Jinsi ya kumjibu mpenzi anapouliza ‘Unanipenda Kiasi Gani?’ - EDUSPORTSTZ

Latest

Jinsi ya kumjibu mpenzi anapouliza ‘Unanipenda Kiasi Gani?’

Wana jopo, karibuni kwenye jamvi letu jipya lililotandikwa kwenye kona maridhawa ya mapenzi.
Hii ni kona iliyoandaliwa maalum kwa ajili ya kujuzana mambo mawili matatu kuhusu masuala ya mahusiano ya mapenzi ambayo ‘yanafanya dunia izunguke’ bila sisi kujua tunazunguka nayo.
Wapo waliowahi kusema mapenzi ni ‘ukichaa’ kwa sababu kila wakitafakari baadhi ya matukio waliyoyafanya kutokana tu na kupenda wanaamini hawakuwa katika hali ya kawaida kiakili! Lakini wapo wanaoamini hakuna hisia nzuri na zenye busara iliyopitiliza kama hisia za mapenzi ambazo hazifichiki hata akipewa ‘bingwa wa kuficha siri za dunia’.
Anyways, tuweke kando hizo blabla… leo tuangazie swali ambalo karibu kila mmoja aliwahi kuuliza ama kuulizwa na mpenzi wake au hata mtu anayemshawishi kuwa mchumba. “Baby, unanipenda kiasi gani?” ni swali la mtihani ambao ulishavuja karibu kwa kila mtu, lakini hata anayeliuliza huwa hajui majibu.
Hivyo, wa kuliwekea alama hutegemea tu kile anachosikia, hata kama sio sahihi anaweza kuweka alama kubwa ya ‘vema’.
Wakati unajibu swali hili, nakushauri usihangaike hata kidogo kutafuta vipimo unavyovijua wewe hata kama ni kipimo cha ukubwa wa dunia na bahari zote. Picha itakayojengeka kichwani kwa unayemwambia itakuwa ya ‘kusadikika tu’.
Usilijibu swali hili kama unavyojibu maswali mengine ya kawaida anayokuuliza, jaribu kutengeneza kwanza mazingira mazuri ya haraka ya kuishika akili yake. Mvute zaidi umakini uwe kwako. Macho yako na muonekano wako uonekane kweli unataka kujibu swali muhimu la mapenzi sio mtihani wa mwalimu ‘Kabuche’. Lol. Hapo utakuwa umetengeneza mazingira ya ushindi.
Mwite jina zuri mwanzo, mfanye ajisikie anaongea na mpenzi, kama mko wawili mshike mkono taratibu, nyuso zitazamane… macho yako yatakusaidia kuzungumza zaidi kinachoelezwa na mdomo.
lovers-looking
Kama wewe ni muongeaji sana, sauti yako ishuke kidogo iwe ‘romantic’. Hii ni kwa sababu moyo wa muuliza swali hupanuka na akili yake hutamani kusikia neno zuri sana kutoka kwako ambalo hata yeye halijui… hivyo inategemea utamwambia nini.
Angalia baadhi ya majibu yanayoweza kufaa, sio lazima uyakopi haya yangu… chukua kama mfano.
Tafadhali sana narudia, usitafute kufananisha nyota, bahari, mchanga na vingine, hii ni dunia ya dijitali na hiyo ilikuwa mifano ya zamani, huenda isimsisimue sana. Ni kama stori ya kunywa maji na kukuona kwenye bilauli!
“Baby, ingawa hakuna kifaa cha kupimia kiasi cha mapenzi, naamini mapenzi hayapimwi kwa maneno bali vitendo. Na hakuna ajuae kipimo cha tendo zaidi ya mtendewa. Kipimo cha mapenzi yangu kwako ni wewe… matendo yangu yanaongea, naomba unipe alama nazostahili. Lakini naamini nakupenda kiasi kisichoelezeka lakini kile kinachougusa moyo wako ni sehemu tu.”
“Baby, nakupenda kiasi kwamba kwamba naamini siwezi kupenda zaidi ya hapa.” Hapa ni kama unasema kuna kipimo na ushafika mwisho wa alama husika.
“Naamini ni neno ‘upendo’ pekee linaloweza kuupima upendo wangu juu yako. Siwezi kusema ni kiasi gani kwa sababu ni vigumu kusimulia kwa uhalisia maumivu ya kidonda, lakini ninaamini hiki ninachokisikia juu yako ndio maana halisi na sahihi kabisa ya neno upendo uliokomaa.”
Hata hivyo, majibu kutoka kwa mtu asiyependa kweli yanaweza kumuumbua tu hata akiyasema vyema kwa sababu macho yanayongea zaidi ya mdomo kwenye mapenzi. Chukua hii.
Maneno matamu yaendane na matendo matamu, hapo ndio utaona kweli mapenzi hayana kiwango cha elimu.
Kumbuka kuchagua maneno kutakusaidia kudumisha penzi lako, usiropoke tu majibu kisa umemzoea mwenzio ama unataka kuonekana mjuaji sana, itakugharimu. Katika mapenzi kila alama ni muhimu kuliko hata umuhimu unaoujua, hata kicheko chako tu kinaweza kushusha alama. Beba mapenzi kwa umakini wa hali ya juu zaidi ya kutembea juu ya trey la mayai.
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz