UKWELI WAJULIKANA MPANZU HAYUPO KAMBINI KWA SABABU HII

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ameweka wazi sakata la kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Elie Mpanzu, kutokuwepo kambini, akieleza kuwa sababu ni majeraha.

Kauli hiyo imekuja kufuatia taarifa zilizosambaa zikidai kuwa nyota huyo amegomea kujiunga na kambi ya timu hadi alipwe fedha zinazodaiwa kuwa sehemu ya ahadi ya mkataba mpya aliosaini hivi karibuni.

Hata hivyo, Ahmed amekanusha vikali taarifa hizo, akisisitiza kuwa hakuna mgogoro wowote kati ya mchezaji huyo na uongozi wa klabu, bali anaendelea na matibabu baada ya kuumia.

Amesema Mpanzu kwa sasa yupo nyumbani akiendelea kupatiwa matibabu, huku akifuatiliwa kwa karibu na jopo la madaktari wa timu hiyo ili kuhakikisha anarejea uwanjani akiwa fiti.

“Ni kweli Mpanzu hayupo kambini. Yupo nyumbani na jana asubuhi daktari wa timu alimpeleka hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi na baadaye akarejeshwa nyumbani kuendelea na mapumziko,” amesema Ahmed.

Amefafanua kuwa ni utaratibu wa kawaida kwa wachezaji wa Simba wanaougua au kujeruhiwa kutokaa kambini muda wote, badala yake hupatiwa huduma stahiki kulingana na hali zao, ikiwemo kwenda hospitali au kutibiwa wakiwa nyumbani chini ya uangalizi wa madaktari.

Ahmed ametolea  mfano wa Abdulrazack Hamza, ambaye pia amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya muda mrefu, akieleza kuwa mara nyingi amekuwa akienda kambini kwa ajili ya matibabu au kufanyiwa tathmini ya maendeleo ya afya yake inapohitajika.

The post UKWELI WAJULIKANA MPANZU HAYUPO KAMBINI KWA SABABU HII appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/QXsgOc6
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post