Yanga, Azam fainali FA mechi ya kisasi, vita iko hapa

 Yanga, Azam fainali FA mechi ya kisasi, vita iko hapa

Hatimaye ile siku iliyosubiriwa ni leo Fainali ya kombe la Crdb federation Cup AZAM FC vs YANGA fainaili ya kisasi Fainali ya kibabe unaanzaje kukosa kuitazama mechi hii live bure kwenye simu yako bonyeza hapa kudownload app itakayoonesha mechi hii live kabisa buree bofya sasa kuidownload mapema ili kuepuka usumbufu muda wa mechi

Mwisho wa ubishi. Ile siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini, ndo leo. Ndio, Yanga wanaotetea taji la michuano ya Kombe la Shirikisho nchini, itavaana na Azam katika fainali ya kisasi inayopigwa leo Jumapili kuanzia saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani hapa.

Pambano hilo la fainali ya tisa tangu kurejeshwa kwa michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 1967 ikifahamika kama Kombe la FAT kisha kuwa Kombe la FA na kuzimika 2002, awali lilipangwa kupigwa Uwanja wa Tanzanite uliopo, Karatu Manyara kabla ya kuhamishiwa huku baada ya uwanja wa awali kutokidhi vigezo.

Ni bonge la fainali inayozikutanisha timu zilizomaliza nafasi mbili za juu za Ligi Kuu Bara hivi karibuni, huku zote zilikuwa zikichuana vikali na kupokezana kiti cha uongozi kabla ya watetezi Yanga kufanya yao na kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo na Azam kushika nafasi ya pili.

Pia ni pambano linalokutanisha wachezaji waliokuwa na vita ya kuwania kiatu cha Mfungaji Bora wa Ligi, Stephane Aziz KI na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kabla ya Mbukinabe kumaliza mbabe akifunga 21 dhidi ya 19 ya Fei, na leo tena kuna vita nyingine ya nyota wa timu hizo wanaowania ufungaji bora wa Shirikisho kati ya Clement Mzize mwenye mabao matano na Abdul Suleiman ‘Sopu’ mwenye mabao manne.

Kubwa zaidi ni mechi ya kisasi kwa timu zote. Ndio, katika pambano la mwisho kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara, Yanga ilicharazwa mabao 2-1, hivyo leo itataka kulipa kisasi cha kipigo ambacho kiliwayumbisha Wananchi kwa mechi za kimataifa kwani baadhi ya mastaa wao waliumia siku hiyo.

Lakini kwa Azam inataka kulipa kisasi cha kufungwa katika fainali mbili ilizokutana na Yanga kwenye Kombe la Shirikisho, ikianza kwa kunyukwa mabao 3-1 msimu wa 2015-2016 kisha kulala 1-0 msimu uliopita jijini Tanga na iwapo leo haitakomaa itakuwa inapigwa fainali ya tatu na wababe hao wa nchi.

BONGE LA FAINALI

Mashabiki wanaenda kushuhudia fainali kali iliyoteka hisia za wengi kuanzia nje hadi ndani ya uwanja, hiyo yote inatokana na wachezaji wanaokwenda kuzipambania timu zao.

Ndani ya Yanga, kuna Ibrahim Bacca, Shekhan Ibrahim na Mudathir Yahya, huku Azam wakiwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wanaotokea wa Zanzibar, hivyo fainali imepelekwa nyumbani mbele ya mashabiki wanaowajua nje ndani na kiu yao ni kuona timu wanazozichezea zinabeba taji hilo.

Kwa Bacca na Sheikhan inaweza isiwe ishu sana, ubishi upo kwa Fei Toto na Mudathir ambao wana mashabiki wao wakitamba kwamba kila upande utafanya kweli, lakini mwisho wa siku wenyewe wamekubaliana Uwanja wa New Amaan Complex, utaamua.

Ukiachana na hilo la mastaa wa Kizenji, lakini kuna bato nyingine ya mastaa wa kigeni wa timu hizo akiwamo Aziz KI, Pacome Zouzoua, Khalid Aucho na wengine dhidi ya kina Kipre Jr aliyemaliza kama kinara wa asisti wa Ligi Kuu Bara, Gjibril Sillah, James Akaminko, Daniel Amoah na wakali wengine.

Licha ya vita ya ufungaji mabao, lakini Mzize na Sopu ni wachezaji wanaowajulia makipa wa timu hizo, hivyo mashabiki wanasubiri kuona kama Sopu ataendelea kumtesa Diarra Djigui au Mzize atamfunga Mohammed Mustafa kama wataanzia kwenye milango mitatu ya timu hizo.

KIU YA TAJI

Yanga itaingia uwanjani ikiwa na shauku kubwa ya kutetea ubingwa wake, wakati Azam ikihitaji kulipa kisasi cha msimu uliopita baada ya kupoteza fainali mbele ya Yanga kwa bao 1-0. Azam imekuwa haifui dafu mbele ya Yanga kila walipokutana katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo.

Msimu wa 2015-2016 wakati michuano hiyo iliporejea kwa mara nyingine, Yanga iliifunga Azam mabao 3-1, wafungaji wakiwa ni Deus Kaseke na Amissi Tambwe aliyefunga mawili, lile la Azam mfungaji alikuwa Didier Kavumbagu.

Msimu uliopita timu hizo zilikutana tena fainali kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Yanga ikashinda 1-0 kupitia Kennedy Musonda.

Safari hii Azam imesema haitaki utani, italipa kisasi huku pia hesabu zake zikiwa ni kumaliza msimu angalau na taji moja.

Ikumbukwe, Azam ilikuwa ya kwanza kufuzu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 yaliyofungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Abdul Seleman Sopu aliyepiga mawili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.


Yanga yenyewe ikaichapa Ihefu bao 1-0 lililofungwa na Stephane Aziz Ki katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwa dakika 120 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Azam tangu msimu wa 2015-2016, tayari imecheza fainali tatu za michuano hii na kushinda moja pekee ilipoichapa Lipuli bao 1-0 msimu wa 2018-2019, wakati Yanga imecheza fainali nne na kushinda tatu, imepoteza moja msimu wa 2020-2021 dhidi ya Simba. Ilizoshinda ni 2015-2016, 2021-2022 na 2022-2023. Klabu hiyo inasaka taji la tatu mfululizo kama ilivyofanya katika Ligi Kuu Bara.

MIPANGO FRESHI

Katibu Mkuu wa ZFF, Hussein Ahmada Vuai, aliizungumzia fainali hiyo akisema:

“Huu ni mchezo mkubwa wa kihistoria, sisi kama ZFF kwa upande wetu tunasema tumepokea kwa mikono miwili ugeni huu unaokuja, ZFF tuko tayari katika hilo. Tunawaomba mashabiki waje kwa wingi na wakate tiketi mapema kwani mageti yatakuwa wazi kuanzia saa nane mchana.”€

Kocha Mkuu wa KMKM, Ame Msimu alisema: “Hii ni fursa adhimu ambayo tulikuwa tunaihitaji wadau wa michezo hapa Zanzibar. Tutajifunza vitu vingi kupitia mchezo huu.

“Pamoja na yote ni fainali kubwa kwa Watanzania, pia ni somo kubwa kwa vijana wetu. Fainali hii itatoa chachu kwa ZFF na klabu zote wapi maendeleo yapo na wapi mwelekeo wetu upo kama Zanzibar.”

WACHANGAMKIA FURSA

Wanasema katika kila unapokuwepo mkusanyiko wa watu, basi ndani yake kuna fursa. Kauli hiyo imetumiwa na wafanyabiashara wa visiwani hapa baada ya kunufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa fainali hiyo.

Huko mtaani, gharama za maisha kwa kiasi fulani imepanda na vyakula bei juu kulinganisha na awali pengine hata mikoa mingine kama vile Dar es Salaam.

Zanzibar, ukikuta matunda uliza bei kwanza usianze kula utakutana na kitu kizito kwani lile chungwa au ndizi ambayo Dar unanunua kwa Sh200, huku ni jero.

Achana na hilo, waendesha bodaboda nao wametumia fursa ya kupandisha bei kusafirisha abiria na wakati mwingine wakikuona umezubaa na hupajui unapokwenda, basi utakamulia fedha nyingi sana.

Nyumba za wageni nazo hazishikiki, siku nne kabla ya mechi, vyumba vilikuwa vimejaa kwa baadhi ya maeneo hasa karibu na Uwanja wa New Amaan Complex.

Ukitaka sehemu nzuri na tulivu karibu na uwanja, kama hauna Sh70,000 hadi 100,000 hutoboi, bora ukakae nje ya mji huko na bei zake zinasimamia Sh40,000 hadi 50,000.

JEZI SIMBA, YANGA ZATAWALA

Wauza jezi nao hawapo nyuma, licha ya kwamba mchezo unazihusisha Yanga na Azam, lakini jezi za Simba nazo zinauzwa sana tu.

Pembezoni mwa Uwanja wa New Amaan Complex, wafanyabiashara wa jezi wameweka bidhaa zao na zile za Simba na Yanga zipo kwa wingi, na chache za Azam.

SAFARI ILIVYOKUWA

Hadi kufika fainali, Yanga ilianza mechi katika hatua ya 64 kwa kuvaana na Hausing ya Njombe na kuifyatua mabao 5-1, kisha kutinga 32 ilipovaana na maafande wa Polisi Tanzania na kuikandika mabao 5-0 na kuingia 16 Bora ilipovaana na Dodoma Jiji na kuichapa mabao 2-0.

Katika hatua ya robo fainali, watetezi hao wa taji walivaana na Tabora United na kuifyatua 3-0 na kutinga nusu fainali na ilikutana na Ihefu na kuifunga bao 1-0.

Kwa upande wa Azam FC safari yake ya kufika fainali ilianza na Alliance ya Mwanza na kuifunga mabao 2-1, kisha ikaenda hatua ya 32 Bora na kukutana na Green Warriors na kuifyatua 5-0 na kutinga 16 Bora na ilivaana na Mtibwa Sugar na kuwanyoosha kwa mabao 3-0.

Katika hatua ya robo fainali Azam ilichuana na Namungo na kuing’oa kwa mabao 4-1 kisha kwenda nusu fainali na kupangwa na Wagosi wa Kaya, Coastal Union ambao waliinyoa kwa mabao 3-0, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na leo ipo Zanzibar kuvaana na Yanga katika fainali.

Nani atakayeibuka na ushindi kwenye mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 2:15 usiku? Tusubiri tuone nani atakayevaa suti ili kulipokea Kombe la Shirikisho la msimu huu timu zitakaporejea Tanzania Bara!

VIKOSI TARAJIWA

Kama hakutakuwa na mabadiliko makubwa kwa timu hizo ni wazi makocha, Miguel Gamondi wa Yanga na Youssouf Dabo wa Azam wataingia uwanjani wakiwa wamefunga busta kwa kuanzisha mastaa wa vikosi vya kwanza ili kazi iwe rahisi.

Yanga inaweza kuanza na kikosi hiki; Diarra Djigui, Yao Kouassi, Nickson Kibabage/Joyce Lomalisa, Ibrahim Bacca na Dickson Job, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Kennedy Musonda/ Mzize, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI.

Kwa Azam mziki unaweza kuwa hivi; Mohamed Mustafa, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Yeison Fuentes, Yannick Bangala, Yahya Zayd, James Akaminko, Abdul Suleiman ‘Sopu’, Kipre Junior, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Gjibril Sillah.

DIARRA APEWA KIFAA KUZUIA MABAO

Yanga inafanya mambo kama wapo Ulaya vile. Juzi jioni iliwaacha watu wengi midomo wazi baada ya kutambulisha kifaa kipya cha mazoezi kwa makipa wao wakiongozwa na kipa namba moja, Diarra. Hapo awali walitambulisha vifaa tofauti mazoezini ikiwemo ball launcher kinachotumika kama mbadala wa wachezaji kuwapigia makipa mashuti langoni.

Kikosi hicho kinajiandaa na mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Azam yenye Sopu anayemtesa sana Diarra wanapokutana sambamba na Fei Toto aliyemtungua mechi ya mwisho Ligi Kuu Bara.

Yanga katika kujiandaa na mchezo huo chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kwenye Uwanja wa Amaan Kwa Wazee, alikitambulisha kifaa hicho katika siku ya pili ya mazoezi.

Kifaa hicho cha kisasa ni kama miwani ambacho kitaalamu kinaitwa Strobe Eyewear au Strobe Glasses na Kocha wa Makipa wa Yanga, Alaa El Meskini, alikuwa akiwanoa Diarra, Aboutwalib Mshery na Kassim, huku wakiwa wamevaa kifaa hicho machoni, huku wakipigiwa mipira na kudaka kwa ufasaha.

Kifaa hiki kimetengenezwa maalum kwa ajili ya kumfanya mtumiaji kufanya uamuzi wa haraka na sahihi kwani macho yanapoona basi taarifa hufika kwa haraka zaidi kwenye ubongo.

Unapovaa kifaa hicho, uchakataji wako wa taarifa unakuwa wa haraka zaidi jambo linalofanya utendaji wako wa kazi kuwa wa kasi na fasaha.

Kipa akivaa kifaa hicho humfanya kudaka michomo mingi kwa usahihi na nadra sana kuruhusu kufungwa kwani macho yake yanapouona mpira, taarifa inafika kwa haraka kwenye ubongo na kurudisha majibu kwa kasi inayomfanya kuwa tayari kufanya uamuzi sahihi.

Thamani ya kifaa hicho inakadiriwa ni Dola 299 (Sh774,506).

FAIDA ZA KIFAA HIKI

Kuongeza umakini, hii inayafanya macho yako kuwa kwenye tukio jambo linalokufanya uende sawasawa na hali ya mchezo.

Ukitumia kifaa hiki, pia huyawezesha macho yako kuona vizuri zaidi ya ilivyo kawaida, pia hukufanya kuwa mwepesi katika kufanya maamuzi sahihi.

Pia kuufanya mwili wako kuwa kwenye sehemu sahihi ya kufanya uamuzi kwani kinakupa uwezo wa kuona pembeni na mbele yako kuna hatari gani.

MAANA KWA YANGA

Yanga inafahamu Jumapili ina kibarua kigumu mbele ya Azam katika mchezo wa fainali, hivyo inajiandaa kwa namna yoyote ile isipoteze mchezo huo.

Inafahamika wazi, fainali kama ikitokea matokeo yakawa sare, basi mikwaju ya penalti itaamua mshindi na Yanga imekuwa haipo vizuri sana ikifika hatua hiyo, kwani inakumbuka katika Ngao ya Jamii msimu huu dhidi ya Simba, ilipoteza.

Lakini, Yanga inakumbuka msimu huu ilipokutana na Azam mara mbili ligi kuu, iliruhusu mabao manne na yenyewe ikifunga manne, lakini mabao iliyoruhusu yalionekana kama kipa wao alishindwa kufanya uamuzi wa haraka kutokana na mashambulizi iliyofanyiwa.

Hivyo uamuzi wa kutumia kifaa hiki unaendana na jambo hilo, kwanza ifahamike mabao ya penalti na faulo yanaitesa sana Yanga hasa inapocheza na timu kubwa kwani macho huwa na kawaida ya kuona jambo lakini mwili unashindwa kuchukua uamuzi wa haraka kutenda, kulingana na kasi ya mpira matokeo yake kipa anashtuka nyavu zinatikisika.

Ukiangalia mechi ambayo Azam ilishinda 2-1 dhidi ya Yanga, bao la kwanza lililofungwa na Gibril Sillah, Diarra alishindwa kuokoa hatari na kuwafanya walinzi wake kujigonga kabla ya kumfikia mfungaji. Bao la pili, ilipigwa krosi ambayo Diarra akiwa amebana kwenye nguzo, Feisal Salum akafunga palepale.

Kutokana na hilo, utumiaji wa kifaa hiki huongeza ufanisi wa macho katika utendaji wake wa kazi, hivyo humsaidia kipa kuokoa hizo hatari hasa zile za kushtukiza. Kumbuka kifaa hiki hakitumiki kwenye mechi, kinaishia mazoezini tu, lakini matumizi yake yana faida kwani ukitumia kisha ukakiacha na kwenda kudaka kawaida, bado uwezo wako wa kuona na kufanya uamuzi wa haraka huwa mkubwa.

ULINZI MAZOEZINI NOMA

Katika kuhakikisha kila mmoja anafanya mambo kwa ufanisi ili kubeba ubingwa kwa tahadhari kubwa ya mpinzani wake asiibe mbinu, timu hizo zimechukua uamuzi wa kufanya mazoezi zikiwa chini ya ulinzi mkali.

Timu hizo zimekuwa zikifanya mazoezi kwenye viwanja vya Amaan Kwa Wazee vilivyopo pembezoni mwa Uwanja wa New Amaan Complex.

Tangu siku ya kwanza ya mazoezi, Mwanaspoti lilifika viwanjani hapo na kujionea kumekuwa na ulinzi mkali kiasi cha watu wasiohusika kuzuiwa.

Mwanaspoti limeshuhudia namna askari waliowekwa getini wakiwa wakali kuzuia watu wasiingie wala kuchungulia pindi timu hizo zinapofanya mazoezi.

Siku ya pili ya mazoezi kwa timu hizo yaliyofanyika juzi Ijumaa, Azam ilikuwa ya kwanza kufika uwanjani hapo saa 10 jioni.

Wakati Azam ikiwa na mazoezi hapo, uwanja mwingine kulikuwa na mechi ya Ligi Kuu Zanzibar ya Mlandege dhidi ya Chipukizi United.

Mashabiki waliokuwa wakiingia uwanjani hapo kwa ajili ya kuangalia mechi hiyo ya Ligi Kuu, walikuwa wakifukuzwa pindi wakionekana wakisogelea sehemu inayofanyia mazoezi Azam kwa kile kilicholezwa hakuna mtu asiyehusika anayeruhusiwa kuangalia kinachoendelea.

“Hapa haturuhusu watu kuangalia mazoezi, tumepata maagizo kutoka kwa Azam, hawataki watu waangalie wanachokifanya, ondokeni,” alisikika mmoja wa askari wanaolinda usalama uwanjani hapo akiwafukuza watazamaji waliokuwa bize kufuatilia mazoezi hayo.

Azam ikiwa inaendelea na mazoezi huku pia mechi ya ligi ikikaribia kumalizika, kikosi cha Yanga kikawasili uwanjani hapo saa 12 jioni.

Hata hivyo, Yanga ilibidi isubiri hadi mechi ya ligi imalizike ndipo iutumie uwanja huo kwa sababu ule mwingine Azam ilikuwa bado haijamaliza programu zao.

Baada ya mechi hiyo ya ligi kumalizika, askari walichukua jukumu la kuwatawanya haraka mashabiki, wachezaji na viongozi wa timu za Mlandege na Chipukizi na zoezi hilo lilichukua muda mchache lakini mvutano mkubwa ulitokea kwa baadhi ya watu kugoma kutoka uwanjani hapo, lakini baadaye walikubali kuondoka.

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post