HAWAKUWEZA kuujaza pomoni Uwanja wa New Amaan Complex unaoingiza watu 15,000 lakini baada ya mchezo wa Dabi ya Kariakoo, Machi Mosi, mwaka huu, mashabiki wa Simba na Yanga wametupa stori nzuri ya kusimuliana hapa kijiweni.
Jambo ambalo limefurahisha wengi ni namna mashabiki walivyoshabikia kistaarabu dakika 90 za mechi ya Watani wa Jadi, Yanga na Simba pasipo rabsha za aina yoyote.
Tofauti na tulivyowazoea zikikutanaga timu hizo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, mashabiki hukaa majukwaa tofauti na wa Yanga hukaa sehemu yao na wa Simba kwao na ukienda kwa mwenzako unaweza kufanyiwa vurugu, juzi Zenji haikuwa hivyo.
Tumeona mashabiki wa vigogo hivyo vya soka nchini wakijichanganya na kukaa pamoja majukwaani na hakukuwa na purukushani wala vurumai ambazo zingefanya baadhi ya watu wasiondoke wakiwa salama.
Kwenye kijiwe hapa hatufahamu hilo limechangiwa na eneo lenyewe ambalo mechi imechezwa au tu mashabiki wa soka letu wameanza kubadilika hivi sasa lakini kinachotokea ni ishara nzuri sana kwa soka letu siku za usoni.
Mashabiki wameonyesha kumbe wanaweza kuitekeleza kwa vitendo dhana ya utani wa jadi uliopo baina ya timu hizo mbili badala ya kuzigeuza Simba na Yanga kama chanzo cha uhasama.
Ustaarabu huu ni utamaduni fulani mzuri ambao ukiendelezwa, soka letu litapiga hatua sana kwa vile tutatumia muda mwingi kujadili mambo mengi ya maana badala ya kufokasi na kutatua migogoro ambayo haina kichwa wala miguu.
Kilichoonyeshwa Zanzibar kinapaswa kuwa na mwendelezo hasa ukizingatia mwakani, nchi yetu itakuwa na tukio kubwa la Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) tunazoziandaa kwa pamoja na Kenya na Uganda.
Tunahitaji umoja wa mashabiki hasa wa Simba na Yanga katika kuisapoti timu yetu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na mashindano kijumla.
The post MASHABIKI WALITUPA LA KUJIVUNIA KARIAKOO DABI appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/heCaluM
via IFTTT
Post a Comment