KUELEKEA mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, waamuzi watakaosimamia Kariakoo Derby kati ya Yanga SC na Simba SC wametangazwa rasmi, huku macho na masikio ya mashabiki yakielekezwa Zanzibar ambako pambano hilo linatarajiwa kupigwa.
Ni mechi inayobeba hisia kali na ushindani wa muda mrefu kati ya miamba hiyo miwili ya soka la Tanzania.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), mchezo huo utachezwa Machi 1, 2026 katika Uwanja wa Amaan Complex kuanzia saa 2:15 usiku.
Uchaguzi wa uwanja huo umeongeza hamasa kwa mashabiki wa pande zote mbili, wakisubiri kuona nani ataibuka kidedea katika pambano hilo la heshima na alama muhimu za ubingwa.
Mwamuzi wa kati wa mchezo huo atakuwa Nassoro Mwinchui kutoka Tanga. Atasaidiwa na Kassim Mpanga wa Dar es Salaam kama mwamuzi msaidizi wa kwanza, huku Hamdani Said wa Mtwara akiwa mwamuzi msaidizi wa pili.
Mwamuzi wa akiba ni Ramadhan Kayoko kutoka Dar es Salaam, wakati tathmini ya waamuzi itasimamiwa na Israel Mjuni, pia kutoka Dar es Salaam.
Mwinchui ameendelea kuwa miongoni mwa waamuzi wanaopewa dhamana ya kusimamia michezo mikubwa ya Ligi Kuu inayozihusisha klabu kongwe nchini.
Takwimu za msimu wa 2024/25 zinaonyesha kuwa aliichezesha Simba katika michezo mitatu ya ligi, akibeba jukumu la kufanya maamuzi muhimu ndani ya dakika 90 za kila pambano.
Katika michezo hiyo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar, ikashinda 1-0 dhidi ya Mashujaa FC, kabla ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons. Rekodi hiyo inaonyesha kuwa kati ya michezo mitatu aliyosimamia, miwili Simba ilishinda na mmoja kupoteza.
Kwa upande wa Yanga, hadi kufikia kipindi hicho cha msimu, Mwinchui hakuwa amechezesha mchezo wowote wa ligi unaoihusisha timu hiyo.
Uteuzi huo wa waamuzi unakuja wakati presha ya mchezo ikiwa juu, huku kila timu ikihitaji ushindi ili kujiimarisha katika mbio za ubingwa. Kwa ukubwa wa Kariakoo Derby, macho mengi yatakuwa kwa waamuzi kuhakikisha wanadhibiti mchezo kwa weledi, umakini na uadilifu, ili haki itendeke na mshindi apatikane uwanjani.
The post NWINCHUI KATIKATI YA DERBY KARIAKOO appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/GwQxASy
via IFTTT
Post a Comment