BAADA ya mvutano wa miezi zaidi ya miwili kuhusu masuala ya kimkataba kati ya mchezaji Feisal Salum, 'Fei Toto' na klabu ya Yanga, Jumatatu ya wiki ijayo huenda ikawa mwisho wa sakata lote ambapo kiungo huyo anatarajia kukutana na Rais wa Yanga, Hersi Said na Mfadhili wa timu hiyo, Gharib Said Mohamed 'GSM' kuweka mambo sawa.
Hiyo ni baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kuthibitisha kwa mara ya pili kuwa Feisal ni mchezaji halali wa Yanga na anatakiwa kurudi kambini baada ya kukata rufaa akikataa maamuzi ya namna hiyo yaliyotolewa awali Januari 6 mwaka huu ambapo Yanga ilimshitaki kiungo huyo kwa kosa la kuondoka kikosini hapo bila makubaliano ya pande zote mbili huku akilipa sh 112 milioni kama pesa ya kununua mkataba wake na mshahara wa miezi mitatu, kitita ambacho Yanga ilikikataa na kumrudishia.
Baada ya kamati kumtaka Feisal arudi Yanga, nyota huyo ameendelea kuweka msimamo wake wa kutotaka kucheza kwenye timu hiyo huku mara ya mwisho akipiga hodi TFF kutaka kuvunja mkataba wake, sasa anaenda kukutana na Rais Hersi, na GSM ili kumalizana kikubwa.
Mwanaspoti limepenyezewa kuwa kikao hicho kitakachofanywa kwa siri kubwa kitakuwa na ajenda mbili hadi tatu, ambapo ya kwanza ni GSM kutaka kummwagia mkwanja mrefu mchezaji huyo na kuboresha mkataba wake maradufu zaidi ya ule wa kwanza ili abaki Yanga, lakini ya pili ni kuzungumza namna ya Feisal aanavyoweza kuvunja mkataba na kuambiwa kiasi gani cha fedha anapaswa kuwalipa Wanajangwani hao ili kuondoka kwa amani.
Katika kikao hicho, Feisal atakutana kwanza mwenyewe na viongozi hao wawili, kisha jopo la wanasheria wake nao watakutana na upande wa Yanga kwa wakati wao ili kulimaliza.
Hata hivyo, chanzo chetu (jina tunalo) kimepenyeza kuwa kivyovyote vile Feisal hana hamu ya kurudi Yanga na hataki kujumuika na kikosi cha kocha Nassredine Nabi kutokana na vitendo mbalimbali vilivyoijitokeza tangu sakata hilo limeanza, huku Yanga ikiamini itamtumia Tajiri GSM atakayemwaga pesa ndefu kumshawishi mchezaji huyo abaki mitaa ya Jangwani.
"Inaonekana tajiri (GSM), bado anamuhitaji Fei, ndio maana ametaka wakutane kuongea na yupo tayari kumlipa pesa anayotaka ili asiondoke ila hapo hapo Fei mwenyewe hataki tena kwenda Yanga na atatumia kikao hicho kutoa dukuduku hilo na kuomba msamaha ili wamuachie kiurahisi.
"Tunatarajia kikao hicho kitakuwa cha mwisho na kutamatisha kabisa 'ishu' hii, na imani yetu kitamalizika kwa kupata suluhisho la kila litu," kilieleza na chanzo hicho na kuongeza;
"Upande wa Mchezaji upo tayari kulipia mkataba uliobaki, pamoja na faini ya kutokuwepo kambini kwa kipindi chote hicho ambacho hakua kambini."
Kama Fei ataruhusiwa kuvunja mkataba huenda akalipa pesa zaidi ya ile sh, 112 milioni aliyoingiza mwanzo kwenye akaunti lakini pia kama atakubali kubaki basi atalipwa mara tatu hadi nne ya mshahara wa sh. 4.7 milioni anaolipwa kwa sasa.
No comments:
Post a Comment