MSIMU WA KIMATAIFA WATUTUPA, AHMED ALLY

BAADA ya Simba SC kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Esperance Sportive de Tunis, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amekiri wazi kuwa msimu huu wa mashindano ya kimataifa umekuwa mgumu na wenye maumivu kwa Wekundu wa Msimbazi.

Ahmed amesema licha ya juhudi kubwa walizozionyesha, matokeo yameonyesha kuwa msimu huu haukuwa rafiki kwa Simba katika anga la kimataifa.

Ameeleza kuwa hali hiyo inauma, lakini ni jambo ambalo wanapaswa kulikubali kwa moyo wa michezo.

Amefafanua kuwa soka lina mzunguko wake, kwani misimu mingine Simba imekuwa ikipeperusha bendera ya taifa kwa kufuzu hatua za robo fainali huku timu nyingine zikishindwa, lakini safari hii hali imekuwa tofaut, huu ni msimu ambao Simba imejikuta ikianguka mapema.

“Hatuna sababu ya kuvurugana wala kutafuta mchawi. Itoshe kusema msimu huu haukuwa wetu au haikuwa riziki yetu,” amesema Ahmed, amesisitiza umuhimu wa kukubali hali halisi na kusonga mbele kwa mshikamano.

Ahmed ameongeza kuwa bado Simba ina mechi mbili za kukamilisha katika mashindano hayo, kabla ya kuelekeza nguvu zote kwenye mashindano ya ndani ambako bado wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kuokoa heshima ya klabu msimu huu.

Katika ujumbe wake kwa mashabiki, Ahmed amewapa pole Wana Simba kwa matokeo hayo, akieleza kuwa kilichokusudiwa kufanyika hakikutimia safari hii, jambo ambalo linaweza kutokea kwa timu yoyote duniani.

Aidha, amewashukuru mashabiki wote waliojitokeza uwanjani na wale waliotoa mchango wao kwa namna mbalimbali kuisapoti timu.

“Tunatambua na kuthamini mchango wenu. Asante Mungu wewe ndiye mpangaji wa yote. Hadi wakati mwingine Wanyama, hakuna kukata tamaa, maisha ya mpira bado yanaendelea,” amesema Ahmed .

The post MSIMU WA KIMATAIFA WATUTUPA, AHMED ALLY appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/ODHI8ZX
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post