Baada ya kuhitimisha takribani siku 10 za awamu ya pili ya pre-season Afrika Kusini, kikosi cha Yanga kimerejea nchini Alfajiri ya leo Jumanne
Yanga iliondoka nchini Julai 18 kuelekea Afrika Kusini ambapo katika sehemu ya maandalizi yake, ilishiriki michuano ya Mpumalanga International Premier's Cup na Toyota Cup
Licha ya kupoteza mchezo dhidi ya Augsburg inayoshiriki ligi kuu ya Ujerumani, Wananchi walitoa upinzani katika mchezo huo uliomalizika kwa Augsburg kushinda mabao 2-1
Yanga ikashinda 1-0 mechi ya pili dhidi ya TS Galaxy na kisha kutwaa Toyota Cup kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs
Akizungumza baada ya kurejea mapema leo, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kikosi chake kimepata maandalizi mazuri ambayo anaamini yatawasaidia kuwa na msimu bora 2024/25
"Yalikuwa ni maandalizi mazuri kwetu, tumecheza mechi zenye ushindani, matokeo sio kitu muhimu sana lakini nikwambie wachezaji wamepata maandalizi mazuri"
"Kama benchi la ufundi, tumepata muda wa kufanya kazi na wachezaji wapya na kuona ni kwa kiasi gani watakuwa na mchango katika timu yetu"
"Tuna wachezaji 27 na wote wako tayari kutumika katika mashindano mbalimbali tutakayoshiriki, muhimu itategemea na mpango wa kila mechi na aina ya mpinzani tutakayekutana nae"
"Tangu mwanzo nilisema hapa hayachezi majina ya wachezaji bali kila mchezaji atapata nafasi kwa kuzingatia kile anachotoa katika uwanja wa mazoezi," alisema Gamondi
Wachezaji wa Yanga wamepewa mapumziko ya siku moja kabla ya kukamilisha maandalizi kuelekea mchezo wa kilele cha wiki ya Mwananchi dhidi ya Red Arrows Jumapili
Post a Comment