Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Kalala Mayele jana Jumamosi, Aprili 29, 2023 alikabidhiwa jezi maalum namba 50 inayomanisha idadi ya mabao hamsini (50) aliyofunga hadi sasa akiwa na klabu hiyo tangu ajiunge nayo mwanzoni mwa msimu wa 2021/22.
Mayele ambaye alijiunga na Yanga akitokea AS Vita Club ya nyumbani kwao nchini Congo, ameitumikia Yanga kwa misimu miwili sasa, amefunga mabao 50 katika mechi mbalimbali za kimashindano zikiwemo za Ligi Kuu Tanzania, Kombe la Shirikisho la Azam, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Mayele amepewa zawadi hiyo na kupongezwa na wachezaji wenzake na benchi zima la ufundi la Yanga wakati wa mazoezi kambini kwao, Avic Town Kigamboni, Dar wakati wakijiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Rivers United.
Akizungumza baada ya kupokea jezi hiyo, Mayele amesema; "Nina furaha sana kupokea zawadi hii ikiwa ni miaka miwili tu tangu nimejiunga na Yanga. Hii inaonyesha namna ambavyo klabu ina thamini mchango wa wachezaji wake.
"Ninawashukuru viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wenzangu wote kwa kunisapoti, kazi hii sikuifanya peke yangu, sote tulishirikiana kwa pamoja, kuna kitu kikubwa benchi la ufundi na wachezaji wenzangu wamekiongeza kwenye carrier yangu ya soka na kunifanya niwe bora zaidi.
"Mashabiki wa Yanga ninawashukuru sana kwa sapoti yenu, mlinipokea na kunionyesha upendo mkubwa na bado mnaendelea kutusapoti, nawaomba msichoke, muendelee kuisapoti timu yetu na kesho (leo) mjitokeze kwa wingi pale kwa Mkapa ili tutimize malengo yetu ya kwenda nusu baada ya kumfunga Rivers United, asanteni sana," amesema Mayele.
Mpaka sasa Mayele ndiye kinara wa upachikaji mabao msimu huu katika Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 16 huku pia akiongoza katika kombe la shirikisho Afrika kwa mabao 5 mpaka sasa. Msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa pili akimaliza na mabao 16 nyuma ya George Mpole aliyekuwa Geita Gold na mabao 17.
Aidha, Yanga leo itatua dimbani kupepetana na Rivers United ya Nigeria ambayo mchezo wa kwanza ilifubgwa na Yanga bao 2-0 nchini kwao.
Post a Comment