilifanya kila kitu alichotaka na bado hakubadilika. Nashukuru uliniambia kuwa mwanaume anabadilika kwakua anataka kubadilika na si kwakua mwanamke kamfanyia kitu flani. Nimekuandikia rasmi na kutaka uandike kisa changu kwakua nimeshafanya maamuzi, nimeanza mchakato wa talaka kwani nataka kuanza ukurasa mpya wa maisha yangu, sina cha kukulipa lakini naamini kwa wengine kusoma kisa changu nao watajifunza wasifanye makosa kama yangu, naomba ufiche jina langu Kaka.
***MWISHO
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz