LICHA ya mpinzani wao wa hatua ya 32 ya Kombe la Shirikisho la CRDB, B19, kuwa timu ya daraja la chini, uongozi wa Simba SC umesisitiza kuwa utaingia uwanjani kwa nguvu ileile iliyotumika katika mchezo wa Kariakoo Derby ili kuhakikisha wanapata ushindi.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi hicho kwa sasa kina ari mpya na kinaendelea kujipanga vyema kuelekea mchezo huo wa Jumamosi dhidi ya B19, maarufu kama Mabeberu wa Jiji.
Katika mchezo huo, Simba watakuwa wenyeji kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam, mechi itakayopigwa saa 1:00 usiku.
Ahmed amesema umoja, nguvu na ushirikiano uliodhihirishwa na mashabiki, viongozi pamoja na wachezaji katika mchezo uliopita wa Kariakoo Derby, ni silaha muhimu ambayo wanahitaji kuibeba kuelekea pambano hilo.
“Umoja, nguvu na ushirikiano ambao mashabiki, viongozi na wachezaji wetu walionyesha katika mechi iliyopita ndio silaha tunayopaswa kwenda nayo siku ya Jumamosi dhidi ya B19,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa baada ya mchezo wa Kariakoo Derby uliochezwa visiwani Zanzibar, timu imejifunza mambo mengi chanya na kuyafanyia kazi, hali iliyochangia kufanya kikosi hicho kuonekana kuwa na sura mpya uwanjani.
“Simba mpya imezaliwa pale Zanzibar. Tunachotakiwa sasa ni kuendelea kuwekeza nguvu kubwa katika michezo yetu ijayo ikiwemo huu wa Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya B19 ili kuhakikisha tunasonga mbele kwenye mashindano hayo,” amesema.
Amesisitiza kuwa malengo ya Simba msimu huu ni kutwaa taji la kombe hilo, hivyo wanalazimika kujiandaa kwa umakini mkubwa ili kupata ushindi.
“Hata kama B19 ni timu ya daraja la chini, hatupaswi kuibeza. Tunaiheshimu lakini tunaingia uwanjani kwa lengo la kushinda na kusonga mbele,” ameongeza Ahmed.
Amesema Simba itaendelea kuwaheshimu wapinzani wake wote lakini hilo halitawafanya waingie uwanjani kwa tahadhari kupita kiasi, kwani dhamira yao ni kuendeleza kasi ya ushindi katika michuano hiyo.
The post SIMBA WAFUNGUA VITA KOMBE CRDB, B19 KWENYE MTEGO appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/hYpEaKn
via IFTTT
Post a Comment