SINGIDA BLACK STARS WAZIPIGA MKWARA SIMBA, YANGA NA AZAM FC

KLABU ya Singida Black Stars imeendelea kuonyesha makucha yake baada ya kutinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, kufuatia ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Mbeya City, hatua inayozidi kuipa matumaini ya kufanya makubwa msimu huu.

Ushindi huo umeifanya Singida kuweka wazi malengo yake makubwa, ikitangaza rasmi kuanza vita ya kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) msimu ujao, jambo linaloongeza presha kwa vigogo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha wa timu hiyo, Muhibu Kanu, amesema wazi kuwa hawapo kwa ajili ya kushiriki tu bali wanataka ushindani wa kweli, akisisitiza kuwa kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinamaliza katika nafasi mbili za juu au kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho.

Kanu amebainisha kuwa kiu yao ni kuona timu inashiriki mashindano ya kimataifa, huku akieleza kuwa tayari amewahamasisha wachezaji wake kupambana kwa nguvu zote ili kufikia malengo hayo makubwa.

“Sisi tunachohitaji ni timu kushiriki kimataifa… tunataka ubingwa na wachezaji tumeawahimiza wapambane kwa bidii ili kuweka rekodi na historia msimu huu,” amesema Kanu.

Kwa sasa, Singida Black Stars inaonekana kuwa tishio jipya kwa timu kongwe kama Simba, Yanga na Azam FC, ambazo zimezoeleka kupigania nafasi za juu, huku ushindani ukizidi kupamba moto kadri msimu unavyoelekea ukingoni.

Katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, Singida inatarajiwa kushuka dimbani kuvaana na Mashujaa FC mkoani Kigoma, katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali huku kila upande ukihitaji pointi muhimu.

The post SINGIDA BLACK STARS WAZIPIGA MKWARA SIMBA, YANGA NA AZAM FC appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/v6JhebT
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post