USIKURUPUKIE NDOA, ZINGATIA MAMBO HAYA MUHIMU  - EDUSPORTSTZ

Latest

USIKURUPUKIE NDOA, ZINGATIA MAMBO HAYA MUHIMU 

USIKURUPUKIE NDOA, ZINGATIA MAMBO HAYA MUHIMU 

TUNAENDELEA na mada tuliyoianza wiki iliyopita. Narudia tena kukusisitiza kwamba suala la kuingia kwenye ndoa halipaswi kufanywa kiwepesiwepesi kwa sababu ukikosea mtu wa kuingia naye kwenye ndoa, maana yake ni kwamba umeyakosea maisha yote.

Kama tulivyojadiliana wiki iliyopita, unapofikia muda ambao sasa umri wako unakuruhusu kuingia kwenye ndoa, mambo ya msingi ya kuzingatia ni lazima uhakikishe huyo unayetaka kuingia naye kwenye ndoa unamfahamu vizuri.

Usidanganywe na sifa za nje kama ambavyo watu wengi huwa wanadanganyika na baadaye wanaishia kulia kilio cha kusaga meno! Ukifuatilia kwa kina chanzo cha ndoa nyingi kuvunjika muda mfupi baada ya kufungwa, ni kwamba watu wengi wanaingia kwenye ndoa wakiwa hawafahamiani vizuri.

Unaingia kwenye ndoa ukiwa na matarajio makubwa kwa mwenzi wako kuliko hata uhalisia wenyewe, matokeo yake mkishaanza maisha unaona kumbe kile ulichodhani ni almasi kumbe ni kipande cha chupa, ugomvi unaanza.

Uzuri wa nje, kama mwanaume mwenye mvuto, mwenye six-pack, mwenye fedha au kazi nzuri, au mwanamke mwenye sura nzuri, mwenye umbo zuri, aliyejazia na mwenye kazi nzuri, siyo vigezo unavyotakiwa kuvitumia unapotafuta mwenzi wa kuishi naye.

Zingatia zaidi sifa za ndani, ambazo kwa bahati mbaya ni kwamba huwezi kuzijua kirahisirahisi. Huwezi kujua kama huyu ndiye anafaa kuwa mumeo au mkeo kwa kukutana na mtu kwenye daladala na kutongozana pekee.

Upo usemi kwamba misingi imara ya ndoa, huanzia kwenye urafiki. Yawezekana mmekutana kama hivyo kwenye daladala, barabarani, chuoni, ofisini au ni mtu mlikuwa mkifahamiana siku zote lakini hukuwahi kufikiria kama unaweza kuingia naye kwenye ndoa, unapotaka kuingia naye kwenye uhusiano ‘serious’ ambao utazaa ndoa, lazima kwanza muanzie kwenye urafiki.

Jenga urafiki naye, mfanye akuamini na wewe muamini, ni rahisi zaidi kumweleza rafiki yako siri za maisha yako kuliko mpenzi wako, ni rahisi kuonesha tabia yako halisi ukiwa na rafiki yako kuliko ukiwa na mpenzi wako! Kwa hiyo, utagundua kwamba ukiwa rafiki yake kabla ya kuwa mpenzi wake, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kumfahamu kwa undani, na yeye atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kukufahamu kwa kina, kwa hiyo hata ikitokea mmeanzisha uhusiano, utakuwa unayajua mapungufu yake na yeye atakuwa anayajua mapungufu yako.

Baada ya hatua hiyo ya urafiki, hatua inayofuatia inakuwa ni hatua ya uchumba ambapo baada ya kuwa kila mmoja ameshajiridhisha na mwenzake, mtaamua kutoka hadharani sasa ili ndugu, jamaa, marafiki na watu wote wanaowafahamu, wajue kwamba tayari mmeianza safari ya kuelekea kwenye ndoa.

Katika kipindi cha uchumba rasmi, mtaendelea kuchunguzana na baada ya kila mmoja kuridhika na mwenzake, hatua ya mwisho sasa itakuwa ni kuhalalisha uhusiano wenu mbele za Mungu.

Suala muhimu la kujua, wengi huwa wanaamini kwamba baada ya kufungandoa basi mambo yote yamekwisha, kama alikuwa anamuonesha mapenzi mwenzake basi yataanza kupungua hatua kwa hatua akiamini ‘si tayari tumeshafunga ndoa?’

Hayo ni makosa, mnapofunga ndoa mnakuwa mmeanza ukurasa mwingine wa maisha, kwa hiyo yale uliyokuwa unamfanyia mpaka akakubali kuingia na wewe kwenye ndoa, inatakiwa uyazidishe na siyo kuyapunguza. Kama ulikuwa unamheshimu, unatakiwa kuongeza kiwango chako cha heshima maradufu, kama ulikuwa unampenda basi unatakiwa kumpenda maradufu, ukiyafanya hayo basi utakuwa unajijengea mazingira ya kudumu kwenye ndoa yako na utayafurahia mapenzi. Tukutane Ijumaa ijayo kwa mada nyingine nzuri.



Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

Edusportstz