Simbachawene "Hali ya Corona ni Mbaya" - EDUSPORTSTZ

Latest

Simbachawene "Hali ya Corona ni Mbaya"AZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema hali ya ugonjwa wa Covid-19 nchini si nzuri hivyo wananchi wasipuuze tahadhari ya kujikinga.

Alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano Mkuu Maalumu wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania.

“Niwaambia Watanzania kupitia mkutano huu wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, chanjo ni jambo jema, hali inayondelea nchini sio nzuri, kwa nafasi yangu kila siku ninapata taarifa za kila mkoa, wilaya ya nini kinaendelea, hali ni mbaya ya vifo,” alisema Simbachawene.

Simbachawene alisema lengo la kusema hayo si kuwatia hofu, lakini ukweli ni huo kwamba Covid-19 unaendelea kuleta madhara vikiwemo vifo.


“Hali ni mbaya ninazo taarifa juzi katika kanisa moja (mkoani Kilimanjaro) wamefanya ibada ya maziko ya majeneza saba, jana (juzi) majeneza nane (leo) jana nimeambiwa sita, sasa wewe endelea kupuuzia ugonjwa huu, usichanje, wakati ukihitaji oksijeni halafu ukaikosa ndio utakumbuka chanjo, wakati huo itakuwa umeshachelewa,” alisema.

Simbachawene alisema serikali inaendelea kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya corona na kuchukua hatua ya kwenda kuchanjwa chanjo kwa hiyari ili kupunguza kasi ya virusi hivyo.

“Niwasihi ushujaa tunaoutafuta haupo, bora sisi waoga tuliochanjwa kuliko kuja baadaye kuitafuta oksijeni na kuokosa, kwa hiyo mwenyekiti nawapongeza sana kwa kumuunga mkono Rais kuridhia chanjo na nyie wenyewe kukubali kuchanja kwa hiari, waambieni ukweli waumini wasikubali kupotoshwa kuhusu chanjo,” alisema Simbachawene.


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Shehe Alhad Mussa Salum alisema wanaunga mkono matumizi ya chanjo nchini na watahamasisha waumini wachanje.

“Tunamshukuru sana Rais Samia, tamko letu tunaridhia uamuzi wa serikali wa kuleta chanjo, tunashukuru imetumika busara na hekima na tumethibitishiwa ni salama, nasi tutaendelea kuwaemilisha wananchi kujikinga na kuchoma chanjo kwa hiari,” alisema Shehe huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima alihimiza wananchi waendelee kujikinga na kukinga wengine kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu.

“Niwaombe tu, msikubali kudanganywa, chanjo ni salama, imethibitishwa na sisi tumeonesha mfano tumechanjwa na hata Rais Samia naye amechanjwa, tunawasisitiza tusingoje hali kuwa mbaya tujikinge, na chanjo hii itasambazwa mikoa yote ili mwenye kuhitaji apate,” alisema Dk Gwajima.
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz