UONGOZI wa klabu ya Yanga umeweka wazi kuamua kumbakiza Kocha Mkuu, Pedro Gonçalves, ni hatua ya kimkakati iliyolenga kulinda uthabiti wa timu, hasa katika kipindi hiki chenye ratiba ngumu ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Viongozi hao wameeleza kuwa kufanya mabadiliko makubwa kwenye benchi la ufundi kwa sasa kungeiweka timu kwenye hatari ya kupoteza mwelekeo.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, uongozi umeona ni busara kuimarisha benchi la ufundi badala ya kulivunja, ndiyo maana wameamua kumrejesha Abdihamid Moalin ili kushirikiana na Pedro katika kuirejesha timu kwenye ubora wake wa awali.
Hatua hiyo imekuja kufuatia mwenendo usioridhisha wa hivi karibuni, ambapo Yanga ilipata sare tatu mfululizo, hali iliyozua presha kutoka kwa mashabiki waliotamani kuona mabadiliko makubwa, ikiwemo kuondolewa kwa kocha mkuu.
Akizungumzia hilo, Kamwe amesisitiza kuwa uamuzi wa kumbakiza Pedro umezingatia maslahi mapana ya timu.
“Maamuzi ya kubaki na Pedro ni yenye busara zaidi. Tungemtimua na kuleta kocha mpya, tungeibomoa Yanga badala ya kuijenga, hata suala la kumleta Moalin limekuja baada ya kocha mwenyewe kuridhia na kushauri hivyo,” amesema Kamwe.
Kamwe amefafanua kuwa kikao kilichofanyika kilihusisha kwa kiasi kikubwa benchi la ufundi, akibainisha kuwa asilimia kubwa ya maamuzi yalitokana na mapendekezo yao.
Ameeleza kuwa kikao hicho kililenga kupokea na kujadili ripoti ya benchi la ufundi, ambayo pia imeakisiwa katika taarifa iliyotolewa kwa umma.
Kwa upande mwingine, Moalin anatarajiwa kuwasili nchini hivi karibuni na kuanza kazi mara moja kwa kushirikiana na Pedro, wakipanga mikakati ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi.
Kamwe amesema uongozi una imani kubwa na maboresho hayo, akitarajia kuanza kuona matokeo chanya mara tu ligi itakaporejea, ambapo Yanga itaanza na mchezo dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
The post YANGA WAPANGA VITA YA MZUNGUKO WA PILI KIMKAKATI appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/07ErWKu
via IFTTT
Post a Comment