Wapo wanawake ambao wameolewa lakini hawaoni hatari kuvaa kimitego bila kujali kuwa, kufanya hivyo ni kuiweka rehani ndoa……Kuna hili vazi la kanga moja ambalo baadhi ya wanawake wamekuwa wakipenda kulivaa hasa maeneo ya mjini, bila kujali ni mchana au usiku, kwenye nyumba ya kupanga au binafsi.
Hapo ndipo penye shida na leo nimeona nilizungumzie ili wale wenye tabia hiyo waache mara moja kama wanazitaka ndoa zao…..Niseme tu kwamba, ukiwa na mumeo chumbani wala sioni tatizo kumvalia kanga moja, wakubwa wanajua faida ya vazi hili katika kuidumisha ndoa.
Pia ikiwa mnaishi peke yenu, siyo hatari hata kidogo kuvaa kanga moja, akazurura nayo sebuleni, jikoni na sehemu nyingine za nyumba yenu. Nasema hivyo kwa sababu, kuvaa minguo kibao mbele ya mumeo naweza kusema ni ushamba, labda kama kuna baridi sana, unaumwa au hauko vizuri na mwenza wako. Kinyume chake unaweza kuvaa vazi hilo na ikawa ni chachu ya mambo yetu yalee.
Shida inakuja pale utakapovaa vazi hilo kisha kutoka na kwenda bafuni kuoga, mbaya zaidi uwe umejaaliwa umbile tata kama langu kisha kwenye nyumba unayoishi kuna wanaume kibao. Unadhani katika mazingira hayo ndoa yako itakuwa salama kweli?
Unadhani wapangaji wenzako watakuheshimu? Sidhani kama itakuwa hivyo. Kwa kuvaa kanga moja ni wazi utapata usumbufu mkubwa kutoka kwa wanaume wakware na wengi watakuona unatangaza biashara. Mumeo naye hawezi kufurahia hilo, labda awe ni miongoni mwa wale malimbukeni.
Naomba nihitimishe kwa kusema kwamba, unapoingia kwenye ndoa unatakiwa kujitofautisha kabisa na wale ambao wako ‘singo’.
Kanga moja ni vazi la kumvalia mumeo tena hasa chumbani.
Usijidhalilishe kuvaa nguo ambayo itakufanya utafsirike tofauti, udharaulike na kuonekana unatangaza biashara wakati una mume.
No comments:
Post a Comment