Unaweza kuolewa na mtu usiyempenda? - EDUSPORTSTZ

Latest

Unaweza kuolewa na mtu usiyempenda?

Ni siku nyingine tunakutana kwenye kilinge. Tunajadili yale ambayo yanahusu uhusiano, uchumba na hata ndoa. Moja kati ya fikra ambazo zimekuwa zikiwatesa wanawake wengi katika mioyo yao, ni suala la kuolewa na mtu asiyempenda. Kila mmoja amekuwa na mtazamo wake katika suala hili. Kuna ambao wanaamini kwamba unaweza kuolewa na mtu usiyempenda lakini wapo ambao wanaamini huwezi.

Wanaosema unaweza, huwa wanasimamia hoja ya kwamba hamuwezi kufanana kwa kila kitu. Mnakutana ukubwani, hivyo suala la mmoja kutompenda mwenzake, linaweza kubadilishika tu mbele ya safari kama vile mtu anavyoweza kumbadilisha mtu tabia yoyote ile.

Wale ambao wanaoamini huwezi, huwa wanasimamia hoja moja tu kwamba utaishi katika kuudanganya moyo wako, hutafurahia ndoa yako na mwisho wa siku unaweza kuwa msaliti. Hoja hizi mbili zote zina mashiko. Kabla ya kuendelea, tusome kwanza mfano huu ambao msomaji wangu aliyejitambulisha kwa jina moja la Jack alinisimulia. “Kaka mimi naitwa Jack, nina miaka 29. Nina mtu ambaye ananipenda, ananijali na ananithamini lakini tatizo mimi sijampenda.

“Ni mtu ambaye ukimuangalia ana kila sifa ya kuwa mume lakini moyo wangu tu haujampenda. Hata yeye nimeshamwambia, ameniambia kwamba niendelee tu kuwa naye, nitajifunza kumpenda. “Kabla yake, nimewahi kuingia kwenye mahusiano kwa nyakati tofauti na wanaume wengine lakini wote waliniangusha kwa staili tofauti. Nashindwa kuelewa nifanye nini, nimkubali au niachane naye.”

Mfano huo unajieleza kwamba, mwanaume amempenda, anamjali na anamthamini lakini yeye moyo wake haupo. Je unatufundisha nini? Ukitoa nafasi ya watu kumshauri, lipo kundi la watu watakaotoa jibu la moja kwa moja tu, ‘achana naye.’  Kundi hilo linaweza kuwa kundi langu, lakini pia lipo kundi la pili ambalo litashauri kwamba oana naye maana hata kama humpendi, utanufaika na vitu vingine kutoka kwake ikiwemo suala la kupendwa, kuthaminiwa na kupewa kipaumbele.

Wanaokuambia achana naye, litakuwa na hoja kwamba kuingia kwenye ndoa na mtu ambaye humpendi hata kama yeye anakupenda, kwako itakuwa ni mateso tu. Ndugu zangu, kikubwa kabla ya kufanya uamuzi wa kuolewa na mtu yeyote unapaswa kujua unataka kuingia kwenye ndoa kwa ajili gani.

Wapo wanaoingia kwenye ndoa kwa ajili ya kupata watoto, lengo lao likitimia kila mmoja anachukua hamsini zake. Ukiwa mtu wa aina hiyo, unaweza tu kuolewa na mtu yeyote maana mkataba wenu hauwafungi, kuna wakati mnaweza kuachana.

Kwa wale ambao wanaingia kwenye ndoa kwa maana ya kufa na kuzikana, hao kidogo ni tofauti. Hao huwekeza nguvu zao katika kuhakikisha kuwa wanaingia kwenye ndoa na mtu ambaye ana sifa anazozihitaji. Watakuambia ndoa ni mkataba wa kudumu, ukikosea ukaingia na mtu ambaye humpendi, utaishia kuumia maisha yako yote maana kila atakachokuwa anafanya moyo wako hautakuwa ukiridhika.

Utapendwa, utadekezwa na kufanyiwa kila kitu kinachoashiria mapenzi ya dati lakini moyo wako haupo hapo. Ukigundua unataka uhusiano wa kudumu na mtu uliyenaye humpendi, basi jipe muda wa kuendelea kutafakari, kujifunza namna ya kumpenda.

Ukifanya hivyo kwa miezi mitatu, sita au hata miaka na ukaona bado unashindwa kumpenda, ni vyema ukaacha kuingia naye kwenye ndoa kuliko kuingia halafu ukawa na matumaini ya kwamba utajifunza kumpenda halafu isiwe hivyo. Mapenzi mazuri ni yale mkutane wawili mnaopendana.


Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz