SIMBA imeanza rasmi kampeni ya kusaka pointi sita jijini Dodoma, ambako itacheza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji FC katika Uwanja wa Jamhuri.
Mchezo wa kwanza unatarajiwa kuchezwa kesho dhidi ya Tanzania Prisons, kabla ya kukipiga na Dodoma Jiji FC Februari 25, huku lengo kuu likiwa ni kuvuna alama zote sita ili kujiimarisha zaidi kwenye msimamo wa ligi.
Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, kikosi hicho kimewasili Dodoma kikiwa kamili na kikiwa na morali ya juu kwa ajili ya kuanza operesheni ya kusaka ushindi katika michezo hiyo miwili.
Amesema wataanza kwa kupambana kesho kusaka alama tatu muhimu dhidi ya Tanzania Prisons, wakilenga kurejesha heshima na kuonyesha ubora wao mbele ya wenyeji hao wanaoutumia Uwanja wa Jamhuri kama dimba lao la nyumbani.
“Tumekuja Dodoma na silaha zetu zote. Tumehamishia kambi yetu hapa kwa sababu tuna michezo miwili mfululizo. Baada ya Prisons, tutacheza pia dhidi ya Dodoma Jiji FC hapa hapa,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa mkakati wa Simba ni kuvuna pointi sita kamili katika michezo hiyo miwili, hatua itakayowapa nguvu zaidi katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
The post DODOMA KWENYE MTEGO WA SIMBA, ALAMA 6 ZATAMANIWA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/2c0sznA
via IFTTT
Post a Comment