NGOMA KUIPASUA KICHWA SIMBA - EDUSPORTSTZ

Latest

NGOMA KUIPASUA KICHWA SIMBA



Hata hivyo tofauti na mashabiki wanavyochukuliwa kwa wepesi mchezo huo, benchi la ufundi na hata mabosi wa Msimbazi wamekuwa wakikuna vichwa wakisaka mbinu za kuweza kumdhibiti mtu mmoja tu pale Yanga.

NAMBA hazijawahi kudanganya kabisa. Pambano la Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga litapigwa Jumatano ijayo pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku mitaani mashabiki wa klabu hizo wanatambiana, Simba wakionekana kuwanyong’onyesha wenzao.


Simba imeonekana kuwa na kiburi kutokana na ubora wa kikosi chao kwa sasa na jinsi watani zao wanavyoonekana wanyonge, ikizingatiwa katika mechi mbili zilizopita baina yao ndani ya mwaka huu, Yanga walilala mara zote.


Hata hivyo tofauti na mashabiki wanavyochukuliwa kwa wepesi mchezo huo, benchi la ufundi na hata mabosi wa Msimbazi wamekuwa wakikuna vichwa wakisaka mbinu za kuweza kumdhibiti mtu mmoja tu pale Yanga.


Mtu huyo wala sio Ibrahim Ajibu kama mashabiki wa Yanga wanavyotambiana mitaani au Amissi Tambwe ambaye amekuwa na bahati ya kuitungua Simba tangu alipohama kimizengwe toka Msimbazi kwenda Jangwani.


Mtu anayeinyima raha Simba ni Mzimbabwe Donald Ngoma baada ya benchi la Ufundi la timu hiyo kuiangalia rekodi yake dhidi ya timu yao na kubaini huyo ndiye mtu ambaye amekuwa akiwanyima raha kila anapokuwa uwanjani kwa sasa.


Rekodi zinaonyesha kuwa, Simba haijawahi kupata ushindi wowote pale Ngoma anapokuwa uwanjani na hicho ndicho kinachowapasua vichwa Msimbazi kusaka mbinu za kuweza kumdhibiti mapema kwani kama hawataweka mikakati, ni wazi wanaweza kulizwa Taifa hiyo Jumatano.


Ngoma alisajiliwa na Yanga miaka miwili iliyopita akitokea FC Platinum ya kwao na Simba na Yanga zimekutana matano, Ngoma akicheza mechi tatu huku akikosa mipambano mingine miwili ya mwisho.


Katika msimu wa kwanza aliisaidia Yanga kushinda nje ndani mabao 2-0 katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2015-2016. Ngoma akifunga bao la kuongoza katika mechi ya marudiano iliyopigwa Februari mwaka jana, jingine likitupiwa na Tambwe.


Katika msimu uliopita wa 2016-2017, akiwa uwanjani Oktoba Mosi, aliifanya Simba kuhenyeka kuchomoa bao dakika za jioni kupitia Shiza Kichuya na kufanya matokeo kuwa bao 1-1, Yanga ikipata bao la utata kupitia Tambwe. Katika mechi ya marudiano ambayo ilipigwa Februari 25, mwaka huu Simba ilishinda 2-1, Ngoma akikosekana uwanjani kama ilivyokuwa katika pambano la nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi ambapo Simba ilishinda kwa penalti 4-2.


Ngoma alikosekana kwenye mechi hizo mbili mfululizo kutokana na kuwa majeruhi, lakini kwa sasa straika huyo aliyeifungia Yanga mabao 25 katika Ligi Kuu Bara tangu alipotua mwaka 2015 na kwa sasa amerejea kwa kasi yake kuliko awali, kitu kilichoifanya Simba kuamua kumwahisha beki wao kisiki, Mganda Juuko Murshid kambini ili kuiongezea nguvu safu yao ya ulinzi kabla ya mchezo huo.


MO ATIBUA


Hata hivyo wakati Yanga wakitabasamu baada ya kubaini kuwa wameiweka Simba kwenye mtego kuelekea pambano hilo, Mwanaspoti limebaini kuwa, uwepo wa Mohammed Dewji ‘MO’ katika amsha amsha za Simba kumewapa mzuka wa kuitibulia Yanga.


Ni kwamba kipindi chote MO Dewji akiwa mfadhili wa Simba na hata alipoamua kujitosa kuipiga tafu timu yake, Wekundu wa Msimbazi haijawahi kupoteza mechi.


Achana na kipindi akiwa mfadhili, hapo juzi tu katika mechi hizo mbili za mwisho baina ya klabu hiyo, MO Dewji aliweka mkono wake na Yanga wakala Taifa na Uwanja wa Amaan Zanzibar, kitu ambacho kama Jangwani hawatakaa sawa watalizwa tena Jumatano kwani MO ndiye kila kitu kwa sasa katika timu hiyo.


SIKIA KINACHOSEMWA


Winga wa zamani aliyewahi kuzichezea timu hizo kwa mafanikio, Ally Yusuf ‘Tigana’ ameweka wazi kuwa, mechi hiyo ya Jumatano itakuwa ya aina yake, kwani ni ya kuwapa ujiko ama kuwaharibia makocha, viongozi na wachezaji, hivyo kila timu itashuka ikiwa na hamu ya kupata matokeo mazuri.


“Mechi hizi ndizo za kuweka rekodi, Shiza Kichuya ameitumia vizuri msimu uliopita na kupata heshima, lakini hakuna anayejua itakuwaje safari hii, ila natabiri litakuwa pambano kali, ila uwepo wa Ngoma, Ajibu na Tambwe, huku Simba ikiwa na kina Okwi na wengine ni ushindani wa hali ya juu,” alisema.


Hata hivyo Ofisa Maendeleo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jemedari Said, alizionya timu zote mbili kutopumbazwa na historia.


“Hizi mechi huja na matokeo ya kushangaza kwa sababu ni zaidi ya kuwa na kikosi bora kwa wakati huo. Unaweza kuwa na kikosi chenye mastaa na hali nzuri kiuchumi na bado ukapoteza mchezo,” alisema.


“Kikubwa timu ambayo itaweza kucheza kwa nidhamu na kufuata maagizo ya benchi la ufundi kwa dakika zote tisini itaibuka na ushindi.”


Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz