WACHEZAJI 13 HATALI LIGI KUU BARA MSIMU WA 2017/2018 - EDUSPORTSTZ

EDUSPORTSTZ

BREAKING

Wednesday, 20 September 2017

WACHEZAJI 13 HATALI LIGI KUU BARA MSIMU WA 2017/2018 WACHEZAJI BORA MSIMU WA 2017/2018
 Ikiwa ni mwanzo mwa msimu hii baadhi ya wachezaji wameanza kwa kasi ya ajabu kwa kuonesha juhudi binafsi katika kuhakikisha timu zao zinafanya vizuri msimu huu. Baadhi ya wachezaji hao ni kama;
Edusportstz
Aishi Manula ( Simba SC )

Dalili za kuendelea kutamba kama golikipa bora nchini mara tatu mfululizo zimeanza tena kuonekana ligi ikiwa bado mbichi. Huyu ni mlinda mlango namba moja wa Simba SC na timu ya Taifa Tanzania. Aishi amejiunga na Simba SC akitokea Azam FC msimu huu wa 2017-18. Akiwa Azam aliweza kuibuka kipa bora wa ligi kuu nchini mara mbili mfululizo kwa misimu ya 2015-16 na 2016-17. Tayari mpaka sasa amekaa langoni mwa Simba SC katika mechi za awali za ligi kuu na hajaruhusu goli lolote mpaka sasa. Licha ya uimara wa beki ya Simba SC lakini kipaji binafsi, uwezo na uzoefu vinambeba kipa huyu . Akiendelea hivyo si ajabu kuibuka kipa bora tena kwa msimu wa 2017-18.

Emanuel Okwi ( Simba SC )

Huyu ni mshambuliaji wa Simba SC akitokea klabu ya SC Villa nchini Uganda. Si mgeni wa ligi kuu Tanzania bara. Kwa nyakati tofauti amezichezea Simba na Yanga kabla ya msimu huu. Okwi amerudi Simba akiwa moto wa kuotea mbali kwenye safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo na ligi kuu kwa ujumla. Mpaka sasa Simba imecheza mechi tatu za ligi na yeye akicheza mechi mbili dhidi ya Ruvu shooting aliyopachika goli 4 peke yake Simba wakishinda 7-0 na mechi nyingine dhidi ya Mwadui FC aliyofunga goli 2 Simba wakishinda 3-0. Ameweza kupachika wavuni goli sita katika mechi mbili wastani ambao kwa zaidi ya misimu mitatu haujawahi kufanywa na mchezaji yoyote ligi kuu. Wafungaji bora msimu uliopita Saimoni Msuva wa Yanga SC aliyeuzwa Al Jadida ya nchini Morroco na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting, walinyakua zawadi na tuzo hiyo kwa goli 14 katika mechi 30 ikiwa ni wastani goli mbili katika mechi mbili lakini Okwi amekuja na wastani wa goli 3 kwa mechi moja . Safu za ulinzi za timu za ligi kuu ni lazima ziwe nae macho sivyo atavunja rekodi ya mfungaji bora wa ligi wa muda wote Mohamedi Hussein ' mmachinga ' aliyemaliza msimu kwa goli 26.

Pappy Tshishimbi ( Yanga SC )

Huyu ni kiungo mkabaji wa Yanga SC aliyesajiliwa msimu huu akitokea klabu ya Mbabane Swallows ya nchini Swaziland lakini ana uraia wa Jamhuri ya watu wa Congo. Katika mechi tatu alizocheza katika kikosi cha mabingwa hao watetezi wa ligi kuu nchini, ameonesha uwezo mkubwa wa kuimiliki safu hiyo nakusimama kama kikwazo kwa wapinzani wa Yanga kuitawala safu yao ambayo kwa misimu kadhaa ilikuwa na tatizo la kiungo.

Katsavairo Michelle ( Singida United )

Katsavairo ni mshambuliaji katika timu ya Singida United iliyopanda ligi kuu msimu huu akiichezea timu hiyo kwa mkopo toka Kaizer Chiefs ya nchini Afrika Kusini. Ni raia wa Zimbabwe na mwenye uzoefu mkubwa wa ligi ngumu kama ya nchini Afrika kusini ( PSL ). Ana goli mbili kibindoni lakini akionesha uwezo mzuri wa kucheza akiwa na sifa zote za mshambuliaji; nguvu, stamina na akili ya mpira . Anaweza kuwa mwiba mkali katika ligi akinuia kujiweka sawa na kurudi kwenye timu yake ya Kaizer akiwa katika kiwango bora au kuiwezesha Singida kubeba kombe la ligi kuu ili apate nafasi ya kucheza klabu bingwa msimu wa 2019.

Mbaraka Yusufu ( Azam FC )

Majeruhi yalimfanya kukosa maandalizi ya pamoja na kikosi cha Azam FC ambao wamemsajili kutoka Kagera Sugar alikowika vyema msimu uliopita . Huyu anacheza nafasi ya ushambuliaji na amebahatika kucheza mechi moja tu baada ya kutoka kwenye majeruhi na kuweza kutikisa nyavu dhidi ya kipa mkongwe zaidi kwenye ligi Juma Kaseja wa Kagera Sugar. Analijua vyema lango, nguvu , stamina na akili nzuri ya mpira . Msimu uliopita alimaliza ligi akiwa na magoli 11 huenda mwaka huu akaenda mbali zaidi akiwa na timu yenye wachezaji wengi wenye uwezo mzuri , huduma nzuri na benchi la ufundi lililokamilika kila idara.

Donald Ngoma ( Yanga SC )

Kwa jicho la haraka katika mechi tatu alizocheza wengi wanamuona amekuwa tofauti na misimu miwili iliyopita. Anacheza taratibu na kwa woga kidogo tofauti na yule Dombo Ngoma mwenye kasi , nguvu na purukushani nyingi. Haya ni mabadiliko ya kiufundi pia ya kisaikolojia ya mchezaji husika na bechi la ufundi la klabu yake . Ngoma aliumizwa vibaya msimu uliopita hali iliyomfanya kukaa nje kwa miezi mitano hii inamfanya kuwa na woga fulani wa kupambana na walinzi ( saikolojia ) lakini kwa mfumo wa Lwandamina wa sasa Ngoma hachezi kama mshambuliaji namba mbili kwa maana ya playmaker bali anacheza kama false 10 akisimama kama mshambuliaji kamili kificho wa kati na ndio maana ameweza kuifungia Yanga magoli mawili muhimu mpaka sasa. Muda mwingi Yanga ikiwa inashambulia hususanj kwa mashambulizi yanayotokea pembeni utamuona Ngoma anaingia kati na kujiweka vyema kwenye 18. Kupungua kwa kasi yake kumemfanya kuondokewa na kukamiwa na ndicho kitamfanya kufunga kirahisi.

Ibrahimu Ajibu ( Yanga SC )

Ni mshambuliaji wa Yanga SC aliyesajiliwa kutokea Simba SC , sitarajii sana kuibuka kama mfungaji bora wa ligi kuu lakini huyu ndio atakuwa mwiba mchungu kwa wapinzani wa Yanga . Anajua vyema kuiunganisha timu kutoka safu ya kiungo na ushambuliaji pia kusimama kama mshambuliaji namba mbili akiwa pia na uwezo wa kupiga mipira iliyokufa. Ni dhahiri Lwandamina anaujenga mfumo wa kushambulia wa timu hiyo kumzunguka mchezaji huyu na viungo wake wengine .

Peter Mapunda ( Majimaji )

Kitakachomuangusha kuwika msimu huu ni wastani wa jumla wa kikosi cha Majimaji katika uwezo wao kudumu katika ubora wao. Ni mshambuliaji ambaye anajiamini, kipaji halisi , nguvu na akili ya mpira . Akicheza mbele ya moja ya beki bora ligi kuu ya mabingwa watetezi wa ligi kuu Yanga SC , aliweza kumtia tumbo joto kocha mkuu wa mabingwa hao Lwandamina hali iliyomfanya kubadili mchezo kipindi cha pili katika mechi yao ya jumamosi iliyoisha kwa sare 1-1 akitupia goli lao nyavuni. Mapunda endapo kocha wa Majimaji atamuendeleza vyema na kumjengea viungo wazuri wa kumlisha mipira mizuri, kwa hakika anaweza kuisaidia timu hiyo.

John Bocco ( Simba SC )

Simba wamekuwa na kikosi kipana msimu huu. John Bocco moja ya washambuliaji wakongwe ligi kuu nchini akidumu kwa zaidi ya miaka tisa akiwa na Azam FC lakini msimu huu amesajiliwa na Simba SC. Alianza ligi na majeruhi hali iliyomfanya kukosa muda wa kutosha kujiweka sawa na wenzie. Muunganiko wake na Emanuel Okwi unaweza kuwa muunganiko hatari zaidi kwenye safu ya ushambuliaji msimu huu. Mechi ya jana dhidi ya Mwadui wote wakicheka na nyavu, ni mechi ambayo ilimrudisha vyema mchezoni mkongwe huyo . Uwezo wa Omog kuwatumia wote watatu pamoja na Nicholas Gyan akitokea wing ya kulia, kunazidi kuwafanya kuwa imara na ndicho ambacho kitamfanya Bocco kuwa tishio kwa uwezo wake wa kumalizia pasi za mwisho.

Mudathiri Yahya ( Singida United )

Huyu ni kiungo wa Azam FC anaeichezea Singida United kwa mkopo. Mudathiri ni mmoja ya viungo wakabaji wazuri kwenye ligi yetu kwa muda mrefu . Utitiri wa viungo Azam FC ulitaka kuua kipaji chake lakini toka atue Singida ameanza kurudi katika makali yake akiwa na goli moja mkononi bora dhidi ya Mbao FC waliposhinda 2-1. Huyu aliwahi kutakiwa na Yanga SC kutokana na umahiri wake hivyo si ajabu msimu huu kurudi tena katika ubora wake.

Eliudi Ambokile ( Mbeya City )

Mbeya city wamebomoka sana msimu huu wakipoteza idadi kubwa ya wachezaji wake tegemeo waliokuwa na timu hiyo msimu uliopita kama Zahoro Pazi aliyejiunga na Ndanda, Rafael Daudi Yanga, Ditram Nchimbi Njombe mji , beki wa kati Rajabu Zahir Ndanda na kiungo Keny Mwambungu aliyejiunga na Singida United. Msimu huu ni kama wanaanza upya na tayari wana mtu anaitwa Eliudi Ambokile ameonesha uwezo mzuri kwenye safu yao ya ushambuliaji akiwa na goli mbili mpaka sasa. Akitunzwa vyema anaweza kuwa msaada kwa timu hiyo.

James Kotei ( Simba SC )

Hii ni injini ya kiungo cha chini cha Simba SC. Raia huyu kutoka Ghana ni mmoja wa viungo wakabaji bora katika ligi kuu Tanzania bara na ndio maana sishangai kumweka nje mkongwe Jonasi Mkude. Ana uwezo mzuri wa kuwalinda walinzi wa kati pia kusimamia mfumo mzima wa timu wa kukaba , kutawanya mipira kwa pasi za uhakika pia kuvunja mipango ya wapinzani. Kotei ni mnyumbufu kucheza na viungo wenzake na mwepesi kung'amua mipango ya kushambulia ya wapinzani wake na kuitibua . Ni akiba pia kama mlinzi wa nyuma kati na pembeni.

Yahya Zayd ( Azam FC )

Bado hajatikisa nyavu mpaka sasa kinda huyu toka timu ya vijana ya Azam FC aliyepandishwa timu kubwa. Nauoana mustakabali wake mzuri kwenye ligi endapo benchi la ufundi la Azam FC litaendelea kumwamini na kumpa nafasi zaidi ya kucheza. Ana uchu wa kuitengeneza historia yake nzuri kisoka nchini ili katika umri wake mdogo aianze mapema safari ya soka la kisasa nje ya mipaka hii.

like facebook page yetu hapa kwa habari za uhakika

For Booking>>>CALL>>>

Voda: +255757441463

JIUNGE NAMI KUPITIA LINK HIZI