Rais wa Brazil Jair Bolsonaro, 66, huenda akahitaji upasuaji wa dharura baada ya kupata kwikwi sugu zinazoendelea kwa siku 10, ofisi yake inasema.
Anahamishiwa hospitali hadi hospitali nyingine huko São Paulo kufanyiwa uchunguzi wa utumbo .
Katika ujumbe wa twitter , Bw Bolsonaro alisema "atarudi hivi karibuni, Mungu akipenda".
Kumekuwa na wasiwasi juu ya afya ya kiongozi huyo wa mrengo wa kulia tangu alipochomwa matumbo kwa kisu wakati wa kampeni mnamo 2018.
Bwana Bolsonaro alijeruhiwa vibaya katika shambulio hilo na kupoteza 40% ya damu yake. Amekuwa na operesheni kadhaa tangu kuchomwa kisu.
Rais alikwenda katika hospitali ya jeshi huko Brasilia mapema Jumatano, na madaktari walisema wakati huo kuwa atachunguzwa kwa masaa 24 hadi 48.
Lakini baadaye, ofisi ya rais ilisema Antonio Luiz Macedo, daktari wa upasuaji aliyemhudumia Bw Bolsonaro mnamo 2018, alikuwa amependekeza rais ahamishiwe São Paulo kwa uchunguzi wa ziada na upasuaji iwapo italazimu .
Fabio Faria, meneja wa mawasiliano wa Brazil, aliwaambia waandishi wa habari Bw Bolsonaro alikuwa amelazwa asubuhi kabla ya kupelekwa São Paulo.
Mtoto wa rais Flavio aliiambia CNN Brasil kwamba baba yake alikuwa amefanyiwa upasuaji mdogo wa kuondoa maji tumboni mwake kama tahadhari.
Flavio aliongezea kuwa baba yake alikuwa na shida kuongea, lakini ikiwa upasuaji unahitajika haufai kuwa utaratibu mbaya.
Bwana Bolsonaro hapo awali alituma picha yake akiwa amelala kitandani hospitalini, akiwa amewekwa nyaya, na mtu ambaye anaonekana kuwa kasisi amesimama kando ya kitanda chake.
Baada ya miaka miwili na nusu ya uongozi wenye utata, Bw Bolsonaro yuko chini ya shinikizo juu ya jinsi anavyoshughulikia janga la Covid-19.
Mwanzoni mwa mwezi, makumi ya maelfu ya watu waliingia barabarani kupinga madai ya ufisadi unaohusu ununuzi wa chanjo.
Kiongozi huyo wa Brazil amekosolewa sana kwa kukosekana kwa mpango wa kitaifa kukabiliana na janga hilo na wasiwasi juu ya chanjo, mashart ya kutotoka nje na hitaji la watu kuvalia barakoa .
Mwezi uliopita, vifo vinavyosababishwa na virusi hivyo huko Brazil vilipita 500,000 - na kuwa nchi ya pili kwa kiwango cha juu zaidi ulimwenguni baada ya Marekani.
Bwana Bolsonaro mwenyewe alipatwa na Covid-19 mwaka mmoja uliopita lakini amepona kabisa.
Post a Comment