HIVI UNAJUA KWA NINI VIJANA WA MJINI HAWAFANIKIWI - EDUSPORTSTZ

Latest

HIVI UNAJUA KWA NINI VIJANA WA MJINI HAWAFANIKIWI


Inawezekana na wewe umekuwa ukijiuliza swali hili lililokuwa likinitatiza kila siku kwamba kwa nini vijana wengi wanaoishi mjini huwa hawafanikiwi kama wale wanaotoka vijijini na kuja mjini? Hili ni jambo linalowatesa watu wengi, wengine wamekuwa wakilalamika kwamba kwa nini fulani ametoka kijijini, kaja mjini kafanikiwa na wakati wao ni maborn town lakini bado wamepigika kitaa.
Nimefanya uchunguzi, nimezungumza na vijana wengi na nimefanikiwa kupata baadhi ya majibu ambayo leo hii ningependa kuzungumza nawe, labda tushauriane mawili-matatu, kama kuna hatua za kuchukua, basi uchukue ili na wewe ufike pale unapotakiwa kufika.
Kumbuka kwamba mimi pia nilizaliwa kijijini, nikakulia huko, nikaondoka na kuja ARUSHA ambapo sikuwa na ndugu, mvua zilikuwa zangu na jua lilikuwa langu. Sikuwa na pa kwenda, katika kituo cha mabasi ya mkoani hapo ndipo nilipokuwa nikilala.
Niliumwa sana na mbu, lakini katika hayo yote, sikujuta, maumivu niliyosikia nilijipa moyo kwamba kuna siku yangekoma, kweli, leo unapozungumza watu waliyoyabadilisha maisha yao kutoka kijijini na kuja mjini, basi mtoto wa mkulima, mimi pia nitakuwepo kwenye orodha hiyo.
Hebu ngoja nikwambie kwa nini vijana wengi wa mjini hawafanikiwi kirahisi.
KUJISHTUKIA
Mjini kuna ajira nyingi kuliko vijijini ambapo ajira yao ni moja tu, kulima. Vijana wengi waliozaliwa mjini huwa hawafanikiwi kirahisi kwa kuwa wanajishtukia. Leo unaweza ukamwambia kijana wa mjini auze sabuni kwa kutembeza, lakini anaogopa, anamuonea aibu mtu fulani atamuona, lakini biashara hiyohiyo, mtu kutoka kijijini anafanikiwa na mwisho wa siku anaachwa kijana wa mjini akilalamika.
Unapoamua kutafuta maisha, usiogope kuchekwa, usiogope kudharaulika. Najua wengi hawataki kubezwa wanapofanya biashara za kutembeza pipi au nyingine, lakini kumbukeni kwamba hata matajiri wakubwa mnaowaona katika Tanzania hii, wameanzia hukohuko, kwenye biashara ndogo, zikakua na kuanzisha kubwa.
STAREHE
Hii nayo ni sababu mojawapo. Vijana wengi wa mjini, baada ya kupata fedha kidogo, wanachokifikiria ni starehe tu. Kijana wa mjini yupo radhi atumie hata elfu hamsini kwa usiku mmoja tu na wakati kiasi anachoingiza ni kidogo.
Kabla ya kufanya matumizi makubwa, hebu jiulize, je kuna umuhimu wa kufanya hivyo? Kama unataka kwenda sehemu kula bata kwa hamsini hiyo, hebu jiulize, je usipokwenda siku hiyo, utakufa? Je usipotumia kiasi hicho cha fedha maisha yatakwisha? Je utachekwa? Kama jibu lako ni hapa, basi achana nalo, acha fedha zako ziwe akiba na zikusaidie hapo baadaye.
Unapoanza starehe, kunywa pombe kupindukia, huwezi kufanikiwa, kila siku utakuwa mtu wa kulalamika. Nafurahi kumuona kijana akiendesha gari, lakini wakati anaendesha gari, nafurahi zaidi kumuona akiwa na biashara inayomuingizia kipato kikubwa.
Huwa sifurahii kumuona kijana akiendesha gari, huku mafuta akitumia mshahara wake. Mtu kama huyu kufanikiwa ni vigumu, acha mshahara ufanye mambo mengine, gari ni gharama, wakati mwingine linaharibika, linahitaji vifaa vya gharama, je mshahara ndiyo utakaotumika tu? Na kama ndiyo, je fedha za matumizi na kufanyia mambo mengine zitatoka wapi?
KUJISAHAU
Ndiyo! Wengine wanajisahau. Kama leo mtu akafanya kitu kikamuingizia laki moja, basi kesho hawezi kufanya kitu kama hicho, atakwambia mpaka fedha hizo ziishe kwanza. Hivi umekwishajiuliza kwa nini makonda wengi wa daladala hawafanikiwi?
Wengi wanapata fedha nyingi, kwa siku konda anaweza kupata hata shilingi elfu thelathini mpaka hamsini, kweli mtu wa namna hiyo hawezi kufanikiwa? Kuna mtu anafanya kazi kwa mshahara wa laki mbili, na anafanikiwa, kwa nini mtu kama konda hafanikiwi?
Nimewahi kukutana na makonda wengi, kauli zao ni kwamba wanapata fedha kila siku, leo akipata elfu hamsini, kesho inaingia nyingine sasa kwa nini niiweke hii ya leo? Ukisikiliza sababu zao unaweza kuona zina mashiko lakini hazina mashiko yoyote.
Mchukulie mtu kama Mengi au matajiri wengine, wanaingiza kiasi gani? Mbona wanajua kuweka akiba na huwasikii wakisema leo imeingia hii, nitumie yote kwa kuwa kesho itaingia ny
ingine? Ni lazima fedha tunazozipata tuziweke matumizi sahihi na tusijisahau kwa kujipa moyo kwamba kesho itaingia nyingine.
Kama tukipambana, tukiingiza fedha na kufanyia vitu vya msingi, tusiporidhika, tusipojisahau basi hii Tanzania itakuwa na mabilionea wengi sana na kila kijana atakuwa na maisha mazuri.
KUKOSA UBUNIFU
Kuna wengine wanapata fedha lakini wanapofungua biashara, wanakosa ubunifu. Kabla ya kufungua biashara fulani ni lazima uangalie je ukiifungua biashara hiyo sehemu fulani, utapata wateja? Je biashara hiyo inahitajika mahali hapo?
Huwezi kufungua baa sehemu yenye vijiwe vya wahuni, watu wataogopa kuja kwa kuwa wanaogopa kukabwa! Huwezi kufungua duka sehemu isiyokuwa na nyumba zaidi ya kumi, unapoamua kufungua biashara, ni lazima uangalie sehemu na kisha ufanye ubunifu.
Hapo ndipo ambapo vijana wengi wamekuwa wakifeli, wengine wanaamua kuanzisha biashara ya mandazi sehemu ambayo kuna wauzaji wengi wa mandazi, je unapotaka kuanzisha biashara hiyo sehemu kama hiyo, unaweza kufanya ubunifu?
Kama unaweza, fanya ila kama hauwezi, achana nayo. Jirani anauza mandazi, na wewe hapa unaanzisha biashara ya mandazi, unahisi utaweza kupata wateja? Ni lazima ufanye ubunifu, yaani kama mtu anauza mandazi, angalia udhaifu wake, kama mandazi yake ni ya kawaida, yako yaweke hiriki, yako yafanye yawe makubwa, huo ndiyo ubunifu.
Kama unataka kuanzisha biashara ya chipsi, angalia udhaifu wa mwenzako. Yeye anauza chipsi bila mishikaki, wewe weka na mishikaki, kama anauza chipsi bila samaki, wewe weka na samaki. Siyo yeye hana samaki, na wewe huna, yeye hata soseji, na wewe huna, yeye hana mishikaki, na wewe huna, ni lazima ufanye ubunifu.
Sasa vijana wengi wa mjini wamekosa vitu hivyo na mbaya zaidi wengi wao hawataki kushaurika. Hili linawakosti sana na ndiyo maana wengi huanzisha biashara na kuanguka chini.
Kwa leo acha niishie hapa, natumaini vijana wa mjini mtafanyia kazi yale machache niliyoshauri. Asanteni.
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz