UONGOZI wa klabu ya Simba umeweka wazi kuwa haujawahi kupoteza mwelekeo, ukisisitiza kikosi chao kinaendelea kuimarika na kiko tayari kukabiliana na timu yoyote katika michuano iliyopo mbele yao, ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ambaye pia aliwajibu wapinzani wao Yanga kwa kueleza kuwa wao hawajawahi “kujipoteza”, bali wameendelea kubaki kwenye ubora wao huku akiipongeza Yanga kwa hatua wanazodai kufikia.
“Kama wao wamejipata, hongera zao. Sisi hatujawahi kujipoteza, timu yetu ipo vilevile na imeendelea kuwa bora zaidi. Tuko tayari kucheza na timu yoyote,” amesema Ahmed.
Akizungumzia matokeo ya sare mbili walizopata dhidi ya TRA United na Pamba Jiji FC, Ahmed ameeleza kuwa hilo halipaswi kuwapa presha, akibainisha kuwa wapinzani wao walicheza kwa kujituma kubwa.
Amesisitiza kuwa Simba ikipeleka kiwango chao halisi uwanjani, wana uwezo wa kupata matokeo wanayoyahitaji.
“Watu waelewe kwamba zile sare hazimaanishi tumeshuka kiwango. Wapinzani walicheza kwa kukamia, lakini tukiamua kucheza soka letu la kawaida, tuna uwezo mkubwa wa kufanya vizuri zaidi,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa kikosi hicho hakina presha kuelekea michezo ijayo, kwani kinafahamu vizuri ushindani wa ligi na malengo yao msimu huu bado yako palepale.
Wakati huo huo, Simba inatarajiwa kushuka dimbani leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ikimenyana na Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB, wakisaka ushindi muhimu utakaowawezesha kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
The post KUMBE SIMBA HAIJAWAHI KUPOTEA, KAULI YA AHMED ALLY YAZUA GUMZO appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/MqETFcw
via IFTTT
Post a Comment