Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
MBUNGE wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku 'Msukuma' ambaye pia ni mwanachama wa Yanga amerusha kijembe kwa watani wao Simba kwamba usajili waliofanya ni mbovu huku akiwabeza kuweka kambi Uturuki ni ulimbukeni wa kufuja fedha kwa wachezaji ambao hawawezi kuleta mafanikio.
Msukuma ametoa kauli hiyo leo Julai 15,2023 wakati akizindua 'Wiki ya Mwananchi' kitaifa katika Uwanja wa Furahisha, Mwanza na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutenga mapema bajeti kubwa ya hamasa kwani msimu ujao Yanga imejiandaa kufanya vyema na kuzoa makombe yote itakayoshiriki.
Akizungumza na umati mkubwa wa mashabiki na wanachama wa Yanga, Msukuma amesema Yanga imeshusha majembe ya moto tofauti na watani wao walioleta watu wasio na viwango vya uhakika.
"Timu yetu ni nzuri na mfadhili wetu bado yuko vizuri wataumia sana, tuna mfadhili wa kweli mtu mwenye hela aongei ana swaga, siyo mtu unasajili wachezaji majeruhi unapeleka Uturuki, tunawapongeza sana viongozi wa Yanga kwa kuendelea kuwa wazalendo, hatuwezi kuwa malimbukeni nchi yetu imeshafunguka tunataka na Wazungu waje pre season Tanzania wacheze pale Avic town,"
"Tuendelee kuwaombea viongozi na timu yetu, najua kuna mishale mingi lakini mmesimama kidete Yanga tutaendelea kuchukua makombe, tunahitaji mwakani tuwe na makombe matano, hata yale tuliyoyakosa tuyapate," amesema Msukuma
Akizungumzia Wiki ya Mwananchi, amesema yeye ni Mwana Yanga kindakindaki na kuuomba uongozi wa klabu hiyo msimu ujao uzinduzi wa tamasha hilo ukafanyike mkoani Geita, huku akiomba wachezaji kufanya vyema kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Kaizer Chief Julai 22, mwaka huu.
"Tuna mechi kubwa siku ya Wananchi, twendeni tukaiheshimishe timu yetu. Tunajua kuna kufungwa na kudroo sisi ni Yanga moyoni tutakuwa na Yanga katika shida na raha," amesema
Chanzo: Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment