Habari Kaka Iddi; Juzi nilikua katika mazishi ya rafiki yangu mkubwa wa tangu “O”Level ambaye alifariki kwa ajali ya gari. Tukiwa kwenye mazishi baada ya kila kitu kukamilikaa basi kama familia tulirudi nyumbani wakati watu wengine washaondoka.
Mambo yaliendelea vizuri lakini katika kipindi hicho kila mtu alikua akimbembeleza mtoto wa marehemu wa mwisho ambaye ana miaka minne. Alikua akimbembeleza kula chakula cha usiku, mchana alikula vizuri tu akiwa amechangamka.
Yaani kumuona ulijua kabisa alikua haelewi kilichokua kinaendelea. Lakini usiku alikataa kula, watu walimbembeleza lakini wapi. Alikua akisema hawezi kula chakula mpaka Baba rudi, watu walimuonea huruma kua anamkumbuka Baba yake.
Walimbembeleza sana lakini alikataa, tukiwa wote tumekataa mtoto mkubwa wa marehemu alikuja na kumuambia kula usiogope Baba harudi tena, alikua akiongea kwa kumbembeleza na kabla hata hatujajua nini cha kufanya alimuambia.
Baba amekufa tushamfukia hawezi kurudi tena hivyo kula usiogope. Tulitaka kumzuia kwani alikua akitumia maneno makali kwa mtoto mdogo, tlijua ndiyo atazidi kumkasirisha na kumfanya sile kabisa. Ndipo yule mkubwa kwa hasira alituambia.
Huyu hamlilii Baba bali anaogopa kua akila usiku Kama Baba hajarudi basi akirudi anampiga Mama kwani anamuambia kua hajatufundisha adabu tunakula kabla yake. Alisema kila kosa wanalofanya woa anapigwa Mama yao ndiyo maana mtoto ameogopa na si kufa kwa Baba yake.
Wote tulishikwa na butwa, mtoto yule alikua akiongea kwa chuki na hasira na alionyesha kama alifurahi Baba yake kufa. Unafikiri kuna mtu anajali hata amekufa! Mtu mwenyewe hata chakula alikua haleti lakini ni kumpiga Mama tu hukua kijifanya anatupenda, mnafiki mkubwa.
Aliongea mtoto wa kiume wa marehemu ambaye ndiyo alikua wa kwanza mwenye miaka kama kumi na tano hivi. Kila mmoja alinyamaza kimya, Mama yake alimtuliza lakini kijana alisema, wewe Mama ndiyo ulikua unamuendekeza kila siku unavumilia kupigwa tu, yaani sasa amekufa bado unamuogopa!
Kisha alimgeukia mtoto yule mdogo na kumuambia. Baba harudi tena, kaenda mbinguni Kama Bibi alivyoenda, hata rudi tena wewe kula tu huko hawezi kumpiga tena Mama, kaenda kuchomwa moto na Mungu, aliongea kwa hasira na chuki ya hali ya juu. Kale katoto kaliuliza mara mbili mbili.
Kakamgeukia Mama yake na kumuuliza Mama yake akamuambia nikweli ndipo kakaanza kula bila wasiwasi. Kusema kweli roho iliniuma na kama wengine nilishikwa na mshangao kwani rafiki yangu yule sikuamini hata kama anaweza kumtukana mkewe achiliambali kumpiga.
Alikua mpole sana na mara zote ukiwa kwake alijifanya kuwapenda wanae hata kutoka alikua akitoka na mkewe wanafuraha. Sikujua kama anaweza kufanya vile. Nilikaa na kuwaza sasa kuna maana gani ya maisha kama mtu utachukiwa hata na wanao?
*****MWISHO
No comments:
Post a Comment