Simulizi za Waliopona Corona Wimbi la Tatu....Wasimulia A to Z - EDUSPORTSTZ

Latest

Simulizi za Waliopona Corona Wimbi la Tatu....Wasimulia A to Z


Moshi/Dar. “Mimi kwa hali niliyopitia na yale niliyoyaona, aina za watu tuliowapoteza niko tayari kuchanja saa yoyote chanjo ikinifikia. Sijali imetengenezwa wapi,” haya ni maneno ya Basil Lema, ambaye ameugua wimbi la tatu la corona na kupona bila kutumia oksijeni.

 Lakini Steven John, aliyelazwa kwa siku tano na kutumia mitungi zaidi ya 10 ya oksijeni anasema: “Ninachokishauri watu wajikinge kwa sababu ile kitu (corona) inaingia kirahisi ila inaondoka kwa shida, halafu mstari kati ya kifo na kuishi ni mdogo sana”.

Adamu Stefano (sio jina lake halisi), mfanyabiashara mashuhuri wa Moshi anasema anamshukuru Mungu kwa kumvusha salama, licha ya kuugua corona wimbi la tatu na kuzushiwa hadi kifo kupitia mitandao ya kijamii lakini anasema amewasamehe.

Hizo ni simulizi za watu waliopata maambukizi ya ugonjwa huo wimbi la tatu na kulazwa katika wodi za wagonjwa hao (Isolation ward) katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC kati ya siku tano hadi 14 na kupona.

Lema, ambaye ni Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro na mjumbe wa Baraza Kuu la taifa la chama hicho, alipata maambukizi hayo na kulazwa wodi maalumu katika hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa siku tano kuanzia Julai 14, 2021.

Kiongozi huyo, ambaye aliruhusiwa kutoka hospitalini Julai 18, 2021, ameishauri Serikali kutoa takwimu za wanaopona ugonjwa huo, akisema taarifa za vifo katika mitandao ya kijamii zinapeleka ujumbe kama vile hakuna wanaopona.

Lema alisema wanaopuuza maelekezo ya wataalamu wa afya ya namna ya kujikinga na corona, ikiwamo kuvaa barakoa na kunawa mikono wanafanya dhambi kubwa mbele za Mungu, kwakuwa madhara yake ni makubwa.

“Ingawa sikufikia hatua ya kupumua kwa kutumia oksijeni, lakini muziki wa huu ugonjwa usitamani kuusikia. Leo hii nimepona namshukuru Mungu, lakini ugonjwa umeniachia madhara. Nimekuwa mchovu, uwezo wa kufikiri umeshuka,” alisema.

“Ukweli kama hujadhurika na corona, utapuuza chanjo kama watu wanavyopuuza kuchukua tahadhari kunakofanywa na baadhi yao, huku wangine wakifanya propaganda za chanjo ambazo ni nyingi sana na zimefanyika dunia nzima,” alisema Lema na kuongeza:

“Madhara ni makubwa ya hizo propaganda. Mimi kwa hali niliyopitia na yale niliyoyaona, aina za watu tuliowapoteza, saa yoyote chanjo ikinifikia ya kwanza yoyote ile nitachanja. Sijali imetengenezwa wapi. Nitachanja.

“Nasema hata kama imetengenezwa Lushoto mimi nitachanja ilimradi inaitwa chanjo na nitaokoa maisha yangu na ya wengine. Naomba Watanzania wanisikilize mimi. Mimi nimeumwa corona. Tusikubali propaganda za kijinga,” alisisitiza.

Asimulia alivyoanza kuumwa

Akizungumzia dalili za wimbi la tatu la corona kutokana na kile kilichompata, Lema alisema kwa sasa hazijionyeshi haraka na pale unapojitokeza tayari unakuwa umeshambulia mapafu kwa sehemu kubwa.


“Mimi nilipata bahati. Ni baada ya kumpeleka mgonjwa akafanyiwa vipimo vya kifua na mimi kwa kuwa ni mtu wangu wa karibu nikaona ni vyema na mimi nifanye vipimo. Sasa yeye mgonjwa niliyempeleka hakuwa na corona.

“Nikiri ndiyo njia ya mimi ya kwanza kabisa ya kunusurika. Vinginevyo ningepata madhara makubwa. Pamoja na kuanza matibabu, siku tano tu baadaye niliugua sana nikakimbizwa KCMC, nikakuta pamoja na kwamba nilikuwa natumia dawa, mapafu yangu yalikuwa yamedhurika zaidi. Kwa hiyo nikalazwa na nikaendelea na matibabu mazito kwa siku tano.

“Inawezekana nimepata nafasi hiyo kwa sababu ya kufuatilia matibabu. Hii variant (wimbi) la tatu ni hatari sana kwa sababu inaingia taratibu kimya kimya bila kukupa tahadhari yoyote.”

Anasema dalili alizosikia ni koo kuwasha, kizunguzungu, tumbo kuchafuka, kichwa kuuma, viungo vya mwili kuuma, misuli na mgongo.

Taarifa za vifo pekee zinatia hofu

Lema alisema ni jambo jema kwa Serikali kutoa takwimu za corona, lakini akaishauri inapotoa idadi ya walioambukizwa na wale waliokufa, ione umuhimu wa kutoa takwimu za wanaopona kwa kuwa ni wengi mno.

“Watu wa nje wanaokupa ujumbe kule ndani hawakupi ujumbe wa wagonjwa waliopona. Wanakupa ujumbe wa wagonjwa wanaokufa. Ukikosea ukashika simu, ukiingia kwenye magroup ya whatsapp, facebook instragram ni hatari.”

Felister John

Mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Felister John (37) anasema alianza kupata vipele vidogo mikononi na alipokwenda duka la dawa aliambiwa ni mzio ‘aleji’, akauziwa dawa ya kununua ya kupaka.

Anasema baada ya kuipaka siku moja baadaye alianza kuhisi baridi kali na uchovu.

“Nakumbuka Julai 16 nilikuwa naenda Kariakoo kufanya manunuzi, nilipokuwa natoka nilivaa sweta na nje kulikuwa na jua. Ndugu yangu akahoji nikamwambia nasikia tu sawa, nikiwa huko homa ilizidi nikapumzika sehemu, lakini hali nilipoona inazidi niliamua kwenda hospitali na ndipo nikashauriwa niende Amana,” alisimulia Felister.

Alisema kwa kuwa alichelewa kwenda hospitali, hali ilizidi kuwa mbaya. “Nikiwa nimelazwa jioni ndugu zangu waliomba nipelekwe Muhimbili na huko nilipatiwa usaidizi wa mashine ya kupumua, hii hali ni mbaya na usiombe ikukute, sikuwa na matumaini tena lakini nikiwaangalia wenzangu mule ndani nilihisi nina afadhali.”

Felister alisema alitumia siku tano katika mashine ya kupumua, hali yake ilipotengamaa iliondolewa na baadaye alirudi nyumbani.

Othman Ngachengwa

Othman Ngachengwa (49) anasema aliugua kwa siku chache akiwa nyumbani akaamua kwenda hospitali alikopewa dawa za maumivu kwa kuwa vipimo vya maabara vilionyesha hana tatizo.

“Nilikwenda zahanati ya kawaida nikapima, wakanipa Panadol na kuniambia nikiona hali inakuwa mbaya nirudi. Usiku nilizidiwa na kwa kuwa nafahamu kidogo taratibu niliingia kwenye wavuti wa wizara ya afya na kuomba kufanyiwa kipimo cha Covid, nilihisi ingekuwa hiyo.

“Nilipima. Lakini kilichonishangaza zaidi nilikuwa natokwa na jasho jingi ingawaje ninasikia baridi. Majibu yalivyorudi nilikutwa na maambukizi nikaenda hospitali kwa matibabu,” alisema.

Licha ya kwamba hakukaa katika oksijeni, Ngachengwa alisema ugunduzi wa mapema ulimsaidia kutopata ugonjwa mkali.

Simulizi ya Steven John

Steven John, ambaye ni mkazi wa Soweto mjini Moshi, anasema alianza kujisikia maumivu ya mwili, kujisikia vibaya, kupoteza hamu ya chakula lakini akawa hachukui hatua yoyote kwa kuwa hana uelewa wa dalili za corona, hasa ya wimbi la tatu.

“Nilikuwa najisikia vibaya, viungo vinaumauma. Lakini hadithi za mitaani zilivyokuwa, nikaona kwenda hospitali ni tatizo kwa sababu ni kama vile ndio kubaya zaidi. Nikaona bora nipambane mwenyewe nyumbani.

“Hali ilipozidi kuwa mbaya zaidi nikaenda kituo cha afya, daktari akaangalia akasema hii itakuwa ni pneumonia, akanitoa wasiwasi kuwa si covid. Wakaniandikia sindano za chrystapen na dawa nyingine hivi kama za siku tatu, lakini hali ikawa inazidi kuwa mbaya. Nikapelekwa KCMC nikawekewe oksijeni kabla ya kupimwa, baadaye nikapelekwe kwenye ex-ray na mtungi wangu. Sasa kile kitendo tu cha kushuka kwenye kitanda ili nipimwe sikuweza, ikabidi wanipime hivyohivyo pale kitandani.

“Majibu yalivyotoka wakasema inaonekana mapafu yamepata madhara wakaniambia hiyo ni pneumonia kali. Wakaanza kunipa treatment,” alisema.

“Baadaye nilipata nafuu wakaanza kunipa elimu ya namna ya kurekebisha zile oksijeni. Kwa sababu kadri unavyo improve wanakushauri upunguze zile oksijeni kwa sababu ukiendelea kuifanya iwe nyingi unajilemaza.

“Unaweza kuwa ulianza na oksijeni ya 10 unaanza kurudi 8, 7 au 5 au saa nyingine unaweka oksijeni pembeni. Unajua kuna wakati unakuta gari la mitungi halijaja (kutoka kwenye kinu cha kuzalisha) halafu kuna wenzenu wanapata shida.

“Wewe kama una nguvu na labda umeufunga unaweza kumpa mwenzako ule mtungi akafungiwa. Ile siku ya kwanza nilitumia mitungi 2 na kwa siku tano nilizolazwa pale nilitumia zaidi ya mitungi 10. Yaani ilipita mitungi 10.

“Ila uzuri KCMC wako vizuri mitungi ni mingi. Yaani kuna vitu vingine unaenda pale unashangaa ni Tanzania au wapi na wana watreat (kuhudumia) wote fair (bila upendeleo), hakuna cha masikini wala cha tajiri. Wote mtahudumiwa sawa.”

Barakoa na chanjo

Steven kama walivyo Watanzania wengine, anasikitishwa na kitendo cha baadhi ya Watanzania kupuuzia kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya akisema siku likiwakuta ndio watajua.

Kuhusu Chanjo, Steven anawataka watu wote wanaopotosha chanjo waache kwa sababu hawajui walitendalo.

“Twendeni tukachanje, ugonjwa huu ni hatari sana, haya ya mitandao tuyaacheni” anasema


Mwananchi

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz