Kimenuka huko Geita gold Minziro apewa mkono wa kwaheri - EDUSPORTSTZ

Latest

Kimenuka huko Geita gold Minziro apewa mkono wa kwaheri


 Kimenuka huko Geita Gold wakati ligi ikiwa inaelekea ukingoni mambo yamekuwa sivyo kwa wachimba madini hao ambao makocha wa timu hiyo kumekuwa na tofauti juu ya mikataba yao dhidi ya uongozi.


Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fredy Felix 'Minziro' mkataba wake unamalizika Mei 28 yaani siku ambayo ligi ilikuwa ikifika tamati kabla ya Bodi ya Ligi (TPLB) kufanya mabadiliko.


Mathias Wandiba ambaye ni msaidizi wake naye mkataba wake unafikia tamati mwezi ujao huku akitajwa kurejea Mbeya City timu ambayo alikuwa akifundisha kabla ya kuondoka. Inaelezwa hakuna maongezi yoyote yaliyofanywa na uongozi japo juzi walikuwa wakae lakini kutokana na kuwepo kwa kikao cha halmashari basi hakikufanyika.


Timu hiyo imesalia michezo miwili yote ugenini dhidi ya Ihefu kisha itafunga pazia la ligi dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo inaelezwa hata katika safari ya kuelekea Mbarali makocha hao hawakuwepo kwenye safari huku ikielezwa kuna mambo mengine nyuma ya pazia.


"Makocha hawakuwepo safarini na badala yake wakamweka kocha wa vijana wa U20, Choki Abeid na hata mazoezi ya jana makocha hao hawakutokea," kilieleza chanzo hicho. Minziro alianza kuifundisha Geita ikiwa Ligi ya Championship lakini baada ya kuipandisha mabosi wakampa timu, Etienne Ndayiragije ambaye hakudumu sana.


Oktoba 23, 2021, uongozi ulivunja mkataba na Ndayiragije kufuatia kushindwa kufikia malengo waliyokubaliana baada ya kuiongoza timu kwenye michezo minne na kuondoka kwake kulimpa nafasi nyingine, Minziro.


Minziro amezipandisha Ligi Kuu timu tatu KMC, Singida United na Geita Gold ambayo ikiwa nyumbani Uwanja wa Nyankumbu timu hiyo haikuwahi kupoteza mchezo wowote wa ligi tangu ikiwa Ligi ya Championship, lakini sasa tayari imepoteza dhidi ya Prisons na Mbeya City.


"Kilichosababisha timu kupoteza ni uongozi kushindwa kutimiza ahadi zake kwa wachezaji sababu msimu uliopita baada ya kumaliza nafasi ya nne tulipewa ahadi ya fedha ambayo hadi sasa haijatimizwa."


Minziro alipoulizwa juu ya hayo alisema utafutwe uongozi wa timu ndio utakuwa na majibu yote kuhusu timu na hatma yake kama yupo kwenye timu au hayupo.


Tafuteni viongozi wanajua kila kitu kuhusu mimi, kama nipo au sipo, wakishakujibu unaweza kurudi kwangu," alisema. Mwenyekiti wa Geita, Leonard Bugomola alipoulizwa alikiri makocha hao kutokuwepo kwenye safari za mwisho ili kufanya nao mazungumzo juu ya kuongeza mkataba.


"Makocha wote ni mali yetu hivyo tuliona tukiwaruhusu makocha hawa kuondoka na kikosi ambapo michezo ya mwisho inakuwa ugenini haitakuwa rahisi kuwapata tena ndio maana hawakuondoka.


"Kuhusu posho za msimu uliopita sisi tunazingatia zaidi makubaliano ya mkataba na sio hayo mengine na msimu huu lengo letu ni kuhakikisha tunamaliza kwenye 10 bora," alisema Bugomola.


Msimu huu ni makocha wawili pekee kwenye ligi ambao hawakutimuliwa, Minziro pamoja na Nasreddine Nabi kocha wa Yanga lakini timu nyingine zote zilifanya mabadiliko ya benchi lake la ufundi na hii inamaana kuwa sasa aliyebaki ni Nabi tu.


Chanzo: Mwanaspoti



Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz