Habari Njema..BOT yatangaza nafuu mikopo sekta binafsi - EDUSPORTSTZ

Latest

Habari Njema..BOT yatangaza nafuu mikopo sekta binafsiDodoma. Kwa mara nyingine, Serikali imetangaza nafuu kwa benki za biashara zitakazosaidia kupunguza riba ya mikopo inayotolewa kwa sekta binafsi, huku kilimo kikipewa nafasi kubwa zaidi.

Awali, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitangaza nafuu Mei mwaka jana ikiziruhusu benki kuwapa nafuu wateja walioathirika zaidi na corona hata mwaka mmoja baadaye, athari za janga hilo bado zinadumu hivyo benki hiyo kutangaza sera zenye nafuu zaidi kwenye sekta ya fedha.

Kuanzia jana, Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga alisema kiwango cha amana ambacho benki huweka BoT kimepungua sambamba na mtaji unaotakiwa kuwapo. Vilevile, BoT imelegeza masharti ya kusajili mawakala wa benki na kuzitaka kutotofautisha kiwango cha riba zinazotoza kwenye akaunti ya Trust inayotumiwa na kampuni za simu zinazotoa huduma za fedha na ile ya akaunti ya akiba.

“Tumeanzisha mfuko maalumu wenye thamani ya Sh1 trilioni wa kukopesha benki na taasisi za fedha, ili ziweze kuikopesha sekta binafsi. Mfuko huu utazikopesha benki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia tatu, ili nazo zikopeshe sekta binafsi kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka,” alisema Gavana Luoga.


Kutokana na mabadiliko hayo yatakayoziongezea benki fedha za kuwakopesha wananchi, BoT imesema zitakazonufaika zaidi ni zile zitakazotoa mikopo ya kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka.

“Benki Kuu ya Tanzania imeondoa sharti la uzoefu wa kufanya biashara kwa angalau miezi 18 kwa waombaji wa biashara ya wakala wa benki. Badala yake, waombaji watatakiwa kuwa na kitambulisho cha Taifa au namba ya kitambulisho cha Taifa tu. “Riba itakayotolewa kwenye akaunti hizi haitazidi riba itolewayo na benki husika katika amana za akiba (savings deposit rate),” alisema.

Profesa Luoga alisema hatua nyingine waliyochukua ni kuanzisha mfuko maalumu wa kukopesha benki na taasisi za fedha, ili zikopeshe sekta binafsi kwa lengo la kuongeza ukwasi na kupunguza riba za mikopo kwa sekta binafsi.

“Benki Kuu imeanzisha mfuko maalumu wenye thamani ya Sh1 trilioni ambao utatumika kukopesha benki na taasisi binafsi.

“Benki au taasisi ya fedha itakayofaidika na mfuko huu itatakiwa kukopesha sekta binafsi kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka,” alisema.

Alisema hatua nyingine iliyochukuliwa na BoT ni kupunguza kiwango cha mtaji kinachotakiwa kuwekwa na benki za biashara kwa ajili ya kuweza kutoa mkopo, lengo likiwa ni kutoa fursa kwa benki za biashara kutoa mikopo zaidi kwa sekta binafsi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

“Benki Kuu imepunguza kiwango cha mtaji kinachotakiwa kuwekwa na benki za biashara kwa ajili ya kutoa mikopo,” alisema.


Benki, wasomi wapongeza

Mwenyekiti wa Chama cha wakurugenzi wa Benki Tanzania (TBA), Abdulmajid Nsekela alisema wanaipongeza BoT kwa ubunifu utakaoongeza utoaji mikopo kwa sekta binafsi.

“Kwa hatua hizi, mtaji wa benki utaongezeka na riba inashuka kwa wateja. Ni ubunifu tuliousubiri kwa muda mrefu...idadi ya mawakala wa benki itaongezeka mtaani,” alisema Nsekela.

Kabla ya mabadiliko haya, benki zilitakiwa kuweka BoT akiba ya asilimia saba ya amana wanazopokea kutoka kwa wateja na kila benki ilitakiwa kuwa na mtaji usipungua Sh15 bilioni. Maeneo haya yote, BoT imetangaza kupunguza viwango vilivyopo.

“Benki zitakuwa na ukwasi mkubwa zaidi. Zitakazopungukiwa zitakopeshwa kwa gharama ndogo hivyo nazo zitakopesha kwa riba nafuu kwa wateja wao. Wananchi wataweza kukopa na kukamilisha mipango yao kwa wakati,” alisema Nsekela ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB.

Wakati wenye akaunti za akiba wakipewa riba ya kati ya asilimia tatu mpaka nne kwa mwaka, Nsekela alisema akaunti ya Trust ilikuwa inapata kiasi kikubwa zaidi ambacho BoT sasa imeagiza kishushwe mna kulingana na hicho.

Alipoulizwa mwenyekiti wa Chama cha watoa huduma za fedha kwa simu za mkononi Tanzania (Tamnoa), Hisham Hendi iwapo hatua hiyo itaathiri biashara yao, aliomba apewe muda kwani hakuwa na majibu ya haraka.

Kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), mhadhiri mwandamizi wa uchumi, Lutengano Mwinuka alisema BoT imekuja na sera ya kuwajali wakulima.

“Watakapowekewa mazingira rafiki ya kupata mkopo, kilimo kitakuwa na mchango mkubwa zaidi,” alisema Mwinuka. Mhadhiri huyo alisema kuimarika kwa sekta binafsi kutatoa ajira nyingi zaidi, hivyo kuongeza mzunguko wa fedha.

Mchumi mwingine, Yoweza Mzava ambaye ni mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Empower Tanzania Kanda ya Kaskazini, alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji.
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz