Sababu Uhaba wa Kinywaji Cha SODA zatajwa - EDUSPORTSTZ

Latest

Sababu Uhaba wa Kinywaji Cha SODA zatajwaDar es Salaam. Wazalishaji wa soda nchini wameeleza sababu za kuadimika kwa bidhaa hiyo kunatokana na upatikanaji kwa shida sukari ya viwandani, changamoto za usafirishaji kidunia na kuongezeka kwa mahitaji mwaka uliopita.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja upatikanaji wa soda katika miji mikubwa umekuwa si wa uhakika, huku baada ya kumalizika sikukuu za mwisho wa mwaka zikiadimika zaidi na baadhi ya wafanyabiashara kuanza kupandisha bei.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa mawasiliano kwa umma wa kampuni ya Cocacola Kwanza, Salum Nassor alisema hali ya usambazaji na upatikanaji unazidi kuimarika hivi sasa na ndani ya wiki moja hadi mbili kuanzia jana huenda tatizo lililopo likaisha kabisa.

Nassor alisema tatizo kubwa ni upatikanaji wa sukari ya viwandani ambao unatokana na changamoto ya makontena duniani, pia muda mrefu unaotumika hivi sasa kuchukua mzigo bandarini tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.


“Siku za nyuma tulikuwa tunatumia siku saba hadi kumi kutoa mzigo wa sukari, lakini kwa Oktoba hadi Desemba tulikuwa tunatumia hadi siku 21 kutoa mzigo bandarini, inafikia hatua mpaka tunapunguza kuzalisha soda zinazohitaji sukari nyingi ili kutafuta uwiano wa sukari iliyopo,” alisema Nassor.

Alisema uzalishaji wa soda ukisimama siku moja unaathiri mauzo ya siku mbili hadi tatu na hilo pengo huchukua muda mrefu kuliziba, lakini sasa kwa kuwa mambo yanaanza kukaa vizuri uzalishaji unafanyika bila kusimama hata siku moja.

Mfanyabiashara wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Frank Dafa aliliambia gazeti hili kuwa wadau wa CTI ambao ni wazalishaji wa vinywaji baridi wanalalamikia kuchelewa kwa sukari bandarini.


Mkuu wa kitengo cha mahusiano ya umma wa kampuni ya SBC Tanzania Limited (wazalishaji wa soda za Pepsi), Foti Gwebe-Nyirenda alisema kwa upande wao hakuna tatizo la sukari ya viwandani, isipokuwa mahitaji yameongezeka.

Akilifafanua hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Eric Hamis alikiri kuongezeka kwa mizigo ya kawaida na makontena, lakini si kwa kiwango hicho cha kusababisha uchelewaji wa mizigo.

Alisema kuna ongezeko kidogo la meli siyo tu kwenye bandari ya Dar es Salaam, bali kimataifa.

“Mfano nikiangalia kwenye programu ya kujua mwenendo wa meli zipo za makontena 60 hivi sasa (jana) zinaelekea bandari ya Durban, Afrika Kusini na 20 zinazokuja Tanzania,” alisema.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz