Askofu Sangu Akutana Na Waganga Wa Kienyeji Gamboshi - EDUSPORTSTZ

Latest

Askofu Sangu Akutana Na Waganga Wa Kienyeji Gamboshi





ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu amekutana na Waganga wa tiba asili na tiba mbadala katika kijiji cha Gamboshi wilayani Bariadi Mkoani Simiyu kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo kuhamasisha maendeleo, imani, pamoja na kuenzi mila na desturi za kabila la Wasukuma.


Askofu Sangu ameyasema hayo leo Oktoba 19,2021 katika eneo la Kigango cha Gamboshi ambapo amewataka waganga kulinda mila na desturi za kabila la wasukuma, kupiga vita ndoa za jinsia moja, utoaji mimba pamoja na mauaji ya watu wenye ulemavu.



Katika hotuba yake Askofu Sangu amewataka waganga hao kuwa sehemu ya kulinda tamaduni za kabila la wasukuma ili jamii iepukane na masuala ya utoaji mimba na ndoa za jinsia moja ambazo zinadhalilisha utu wa mtu na kwamba waganga hao wanatibu watu kwa asilimia kubwa sana.



"Mila na desturi mtazilinda ninyi, kuna mengi yanafanyika katika jamii yetu…kupitia nafasi ,mlizonazo katika jamii, tukapandikize uhai katika maisha ya binadamu, tulinde uhai wa binadamu tangu mimba inapotungwa hadi mtoto anapozaliwa", amesema Askofu Sangu.



Amesema huko nyuma (zamani) watu wenye ulemavu wa ngozi walikuwa wakiuwawa bila hatia na kwamba lawama zote walitupiliwa waganga wa kienyeji jambo ambalo lilikuwa linaleta ukakasi katika jamii na kuonekana waganga hao hawana tija katika jamii.



Amesema tatizo la mauaji ya watu wenye ualbino lilikuwa kubwa kwa sababu walikuwa hawashirikishwi ili kutoa maoni yao wakati wanalinda mila na desturi ambapo amewataka kutunza mila nzuri na kuachana na mila potofu.



Katika hatua nyingine Askofu Sangu amewataka waganga hao kusomesha watoto kwa kuwapeleka shule, pia kuendelea kushirikiana baina ya jamii, kanisa pamoja na serikali ili kuistawisha jamii kimwili na kiroho.



Mwenyekiti wa Waganga wa tiba asili wilaya ya Bariadi Saguda Busaliguki amempongeza Askofu Sangu kwa kukutana na waganga hao ambao zamani walionekana hawana faida kwa jamii wakati wanatibu na kuponya wagonjwa kama zilivyo hospitali na vituo vya afya vya serikali.



Amesema tatizo la mauaji ya watu wenye ualbino liliwatesa sana waganga, lakini baada ya kukaa pamoja na serikali kwa sasa wanafanya kazi kwa amani bila bughuza yoyote huku akiwataka waganga wenzake kufanya kazi kwa kuzingatia maelekezo ya serikali.



"Tatizo limeisha, tulikuwa hatuna elimu na kuna baadhi yetu walikuwa wakifanya mambo tofauti, tunakuomba utusaidie tupate shule katika eneo letu sababu elimu ya watu wa Gambosho bado iko chini sana",  amesema Busaliguki.



Kezia Masuku mkazi wa Kijiji cha Gamboshi amesema Gamboshi ni kijiji kama vijiji vingine na kwamba uvumi wa kuwa kijiji cha wachawi ulienezwa na masuala ya mbina za Wagalu na Wagika.





Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz