KIPA namba moja wa Yanga SC, Djigui Diarra, amemaliza adhabu yake ya kufungiwa mechi tatu na sasa anatarajiwa kurejea kikosini katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Alhamis kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Diarra alikuwa akikosa huduma ya kikosi hicho katika michezo mitatu mfululizo dhidi ya Tanzania Prisons, Pamba Jiji na TMA kutokana na adhabu aliyokuwa akiitumikia, hali iliyolazimu benchi la ufundi kufanya mabadiliko kwenye safu ya ulinzi wa goli.
Wakati kipa huyo akirejea, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ally Kamwe, amesisitiza umuhimu wa mchezo huo na kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao, akisema ushindi ni muhimu na unahitaji nguvu ya pamoja uwanjani.
Kamwe amekumbushia pia namna Mbeya City ilivyowapa wakati mgumu katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliomalizika kwa sare, akisisitiza kuwa sasa ni muda wa kulipa kisasi na kuhakikisha pointi tatu zinabaki nyumbani.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Aprili 15 kwenye Uwanja wa KMC, na Kamwe ameongeza kuwa maandalizi ya kikosi yamekamilika kikamilifu, huku wachezaji wakiwa kwenye morali kubwa baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, jambo linaloongeza hamasa kuelekea pambano hilo muhimu.
The post DIARRA AREJEA, KAMWE AIBUA HAMASA KABLA YA MBEYA CITY appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/imUYpRb
via IFTTT
Post a Comment