Meneja Tanroads aanguka akiwa katika ziara ya RC Mahenge - EDUSPORTSTZ

Latest

Meneja Tanroads aanguka akiwa katika ziara ya RC Mahenge


Singida. Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Singida, Matari Masige ameanguka na kupata majeraha kichwani wakati akimuonyesha mkuu wa Mkoa wa Singida,  Dk Binilith Mahenge maendeleo ya ujenzi wa daraja la Sibiti lililopo mpakani mwa mkoa wa Singida na Simiyu.

Tukio hilo limetokea leo Jumanne Juni 22, 2021 Wilaya ya Mkalama mkoani Singida unapotekelezwa mradi huo wakati bosi huyo Tanroads akiwa katika ziara ya Dk Mahenge ya kukagua miradi ya maendeleo ya ujenzi wa madaraja ya Sibiti na msingi yanayotekelezwa na wakala huyo.

Kwa mujibu wa mganga mfawidhi wa hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk Deogratius Banuba, Masige alifikishwa hospitali ya mkoa huo leo jioni akiwa na jeraha kichwani.

"Tumempokea na tunaendelea kumpa matibabu na anaendelea vizuri," amesema Dk Banuba.

Kabla ya kufikishwa hospitali ya mkoa chini ya usimamizi na uratibu wa mkuu wa mkoa, Masige alipatiwa huduma ya kwanza katika zahanati iliyopo Bukundi, Meatu Mkoa wa Simiyu jirani na ulipo mradi wa ujenzi wa daraja hilo.

Awali akitoa taarifa ya hatua za utekelezaji wa mradi huo, Masige amesema kukamilika kwa daraja hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 95 utarahisisha usafiri wa kutoka Singida hadi Bariadi kwa kupunguza urefu wa takribani kilomita 200. Ikilinganishwa na urefu wa kutoka Singida Nzega hadi Bariadi kilometa 674.

Pia, kwa mujibu wa Tanroads daraja hilo lenye urefu wa mita 82 linalojengwa kwa Sh28.5 bilioni  litarahisisha na kufungua huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wanaoishi mpakani wa mikoa ya Singida na Simiyu.





Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz