Uongozi wa Wekundu wa Msimbazi umefunguka kuhusu tetesi za mshambuliaji wao, Kibu Denis, kutakiwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinasema Mamelodi Sundowns imewasilisha rasmi ofa kwa Simba ya kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa yuko katika kikosi cha Timu ya Taifa kilichoko kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini, Ivory Coast.
Chanzo chetu kinasema hii ni mara ya pili kwa Mamelodi Sundowns kutuma ofa kuhusiana na Kibu lakini uongozi wa Simba ukikaa kimya kuhusiana na maombi hayo.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema katika meza ya klabu hiyo hakuna ofa kuhusu Kibu au mchezaji mwingine anayetakiwa na wao kwa sasa wanafikiria kuimarisha kikosi chao.
Ahmed alisema Simba inahitaji kukijenga imara kikosi chao ili kuongeza ushindani na kufanya vizuri katika michezo iliyopo mbele yao.
Alisema mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi juu ya taarifa hizo kwa sababu hakuna taarifa rasmi waliyopokea ya kutakiwa kwa Kibu au Willy Onana ambaye naye anahusishwa kuwindwa na JS Kabylie ya Algeria.
"Hawa wachezaji wako katika mipango ya kocha wetu (Abdelhak Benchikha), kwa sasa tunahitaji kuboresha kikosi cha timu kama ulivyoona tumeshatambulisha wachezaji watatu akiwamo, Salehe Karabaka, Babacar Sarr na Ladack Chasambi, na hivi karibuni tutamtambulisha nyota mwingine.
Tunahitaji kuongeza mtu, hiki kipindi sio cha kuondoa wachezaji muhimu kwa kuuza kwa sababu ni muda wa kuboresha kama ilivyo kwetu tunaboresha kulingana na nafasi zilizopendekezwa,” alisema Ahmed.
Aliongeza uongozi umeamua kumwachia majukumu yake Benchikha kwa kutoingilia mambo yake hasa katika kuhakikisha Simba inakuwa imara na wachezaji kujutuma kwa kupambana.
No comments:
Post a Comment