Hoteli za Ngurdoto, Impala, Naura kupigwa mnada - EDUSPORTSTZ

Latest

Hoteli za Ngurdoto, Impala, Naura kupigwa mnada




 
Hoteli za Ngurdoto, Impala, Naura kupigwa mnada
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha Masjala Ndogo ya Kazi imeamuru mali za aliyekuwa mfanyabiashara Meleu Mrema zikiwemo hoteli zipigwe mnada kufidia deni la malimbikizo ya mishahara na stahiki zingine zinazodaiwa kufikia shilingi bilioni 1.3.

Mrema alifariki dunia mwaka 2018 na aliacha mali jijini Arusha zikiwemo hoteli ikiwemo Impaka, Naura Spring, Ngurdoto, nyumba za kupanga na viwanja.

Mahakama imemwamuru dalali wa Mahakama, kampuni ya Nutmeg Actioneers Property ya jijini Arusha iuze mali hizo kabla ya Oktoba 15 mwaka huu.

Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Ruth Masama alidai kuna makubaliano yaliyofikiwa na upande wa mdai na mdaiwa kuhusu uuzwaji wa mali hizo.


 
Alizitaja kuwa ni pamoja na viwanja kitalu namba 16, 17, 18 19,20,21,22 na 23 vilivyopo eneo la Uzunguni jijini Arusha hivyo viwe vimeuzwa na wafanyakazi walipwe stahiki zao ndani ya muda huo.

Ofisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Arusha, Emmanuel Mweta aliieleza mahakama hiyo kwamba walifika mahakamani hapo kusajili mkataba wa maridhiano kwa ajili ya kuuza mali za mwajiri ili kufidia madai ya wafanyakazi yanayotokana na malimbikizo ya mishahara.

Mweta alidai kuwa katika mahakama hiyo kuna mashauri yanayofikia 10 yaliyofunguliwa na wafanyakazi dhidi ya mwajiri wao yakiwa na madai likiwemo la mishahara hivyo baada ya kukaa na kukubaliana na mdaiwa imependekezwa ni vema mali hizo ziuzwe.

"Awali mahakama hiyo iliamuru baadhi ya mali za mwajiri huyo kukamatwa na kupigwa mnada lakini tumeamua kukaa chini na mdaiwa na kukubaliana kuliko kuuza mali kidogo kidogo ni bora wauze mali hizo ili kulipa madeni yote ya wafanyakazi"alisema.

Msajili alidai kwamba anakubaliana na maridhiano hayo na kumtaka dalali wa mahakama hiyo,Boniphace Bubelwa kuhakikisha ifikapo oktoba 15 mwaka huu awe amewalipa stahiki za wafanyakazi hao wapatao 234 wakiwemo 68 wa Hotel ya Naura springs na wengine wa Hotel ya Impala .

Mwenyekiti wa wafanyakazi hao, Jacob Joel alisema wanaishukuru serikali kupitia mahakama kwa kuhakikisha wanapata haki zao na wana uhakika Oktoba 15 watapata haki zao.

Alisema kwamba orodha ya majina ya wafanyakazi wanaodai haki zao ipo wakiwemo waliopoteza maisha hivyo kila kila mfanyakazi atapata haki yake.


 
Wafanyakazi waliishukuru serikali kupitia mahakama kwa kusimamia haki zao kwa madai kuwa waliteseka kwa muda mrefu. Baada ya Mrema kuaga dunia mali zilikuwa chini ya kampuni ya Impala Group Hotel chini ya Mkurugenzi, Randy Mrema.

 Kampuni ya Impala Group Hotel ina wakurugenzi watatu, Randy, mke mkubwa wa marehemu Mrema, Janeth Kimaro na dada wa marehemu, Pelagia Mrema.




Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz