;
Upo Bize, Sawa Lakini Unakumbuka Kutenga Muda Kwa Ajili Ya Umpendaye? - EDUSPORTSTZ

EDUSPORTSTZ

BREAKING

TUFOLLOW UWE MIONGONI MWA WANAOTUMIWA HABARI KILA SIKU

Sunday, 28 June 2020

Upo Bize, Sawa Lakini Unakumbuka Kutenga Muda Kwa Ajili Ya Umpendaye?

Upo Bize, Sawa Lakini Unakumbuka Kutenga Muda Kwa Ajili Ya Umpendaye?

NI siku nyingine tunapokutana katika uwanja wetu huu mzuri, tukijuzana na kuelimishana kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo mapenzi. Mada yetu ya leo ni kama inavyojieleza hapo juu. Je, mara ya mwisho kwa wewe na mpenzi wako kupata muda wa kukaa pamoja au kutoka ‘out’ ilikuwa ni lini? Una desturi ya kutoka na umpendaye, mkaenda mahali tulivu ambapo mtapata muda wa kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu maisha na mapenzi?

Kama jibu lako ni hapana, unaishi kwenye mapenzi yaliyokosa uhai. Maisha yanaenda kasi sana, wanandoa wengi au watu ambao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi, wanajikuta wakikosa kabisa nafasi ya kuwa pamoja kutokana na kila mmoja kuweka kipaumbele katika kazi, biashara au shughuli nyingine za utafutaji pesa au malezi ya watoto.

Matokeo yake, watu wengi wanaishi kwa mazoea tu lakini katika uhalisia, mapenzi yanakuwa yamepungua sana au hayapo kabisa. Watafiti wa mapenzi wanaeleza kwamba hakuna kazi ngumu kama kuishi pamoja wewe na mpenzi wako, iwe ni kwenye ndoa au uhusiano wa kawaida wa kimapenzi kwani ni rahisi sana watu kuchokana.

Hata kama unampenda vipi, lazima kuna muda utamchoka au utachoshwa na mazingira ambayo mmekuwa mkiishi siku zote. Unapofikia hatua hii, kitu pekee kinachoweza ku-refresh akili na hisia zako, ni wewe na umpendaye kutoka pamoja na kwenda sehemu tofauti kama ufukweni, hotelini au sehemu yoyote tulivu ambayo mtakaa pamoja, mtakunywa au kula na kufurahi.

Kitendo hiki kinatajwa kuwa siri kuu ya kufufua mapenzi na kuondoa ile hali ya kuchokana. Haijalishi umeishi kwa muda gani na mpenzi wako, hata kama mna miaka kibao, lazima muendelee kutoana out mara kwa mara.

Hata kama tayari mmeshazaa watoto na wamekuwa wakubwa, suala la out halikwepeki kama mnataka kuishi kwa amani na upendo. Wengi wanaamini kwamba mpenzi mpya pekee ndiye anayetakiwa kutolewa ‘out’, jambo ambalo siyo sahihi. Mkirudi, kila mmoja atashangaa mapenzi yake kwa mwenzake, yatazidi maradufu, kama kulikuwa na migogoro ya hapa na pale, itaisha na mtaendelea kuishi kwa amani na furaha.

Wengi tunasumbuliwa na kasumba kwamba ili kumtoa mpenzi wako out, ni lazima waleti yako iwe imejaa, lazima mkatumie fedha nyingi au lazima umpeleke sehemu ya gharama.

La hasha, siyo lazima kabisa. Kwa mfano, inakugharimu nini wewe na mpenzi wako kutoka na kwenda ufukweni,
mkaagiza soda, maji au vinywaji mnavyovipenda, mkakaa kwenye mchanga wa bahari na kupunga upepo mwanana? Hata kama hakuna ufukwe hapo mnapoishi, mnaweza kutoka na kwenda sehemu yoyote tulivu, iwe ni kwenye uwanja wa mpira muda ambao hakuna watu, sehemu za milimani au mahali popote ambapo mtakuwa wawili tu, inatosha kabisa.

Unaweza kununua matunda, vinywaji au vitafunwa mnavyovipenda, mkaenda navyo mpaka sehemu mliyoichagua, siyo lazima uwe na fedha nyingi. Ili mtoko wako na umpendaye ukamilike, kuchagua sehemu ya kwenda ni jambo la kwanza lakini kubwa zaidi, lazima ujue kwamba mkiwa ‘out’, unapaswa kufanya nini ili mpenzi wako afurahi na kufufua upya hisia za mapenzi ndani ya moyo wake.

Ni matumaini yangu kwamba utakuwa umejifunza kitu kikubwa na nakuhakikishia kwamba ukiyafanyia kazi haya, utayafurahia mapenzi. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo chini.
Pakua App ya 'EDUSPORTSTZ NEWS' Uweze kufurahia Habari zote za Mapenzi; Udaku, Ajira na Michezo kila siku Ipo Google Playstore, Kwa Ku BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD Kwenye Simu yako Utasoma habari zote hata kama hauna MB