MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi Ataka Ukwepaji Kodi uwe Kigezo Kuengua Wagombea - EDUSPORTSTZ

Latest

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi Ataka Ukwepaji Kodi uwe Kigezo Kuengua Wagombea



MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi, ameipongeza Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kuwafuata wafanyabiashara kwenye maeneo yao ya kazi ili kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi, akisisitiza kutawajengea ari ya kulipa kodi kwa hiari.

Vilevile, ameshauri ukwepaji wa kulipa kodi uwe miongoni mwa vigezo vya kuwaengua wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi nchini.

Hapi alitoa kauli hiyo juzi wakati timu ya maofisa wa TRA ilipomtembelea ofisini kwake Musoma mjini kumpatia taarifa ya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango ambayo ilimalizika juzi mkoani humo.

Alisema kuna baadhi ya nchi wamefikia hatua anayegombea nafasi ya uongozi, historia yake ya ulipaji kodi inafuatiliwa na ikibainika aliwahi kukwepa kulipa kodi, anapoteza sifa ya kugombea, ikiwamo uchaguzi mkuu.

“Naamini kama nchi siku moja tufike mahali ambapo ili ugombee uongozi, historia nzuri ya ulipaji kodi iwe moja ya sifa, iwe fahari kuwa mimi ni mmoja wa walipakodi na ni sehemu ya maendeleo ya taifa,” alisema Hapi.


Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, aliushukuru uongozi wa Mkoa wa Mara, viongozi wa wafanyabiashara pamoja na wafanyabiashara wote kwa ushirikiano walioutoa kwa timu ya maofisa wa TRA waliofanya kampeni hiyo mkoani humo na kufanikisha kuwafikia jumla ya wafanyabiashara 4,014.

“Katika zoezi hili, tumefikia jumla ya wafanyabiashara 4,014 ambapo Wilaya ya Tarime tumefikia wafanyabiashara 2,088, Bunda 1,126 na Musoma Mjini tumefikia wafanyabiashara 800,” alibainisha Kayombo.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Kilimo na Viwanda (TCCIA) Mkoa wa Mara, Boniphace Ndengo, aliishukuru TRA kwa kutoa elimu mkoani humo ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha mabadiliko ya sheria za kodi kila zinapopitishwa na Bunge.


“Niishukuru Idara ya Elimu kwa Mlipakodi, kazi mnayoifanya ya kutuelimisha ni kubwa sana. Moja ya eneo ambalo wafanyabiashara tumekuwa tukilalamika ni kwamba sheria inapotungwa inaanza kutekelezwa mara moja lakini kwa sasa tunashukuru mnavyokuja kutupatia taarifa mapema ili na sisi tujipange vizuri,” alisema Ndengo.

Wafanyabiashara wa Wilaya ya Musoma mkoani humo kwa nyakati tofauti walisifia kitendo cha TRA kupita mlango kwa mlango kuwapatia elimu na kusema kwamba wameepushwa na makosa yanayotokana na kutokuwa na uelewa wa masuala ya kodi.

Nyangaro Mseti ni mfanyabiashara wa Musoma Mjini ambaye alisema utaratibu huo unawasaidia kupata muda wa kutosha kuuliza maswali na kupatiwa ufafanuzi kuhusu kero mbalimbali za kikodi zinazowakabili.

Mfanyabiashara mwingine Eunice Julius alisema awali walikuwa wakiitwa eneo moja kwa ajili ya kuelimishwa juu ya masuala mbalimbali ya kodi, lakini baadhi yao walikuwa hawaendi kwa sababu walishindwa kufunga biashara wakihofia kukosa mauzo.


“Sasa mnatufuata na kutufundisha, akija mteja mnasubiri mpaka nimalize kumhudumia kisha mnaendelea, kwa kweli utaratibu huu ni mzuri sana maana elimu tunapata na mauzo hayapungui ndiyo maana naomba mwendelee tena, mje mara kwa mara,” alisema Julius.

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango mkoani Mara ilianza Februari 7, mwaka huu na ilimalizika jana ambapo timu ya maofisa wa TRA waliofanya kampeni hiyo wamefanikiwa kuwaelimisha wafanyabiashara wa Wilaya za Tarime, Bunda na Musoma Mjini.




Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz