IMEELEZWA kuwa Mshambuliaji wa Simba Sports Club, Jonathan Sowah, amejibu tuhuma mbalimbali zilizotolewa dhidi yake na uongozi wa klabu hiyo, akisisitiza kuwa baadhi ya madai yaliyotolewa hayana ukweli na yanahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.
Hivi karibuni uongozi wa Simba ulimsimamisha nyota huyo na kumfikisha kwenye kamati ya nidhamu, ukimpa siku tatu kujibu tuhuma kadhaa zilizokuwa zikimkabili.
Mtoa habari huyo amesema Miongoni mwa tuhuma hizo ni madai ya kukataa kushiriki mazoezi yaliyofanyika Februari 17 kabla ya mchezo dhidi ya Greenland FC, jambo ambalo Sowah amelikanusha vikali.
Amesema nyota huyo alifafanua kuhusu tukio hilo, kwa kusema kuwa licha ya kusimamishwa na kutokuwa na ruhusa ya kushiriki kikamilifu mazoezini au kucheza mechi, alihudhuria na kukamilisha programu ya mazoezi ya “activation session”. Alieleza kuwa baada ya kumaliza programu hiyo, mkufunzi alimruhusu kuondoka kama ilivyokuwa imepangwa.
Kuhusu mazoezi ya ziada yaliyodaiwa kufanyika Februari 22, mshambuliaji huyo amesema kulikuwa na mkanganyiko uliosababishwa na changamoto za usafiri pamoja na kuchelewa kupatikana kwa vifaa vya mazoezi.
Hata hivyo, alibainisha kuwa mazoezi hayo yalifanyika baadaye katika hoteli ya timu, akiwa na baadhi ya wachezaji wenzake pamoja na kocha wa viungo, akisisitiza kuwa kuna ushahidi wa video unaothibitisha hilo.
Amesema akizungumzia madai ya kuchelewa mazoezini Februari 16, Sowah alikiri kuchelewa kwa takribani dakika tano baada ya kulala usingizi bila kukusudia kufuatia kikao cha uchambuzi wa video kilichofanyika awali. Alisema alimjulisha kocha mara moja na kusisitiza kuwa haikuwa tabia ya makusudi.
Aidha, Sowah alipinga madai ya kuchelewa katika mikutano ya timu, akieleza kuwa hajawahi kufanya hivyo katika kipindi chote alichokuwa ndani ya kikosi cha Simba.
Kuhusu tukio la kuvaa jezi tofauti wakati wa safari ya Angola, Sowah alikanusha madai ya kuvaa jezi ya SL Benfica, amesisitiza kuwa alivaa jezi rasmi ya Simba. Aliongeza kuwa hilo linaweza kuthibitishwa kupitia picha na video zilizowekwa kwenye mitandao rasmi ya kijamii ya klabu hiyo.
Pia alizungumzia madai ya kufanya faulo zisizo za kawaida uwanjani, akisema aina ya uchezaji wake wa kuwania mipira ni sehemu ya ushindani wa kawaida wa soka na haukuwa jaribio la makusudi la kuwaumiza wapinzani au kusababisha kutolewa kwa kadi.
Katika hatua nyingine, Sowah alikanusha vikali uvumi wa kupokea fedha kutoka Young Africans Sports Club na Singida Black Stars, akiyataja madai hayo kuwa ya uongo yenye lengo la kumharibia sifa.
Nyota huyo raia wa Ghana ameutaka uongozi wa Simba kufanya uchunguzi wa kina na kutoa ufafanuzi rasmi ili kuondoa sintofahamu iliyopo. Aidha, alisisitiza kuwa bado ana dhamira ya kuitumikia Simba na kupambana kwa ajili ya mafanikio ya timu hiyo.
Sowah pia ameomba uongozi wa klabu hiyo kuondoa kusimamishwa kwake au kuitisha kikao cha haraka cha kamati ya nidhamu ili suala lake lipatiwe ufumbuzi na aweze kurejea kuendelea na majukumu yake ya soka.
The post SAKATA LA SOWAH LAPAMBA MOTO SIMBA, AOMBA UCHUNGUZI WA KINA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/27KH58u
via IFTTT
Post a Comment