MIMI NA NAFSI YANGU; MUME WANGU NYANYUKA UWAONE WATOTO WAKO! - EDUSPORTSTZ

Latest

MIMI NA NAFSI YANGU; MUME WANGU NYANYUKA UWAONE WATOTO WAKO!

IDD MAKENGO
Naandika huu ujumbe huu nikiwa juu ya Kaburi la mume wangu, naomba univumilie Kaka Iddi kwani nina mengi ya kuandika, sina nia ya kukuchosha lakini baada ya Makala yako ya jana nilitamani sana kama mume wangu angeamka kutoka katika Kaburi lake na kuja kukusoma angalau kwa dakika tano tu basi labda hii leo na mimi ningekua na furaha.
Mimi ni Mama wa miama 40, miaka 15 iliyopita nilifunga ndoa na mume wangu mpendwa, wakati huo mimi ndiyo nilikua nimemaliza Cheti cha ualimu wa shule ya msingi na nilipangiwa kufundisha shule moja hapahapa Dar. Mume wangu yeye alikua ni meneja wa Benki tena kijana kabisha hivyo yeye kidogo alikua na hela.
Kwakua shule niliyokua nikifundisha haikua mbali sana na nilipokua naishi niliendelea kufundisha. Mume wangu alikua ni mtu wa upendo sana, alinipenda na kunijali, namshukuru Mungu hakuwahi kuninyanyasa, hata ndugu zake ambao karibu wote nimeishi nao na kuwalea kwangu nao walinipenda na kuniheshimu kama mke wa Kaka yao, Mama mkwe wangu naye alinipenda, Baba mkwe alishafariki tangu mume wangu wakiwa wadogo.
Ilikua ni familia yenye ukaribu sana, mara nyingi mambo yao walikua wakifanya pamoja. Tatizo kubwa katika ndoa yetu nikuwa mume wangu alikua ni kama haniamini. Kila kitu alikua akifanya kimyakimya, akiwashirikisha sana ndugu zake hasa wakiume na Mama yake mzazi. Katika mali za mume wangu Mama yake alikua ndiyo kila kitu, walikua wakishauriana na kufanya mambo yao kimyakimya.
Mara nyingi nilikua nashtukia tu kitu kimefanyika, kwa mfano mume wangu alikua anaweza kununua kiwanja mpaka kuanza kujenga, unakuja unashtuka nyumba iko kwenye lenta. Ingawa alikua haninyanyasi lakini kama ukimuuliza mambo kuhusu mali basi huwa mkali na majibu yake huwa ya kukatisha tamaa, kwa mfano wakati mmoja alikua anajenga nyumba.
Mimi sikuwa nikijua chochote, siku moja wakati ninafua nilikuta list ya vitu alivyonunua, niliamua kumuuliza alinijibu ni kweli anajenga na nilipomuuliza kwanini hanishirikishi alinijibu “Kwani ulitaka uchangie nini! Hako kamshahara kako kanaweza kununua hata misumari?” Kusema kweli niliumia sana hasa ukiangalia kua mimi niliuliza kwa uzuri tu. Amekuja kunionyesha nyumba anaezeka.
Siku nyingine alinunua Gari nikajua kupitia kwa Mama yake wakati anaongea anajisifia kua “Sasa tuna Daladala tatu!” Wakati huo nilikua sijui hata kama ana hiyo moja. Kila nilipomuuliza alikua akisema nataka nijue ili nini? “Unataka kuniibia au hapa ndani kwani unakosa nini? Kuna siku nilishakuuliza kuhusu hako kamshahara kako? Sasa kwanini utake kujua mambo yangu?”
Sikua na majibu zaidi ya kunyamaza kwani kila inapotokea tumekwaruzana kwa namna hiyo basi huweza kununa hata siku tatu mpaka niombe msamaha mimi. Niliamua kukaa kimya kwani kweli alikua ananihudumia ingawa kwa suala la kusaidia ndugu zangu alikua anakua mkali, hivyo mshahara wangu ndiyo nilikua nikitumia kuwasidia, kutuma matumizi na kusomesha wadogo zangu.
Maisha yaliendelea na kwakua nilitaka amani basi nilivumilia, siku moja nilikua nimetoka kazini, nakumbuka ilikua ni mwaka 2013, nilikua na ujauzito wa mtoto wetu wa tatu na wa mwisho. Nilikua sijisikii vizuri kwani mimba ilikua inanisumbua, nilimpigia simu mume wangu lakini haikupokelewa, nilipiga sana kisha nikamtumia meseji lakini hazikujibiwa.
Haikua kawaida yake kwani hujali sana, wakati wa ujauzito huwa makini sana na kwakua mimba zangu hunisumbua hataki hata nipande Tax hivyo kama ni kwenda kazini hunipeleka na wakati wa kurudi huja kunichukua au kumtuma Dereva wake. Nilimpigia simu Dereva wake lakini nayo iliita tu bila kupokelewa. Huku nikijua kua atanigombeza niliamua kupanda Tax mpaka nyumbani ambapo hakukua mbali sana.
Ile kushuka tu nikashanga kuna watu wamejazana, walikua wamesimama nnje ya Geti la nyumba yetu mafungu mafungu. Nilipata wasiwasi kidogo na niliposhuka tu akina Mama ambao walikua pale nnje walinifuata, nilijikuta naanza kupiga kelele na ikichanganywa kutokupokea simu kwa Mume wangu nilijua tu kuna kitu kibaya kimetokea. Kweli nilipoingia ndani niliambiwa mume wangu alikua amefariki kwa ajali ya Gari na Dereva wake yuko mahututi Hospitalini.
Nguvu ziliniishia na kupoteza fahamu, na nilipozinduka nilikua Hospitalini, nilitaka kwenda kumuona mume wangu lakini walinikatalia katakata, alikua kaharibika sana, hata katika kuaga jeneza halikufunguliwa lakini mimi nililazimisha kumuona. Mpaka sasa ile picha hoiondoki kichwani kwangu na kila nikikumbuka huwa nalia sana kwani, sikupata hata dakika tano za kumuuguza mume wangu mpendwa.
***
Baada ya mazishi na kumaliza arubaini ilikua ni wakati wa kugawa mali za marehemu, kutokana na namna walivuokua wakiishi na ndugu zake sikuona kama kutakua na shida, aliwasomesha wadogo zake na wote walikua na kazi nzuri na wakati wa uhai wa mume wangu hawakuwahi kuonyesha kama wana shida na mali zake.
Siku ya kugawa mali na kuchagua msimamizi kikao cha ukoo kiliitishwa, kumbuka bado nilikua mjamzito. Ile kuanza tu walikubaliana kua mimi ndiyo nitakua msimamizi wa mali za marehemu nikisaidiwa na mdogo wake mmoja wa kiume, hawakutaka kuchukua chochote, nilimshukuru Mungu kwa hilo.
Kimbembe kilikua katika kukabidhiwa hizo mali, walisoma kua mume wangu alikua akimiliki Gari moja ya kutembelea, na viwanja viwili, kimoja kilikua Kijijini kwao na kingine kilikua hapahapa Dar ambacho nakumbuka hata si yeye aliyenunua, alikua kama shahidi tu kwani mimi ndiyo nilinunua kwa hela yangu ya mshahara.
Walijifanya kunikabidhi kuhu Mama mkwe akisema “Najua mwanangu hakuacha vitu vingi lakini mimi bado ni Mama yenu, ni wajibu wangu kuwatunza wanae, hamtakosa kitu, utakaa kwenye nyumba yangu hiyo mpaka utakapoamua kuolewa lakini watoto wake watakaa tu!” Nilikua natetemeka kwa hasira, niwazi nilikua nadhulumiwa kijanja na sikua tayari.
Nilikua najua haki zangu nazijua mali za marehemu hivyo sikua tayari kuona nadhulumiwa, palepale katika kile kikao niliwaambia kabisa kua najua marehemu ana nyumba zaidi ya tano, tatu nilikua nazijua na nilishuhudia ujenzi wake na mbili nilimkuta nazo, ana magari matatu ya biashara na matatu ya kutembelea. “Mama wewe mwenyewe ndiyo uliniambia kuhusu magari ya mume wangu.”
Niliongea sana lakini hawakupaniki, nikama walikua wamejiandaa kwani baada ya kuongea vile, Mama mkwe alitoa briefcase iliyokua na nyaraka mbalimbali, niliikumbuka, ilikua ni ya mume wangu, mara nyingi alikua akija nayo na kuweka vitu vyake, nilikua sijawahi kuiona pale nyumbani na kamwe hakutaka niiguse. Alifungua na kutoa nyaraka mbalimbali na kuondoka nayo.
Kulikua na hati za viwanja kama vitano hivi, hati za nyumba saba, kadi za magari nane na nyaraka nyingine nyingi, vyote vilikua na majina ya Mama mkwe. Mume wangu aliandika mali zake zote kwa majina ya Mama yake hivyo hatukua tukimiliki chochote, nilikumbuka mara kadhaa alikua akisema mtu pekee alityekua akimuamini alikua ni Mama yake tu.
***
Nikiwa naamini kua ni haki za wanangu sikukubaliana na ile hali, nilienda Mahakamani kudai mali za mume wangu, lakini huko nako nilishindwa kwani hakukua na mali za mume wangu. Hakukua na ushahidi wowote kuwa mume wangu alijenga chochote, kila kitu mpaka risiti za vitu alivyokua akinunua mume wangu vilikua katika ile briefcase hivyo alikua navyo Mama mkwe wangu.
Ingawa alikua hana kazi yoyote lakini alikua na watoto na wote walishikana kwa pamoja kua walimsaidia Mama yao kujenga, lakini pia kulikua na Biashra za mume wangu ambazo zilikua na majina yake. Nilirudi patupu. “Sitakutupa mwanangu, huna haja ya kuhangaika na kuhuzunika, hizi mali si zangu ni za watoto wa marehemu, mimi ni kama msimamizi tu.
Aliniamini mimi kama Mama yake hivyo siwezi kula hata senti kumi ya wajukuu wangu.” Mama mkwe aliniambia baada ya kutoka Mahakamani na kushindwa kesi. Pamoja na kuwashitaki lakini hawakuniwekea kinyongo, waliendelea kunisaidia na kweli, Mama mkwe wangu alihakikisha hatukosi chochote, aliacha tutumie nyumba, magari na alikua akilipa ada na kutoa matumizi ya nyumbani.
Kwa mwaka mmoja ambao Mama mkwe wangu alikua hai niliishi vizuri tu bila tatizo lolote. Lakini Mama mkwe alianza kuumwa, alikua na tatizo la Figo na wakati wakijiandaa kumfanyia upasuaji ili apandikizwe Figo nyingine alifariki Dunia, ulikua ni kama mwaka na nusu hivi baada ya mume wangu kufariki. Lilikua ni pigo kubwa kwa familia kwani yeye ndiyo alikua anaishikilia na kuisimamia.
Hapa ndipo maisha yangu na wanangu yalibadilika na hapa ndipo nilijikuta namchukia marehemu mume wangu. Mali za mume wangu bado ziliendelea kubaki katika majina ya Mama yake, hivyo baada ya kifo chake ilimaanisha kua mirathi ilibaki kwa wanae watano ambao walikua hai. Mume wangu tayari alishafariki hivyo hakuambulia kitu.
Bila aibu wala kufikiria kua zile mali zilikua za Kaka yao waligawana kila kitu, kuanzia magari nyumba na biashara za mume wangu. Mimi na wanangu tuliachiwa nyumba ambayo tulikua tukiishi tu. Ndiyo walikua na haki ya kuchukua kwani vile vitu vilikua ni vya Mama yao, nilichanganyikiwa, watoto waliokua wanasoma shule nzuri ilibidi kuwatoa kwani sikua na uwezo wa kuendelea kuwalipia ada.
Ndugu wa mume wangu waliona kwakua nina kazi na tayari nina nyumba basi hakuna shida, walijifanya kunipenda na hata kutaka kubadilisha hati ya nyumba ili isomeke jina langu. Nikama walitaka kujitenga na mimi, hawakutaka kushirikiana na mimi na kweli walijitenga na mimi baada ya kugawana mali sikuwaona tena.
Kila nilipoenda kuwalilia matatizo walilalamika hali ngumu huku wakitupiana mpira juu ya nani wa kutusaidia. Lakini kwakua Mungu alinipa mikono miwili sikukata tamaa, sikutaka kulalamika sana kwani ningekua na kufuru na naamini ningekua na muumiza marehemu mume angu. Niliijua nia yake, kama wanaume wengine alikua haamini wanawake.
Aliwaamaini ndugu hasa Mama yake akiamini hawezi kumdhulumu, hakumdhulumu kweli lakini alisahau kuwa Mama yeke hakua Mama yake peke yake, alikua Mama yake na ndugu zake. Lakini maisha ilikua ni lazima yaendelee na angalau wanangu walikua na sehemu ya kulala. Lakini miezi mitatu tu baada ya Mama mkwe kufariki na kukabidhiwa nyumba walikuja watu wa Benki.
Ilionyesha kuwa Mama mkwe wangu alichukulia ile nyumba mkopo hivyo nilitakiwa niwe na lipa kila mwezi. Mpaka leo sijui ni nani aliuchukua ule mkopo kwani ingawa nyaraka zote zinaonyesha kuwa ulichukuliwa na Mama mkwe wangu lakini nina uhakika ni shemeji zangu kwani ndiyo walikua wakihusika na mambo ya fedha na Mama mkwe wangu alikua hajui.
Walikua wamechukua mkopo wa Shilingi milioni 80, zilikua ni pesa nyingi sana kwa mimi kuweza kulipa, ilinibidi kuuza Gari ambayo ilibaki kwa jina la mume wangu, sikuweza kulipa na kwakua sikutaka kupoteza nyumba kwaajili ya wanangu ilinibidi kutumia mshahara wangu kulipia mkopo huo kila mwezi. Kama mnavyofahamu mshahara wa Mwalimu haukutosha kabisa hivyo nilikua nikukopa kopa kwa watu.
Ilibidi kupangisha ile nyumba sehemu kubwa mimi na wanangu kubaki na vyumba viwili tu ambavyo tulitumia mimi na watoto wangu watatu. Ndugu wa mume kila mtu alikua bize na mambo yake, hakuna aliyetaka kunisaidia wala aliyekubali kua alikopa yeye. Lakini sikua na chakufanya, maisha ilikua lazima yaendelee na wanangu ilikua ni lazima wale.
Mwaka jana mambo yalizidi kuwa mabaya, katika zoezi la uhakiki wa vyeti lilinikumba. Wakati namaliza kidato cha nne matokeo hayakua mazuri hivyo nilitumia cheti cha Dada yangu ambaye aliolewa, lakini nayeye baada ya kukaa kwenye ndoa na mambo kua magumu alimaua kujiendeleza hivyo wote tulikua walimu, uhakiki ulipoanza tu niliamua kujitoa mimi.
Hii ikimaanisha sikua na kipato chochote. Hapa ndiyo nilihisi kuchanganyikiwa, kumbuka bado sijamaliza deni Benki, nyumba nimepangisha na kodi yote napeleka kulipa Benki, kazi sina na watoto wote wanasoma. Wana mahitaji na ndugu wa mume wangu wakitoa elfu kumi kwa mwezi watapiga mpaka na picha za kutuma Instagram kuonyesha kua hawajawasahau watoto wa ndugu yao.
Sijakata tamaa bado, nilikua na Charahani sasa hivi nashona kama fundi kuweza kuhudumia familia. Naandika haya yote nikiwa juu ya Kaburi la mume wangu, natamani anyanyuke awaone watoto wake wanavyoteseka kwakua tu hakuniamini. Simlaumu yeye peke yake najilaumu na mimi kwa kuwa mjinga kuacha kupigania haki yangu wakati mume wangu akiwa hai.
Samahani Kaka Iddi kwa kukuchosha ila nilitaka nilitoe hili tu ili kama kuna wanaume ambao wanawaona wake zao kama maadui wajue tu kua sisi wanawake ndiyo tutahangaika na watoto wao pindi Mungu akiwachukua na kama kuna mwanamke kakaa na kubweteka kama mimi aamke kwani mateso ninayopata sasa na nikiangalia ndugu zake wanavyofaidi nina uhakika mume wangu akinyanyuka atakufa tena kwa maumivu.
***MWISHO
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz