Leo nimeamua kuja na sababu zinazotokana na tafiti za wanaume kutokuwa waaminifu kwenye mahusiano na ndoa. Ikumbukwe kwamba sababu za wanawake kutokuwa waaminifu hazifanani moja kwa moja na sababu za wanaume, na hata kitendo chakutokuwa mwaminifu kwenye ndoa kwa mume au mke pia huathiri ndoa husika katika uzito tofauti.
Hii ni kutokana na sababu za kiasilia, kiuumbaji, kijinsia na kisaikolojia.
Zifuatazo ndizo sababu za wanaume wengi kuchepuka:
Kisasi.
Mara nyingi wanaume hutumia kitendo cha kutoka nje ya ndoa au nje ya mahusiano kama fimbo ya kulipiza kisasi kwa maumivu au hasira yoyote aliyokuwa nayo dhidi ya mpenzi au mke wake. Kwa mfano, wanaume wengi nilioongea nao binafsi, hususani wale ambao walikuwa wanalalamika kuwa mke wangu haniheshimu, mke wangu ananidharau, mke wangu hanisikilizi, mke wangu anafanya hivi au anafanya vile, wengi baada ya kuongea au kulalamika kwa muda mrefu pasipo kuona mabadiliko baadaye waliamua kuanza ku “cheat”.
Kisaikolojia, mwanaume anapochepuka kwa sababu ya kisasi, huwa inamwondolea ile hali ya kujishtaki au kushtakiwa nafsini kwamba amefanya kosa “guilty conscious” na hiyo inaweza kumfanya aendelee kuchepuka kwa muda mrefu tu, tofauti na mwanamke anapochepuka.
Ni vema ukachukua tahadhari hii, pale unapoona mume wako analalamika sana kuwa haumuheshimu, unamdharau, haumsikilizi, haushuki au kunyenyekea basi fahamu kwamba kunauwezekano mkubwa ameshaanza kuchepuka au yuko kwenye kuisoma ramani ili aanze. Kama kunauwezekano wa kubadili tabia na kushuhulikia hayo malalamiko yake ni bora ukafanya hivyo maana kifuatacho chaweza kuhatarisha mahusiano yenu.
Kujifariji kwamba kila mtu anafanya
Wapo wanaume wengi walioonyesha kuchepuka kwasababu tu ndani yao walikuwa wanakosa umaana wa kuwa waaminifu kwasababu wanaona hata wale watu ambao wao waliwaamini kwamba labda wanaweza kutochepuka na wao pia walichepuka, sasa mtu anasema kumbe kila mwanaume anachepuka, basi yanini kujibanabana wakati namimi ninahamu na fursa inaruhusu.
Kile kitendo chakuona wanaume wengi wanatabia ya kutokuwa waaminifu kudhoofisha mioyo ya wanaume wengine kwa kujifariji kwamba kumbe hichi kitu sio kipya, kila mtu anakijua na anafanya, chakujitahidi tu ni kutokugundulika. Pamoja na hayo wito wangu kwa wanaume wenye fikra hizi ni kwamba, kuwa kwako mwaminifu kwa ndoa yako hakutakiwi kuyumbishwa na tabia za wengine, usimtegemee mtu kukutengenezea misingi ya uaminifu wa ndoa yako, je kama kila mwanaume anampiga mke wake na wewe ndio uanze kumpiga? Kama kila familia inaugomvi, na wewe ndio utafute ugomvi hata kama hakuna mazingira ya ugomvi? La hasha.
Ifahamike kwamba, haijalishi ni sababu gani imemfanya mwanaume au mwanamke kuchepuka au kukosa uaminifu katika ndoa yake, madhara ya tabia hii yanaweza kuigharimu ndoa yako kwa kiasi kikubwa sana. Madhara yake yanaweza pia yasiishie kwenu ninyi wanandoa tu bali yakawaathiri hata watoto wenu. Wito wangu ni kila mwanandoa kuithamini na kuiheshimu ndoa yake kutoka ndani yamoyo na sio kinafiki.
No comments:
Post a Comment