Polisi Lawamani Tisho la Bunduki - EDUSPORTSTZ

Latest

Polisi Lawamani Tisho la Bunduki



Dodoma. Tukio la kutishiwa bastola kwa Kisumo Msangi hadharani kisha kumalizwa kituoni kimyakimya, limeacha lawama kwa Jeshi la Polisi mkoani hapa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa, Martin Otieno aliahidi kufafanua kuhusu tukio hilo lililotokea Desemba 30 mwaka jana na kuripotiwa kituo cha polisi kwa DOM/RB/14863/2021, lakini hakufanya hivyo.

Wakati linatokea, aliyekuwa kamanda wa Polisi Dodoma, Onesmo Lyanga aliagiza mhusika akamatwe, lakini aliachiwa siku iliyofuata.

Chanzo cha ugomvi huo ni Msangi kununua nyumba iliyokuwa inamilikiwa na Iman Ilomo kwa mnada wa mahakama kutokana na deni la benki alilokuwa akidaiwa, lakini mhusika hakukubaliana na bei iliyouzwa.


Siku ya tukio, inaelezwa Msangi akiongozana na ndugu zake pamoja na balozi wa mtaa, Tisa Msoso ghafla alitokea Ilomo na kumnyooshea bunduki huku akimwamuru asali sala yake ya mwisho.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Abinery Alex alisema hofu ilitanda kiasi cha akinamama kupiga mayowe kwa hofu ya kutokea mauaji.

“Tulipiga simu polisi ambao walifika dakika chache na kumkamata mhusika akiwa na bunduki mkononi. Walisema risasi iligoma kutoka, vinginevyo angemuua mbele yetu, jambo la ajabu eti kesi imeisha kinamnanamna tu, polisi Mungu anawaona jamani,” alisema.


Kwa upande wake, Msangi alikiri kutokea kwa tukio hilo akisema nyumba aliinunua kisheria ila anashangaa ukimya wa polisi uliodumu kwa miezi mitano sasa.

“Tulikuwa na ugomvi mkubwa kwenye nyumba hata nimeamua kuilipia mara mbili, maana pesa zinatafutwa lakini roho haitafutwi, kwa hiyo huko tumemalizana mimi nimekula hasara kwa mara ya pili, hili la bunduki…linanikumbusha maumivu, namuachia Mungu,” alisema Kisumo.

Naye Msoso alisema haelewi kilichofanyika hata polisi wakaamua kulimaliza tukio hilo kubwa kimyakimya.

“Binafsi ni tukio kubwa la kwanza kulishuhudia, nashangaa hata siku moja polisi hawajawahi kuniita nitoe ushahidi, kwa hiyo inaonyesha lilimalizwa kwa mazingira wanayojua wao,” alisema Msoso, balozi wa mtaa lilikotokea tukio hilo.

Mwananchi





Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz