Kuelekea mchezo wao robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns, jana Klabu ya Yanga ilizindua hamasa zake katika Makao Makuu ya Klabu hiyo, Jangwani, jijini Dar es Salaam ambapo mitaa ya Kariakoo yote ilitikisika.
Mchezo huo ambao ni maalum kwa kiungo wao, Mudathir Yahya ukiwa na kauli mbiu isemayo ‘SIMU ZIITE, TUKUTANE KWA MKAPA’, utachezwa Machi 30, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Baada ya jana, hamasa itaendelea tena leo Jumatano ambapo itakuwa zamu ya maeneo ya Makumbusho kuanzia saa 6 mchana.
Kesho Alhamisi ikiwa ni siku ya mwisho kufanya hamasa mitaani, itakuwa zamu ya meneo ya Tandika.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Young Africans SC, Ally Kamwe, amesema: “Afrika inajua mechi kubwa ni moja ambayo ni Young Africans SC na Mamelodi. Kila Mwafrika anaizungumzia mechi hii. Hii ndiyo mechi ambayo imetikisa zaidi Afrika kwa sasa.
“Huu ni muda wetu na hii ni mechi ya Muda. Hii ndio timu kubwa nchi hii. Tutavuka kwenda nusu fainali kwa soka safi.
“Hao mnaowaita Wabrazil watambe wanakotambaga, lakini katika ardhi hii hakuna wa kututambia, tunatamba wenyewe, anayebisha aseme yeye ametamba mbele yetu? Suala la kupandisha mnara hatutanii, tunapandisha kwa yeyote.”
PATA GB 30 KILA MTANDAO BURE HAPA
No comments:
Post a Comment