-->

Type something and hit enter

On
 Umekutana na mwanaume, wote mna maisha ya kawaida, hamna pesa za kihivyo, mnaingia kwenye ndoa, labda na wewe unafanya kazi au hufanyi lakini kama mke unamsaidia mume wako kimawazo. Mume anafungua biashara, lakini unajiona kama uhusiki, biashara inaenda vizuri wewe umekaaa tu, hujui inafanyikaje, hujui wateja anapata wapi, hujihusishi kwa chochote. Labda amekukataza au ni wewe mwenyewe tu, kwakuwa unaona anahudumia kila kitu unaona huna haja ya kuhangaika.


Wanawake wengi wanaohudumiwa kila kitu wanajisahau na kuona tunafanikiwa wote, ananunua gari la kwanza kwa jina lake unaona ni letu, ananunua kiwanja laba mmechanga pesa anaandika jina lake, unasema ni chakwetu, si hakunyanyasi hivyo huoni haja ya kumuambia labda muandike majina yenu au ya mtoto. Lakini unaogopa, unaona kuwa labda ukimwambia kuwa unataka muandike majina yenu atakuona unataka kumdhulumu, lakini labda umemwambia na amekataa, hushtuki kwanini anakataa?

Narudia ndoa wakati huo iko vizuri, mnajenga mpaka nyumba ya tatu, mnafungua duka na biashara kibao na vyote ni kwa majina ya mwanaume. Hapa ingawa wanawake huona ni vyao, utasikia nyumba yetu, gari letu, biashara yetu na wakati mwingine huishia kusema hata tukitengana tunagawana nusu kwa nusu! Nikwambie dada yangu kama hakina jina lako si chako na hakikuhusu, huna maamuzi nacho, najua unawaza mkitengana vitakuwa vyenu, lakini nikuulize je unajua hati ziko wapi?

Lakini wala achana na mambo ya kutengana, hamtatengana lakini wanaume wengi, narudia si wote lakini ni wengi, akipata pesa huwa na kiburi na huu ndiyo wakati wa kutembea na wale wanawake ambao alikuwa anatamani kutembea nao lakini alikua hana pesa na alikua anawaona kama si wa hadhi yake! Huu ndiyo wakati ndugu zake huanza kumpenda na kujifanya “Kaka yetu ana pesa!” bila kujali alikuwa kapauka wakati anakuoa ndiyo wakati wananza kukwambia umempendea pesa na kutaka kukupangia kila kitu.

Najua sasa hivi bado mnapendana ila kama mume wako amefanikiwa peke yake, wewe huna hata kitu kimoja cha jina lako, huna hata kabisahara yaani una pesa kibao lakini ukitaka hata Pedi ni lazima umuombe, na hata hayo magari yote unayoendesha yana majina yake mara nyingi unaishia kunyanyasika. Mwanamke ni lazima kufanikiwa na mume wako, mafanikio hayaambukizwi kwa ndoa wala mahusiano, nilazima ujue kuzifanya hizo biashara, uwekeze kwa jina lako na si kusema “Tuna nyumba…Gari…biashara wakati hata hujui vina majina ya nani?

Kama sasa hivi unaogopa kumwambia mume wangu nataka kuandika jina langu au tuandike majina yetu. Kama sasa hivi huwezi kwenda kununua kiwanja chako na wakati una pesa, kwamba hata kama pesa ni zako basi ni lazima uandike jina lake basi jua ushaanza kunyanyaswa. Nilazima uwe na ujasiri wa kuongea naye na pale anapokwambia kuwa “Inamaana huniamini?” Uwe na ujasiri wa kumjibu kuwa “Nakuamini lakini kuna leo na kesho, hata mimi nataka kumiliki kitu!”

Lakini pia uwe na ujasiri wa kununua chakwako kama unafanya kazi tena bila kificho ajue kuwa kuaminiana ni kwa pande mbili. Hebu jiulize utamuaminije mtu ambaye hataki muandike majina yenu wawili lakini anataka aandike jina lake peke yake? Najua wengi mtalichukulia tofauti kwasababu kiasilia wanaume ndiyo huonekana kama wanatakiwa kumuliki mali, lakini kama mwanamke umechangia acha ujinga wa kumuachia kila kitu peke yake, na kama hujachangia labda huna kazi huu ndiyo wakati wa kutafuta kazi na kuwa na uwezo wa kutafuta kazi yako mwenyewe.

Inawezekana kweli nyumba ya kwanza labda kaandika jina lake, mmechangia wote au hata hukuchagia, lakini ya pili pia anataka kuandika jina lake, wewe kila wakati unakuwa kama shahidi tu. Wakati mnapendana hakuna shida, wakati ndiyo mko chini pesa za kuunga unga mtavumiliana, lakini pesa zikishachanganya ndugu na wanawake wengine kuanza kumuona ni wamaana hapo ndipo mambo huanza kubadilika. kuna mtu kaniomba ushauri wamejenga nyumba tisa zote majina ya mume na mwanaume anamnyanyasa anamwambia hana chake!

Click to comment
 
Blog Meets Brand