Baada ya kumalizika kwa mchezo uliowapeleka Yanga SC robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kiungo wa timu hiyo, Pacome Zouzoua amezungumza kwa hisia kubwa baada ya mchezo huo.
Mchezo huo uliopewa jina la Pacome Day kama sehemu ya hamasa kwa Wananchi, ulichezwa jana Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na timu ya Young Africans SC ikaichapa CR Belouizdad magoli 4-0.
Katika mchezo huo wa Kundi D, Pacome ambaye ni raia wa Ivory Coast alionesha kiwango kikubwa sana ikiwemo kutoa pasi ya mwisho kwa goli la tatu lililofungwa na mshambuliaji raia wa Zambia, Kennedy Musonda.
“Kiukweli nina furaha sana, sikutarajia katika maisha yangu kama tukio kama hili la PACOME DAY lingetokea na kufana namna hii.
“Mke wangu kutoka Ivory Coast alikuja hapa nchini kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Belouizdad, niliongea naye kabla ya mechi, lakini baada ya mechi kumalizika alibubujikwa na machozi mengi ya furaha, kiufupi alilia sana.
“Hali hii ilinipa imani kubwa kuwa kuna kundi kubwa la Wananchi nyuma yangu ambalo liko tayari kwa lolote ili tuwape furaha. Narudia tena, nina furaha isiyo kifani.
“Nawashukuru sana Wanachi kwa mapenzi makubwa waliyoyaonesha, tuendelee kumuomba Mungu na nina imani tutafanya vizuri kwenye hatua ya robo fainali mpaka hatua zinazofuata,” alisema Pacome
No comments:
Post a Comment